in ,

YANGA WAWATWANGA WATANI

 

Dar-es-salaam Young Africans wamewatwanga Simba Sports Club mabao mawili bila majibu kwenye mchezo wa raundi ya nne ya Ligi Kuu ya Vodacom jioni hii. Yanga walipata bao katika kila kipindi, bao la kwanza likifungwa kwa ustadi na Amisi Tambwe dakika chache kabla ya kipenga cha kuashiria mapumziko kupulizwa na Malimi Busungu akaongeza la pili kwenye dakika ya 79.

Simba waliutawala mchezo kuanzia dakika za mwanzoni za kipindi cha kwanza. Hata hivyo Yanga nao walijaribu kulikaribia lango la Simba na hatimaye usumbufu wa washambuliaji wao ukapelekea mlinzi wa Simba Juuko Murshid kuwa mchezaji wa kwanza kuingia kwenye kitabu cha mwamuzi baada ya kurambwa kadi ya manjano kwenye dakika ya 12 alipomwangusha Donald Ngoma.

Shuti la kwanza la mchezo likapigwa na Simba kwenye dakika ya 21 kupitia kwa mlinzi wao wa kushoto Mohammed Hussein. Hata hivyo shuti hilo halikulenga lango. Yanga nao walipiga shuti lao la kwanza kwenye dakika ya 22 lakini golikipa Peter Manyika akaudaka mpira ule dhaifu uliopigwa na Mwinyi Haji.

Simba wakajibu mapigo kwa mashambulizi mfululizo ambayo walinzi wa Yanga na golikipa wao walifanya kazi ya zaida kuyazuia. Kwenye dakika ya 28 ndipo Simba walipofanya shambulizi kali zaidi ambapo Hamis Kiiza alipokea pasi safi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto na kupiga shuti zuri lililopanguliwa vyema na Ally Mustafa na kuzaa kona.

Dakika mbili baadaye nahodha Mussa Hassan Mgosi akapata nafasi ya kupiga kichwa ambacho kilipaa juu ya lango. Kwenye dakika ya 44 Amis Tambwe akaipatia Yanga bao la kwanza baada ya kutulia na kupiga shuti zuri ingawa alikuwa amezungukwa na walinzi wa Simba. Kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga wakiwa mbele kwa bao moja dhidi ya Simba ambao waliutawala mchezo zaidi na kupiga mashuti mengi zaidi.

Kwenye kipindi cha pili Yanga walionekana kuutawala mchezo zaidi hasa eneo la katikati kupitia viungo wao Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima. Kocha wa Simba Dylan Kerr akaamua kumtoa nahodha Mussa Hassan Mgosi kwenye dakika ya 62 ya mchezo na kumuingiza Ibrahim Ajibu.

Hata hivyo hakuna timu iliyoweza kufanya shambulizi lolote kali mbaka kufikia dakika ya 79 ambapo Malimi Busungu aliwapatia Yanga bao la pili baada ya walinzi wa Simba kushindwa kuuondosha kwenye eneo la hatari mpira uliorushwa kwa nguvu na Mbuyu Twite.

Mpira uliendelea mashambulizi kadhaa yakifanywa na timu zote mbili lakini nafasi ya wazi kuliko zote ikaja kwenye dakika ya 88 ambapo Awadhi Juma alibakia na mpira ndani ya 18 golikipa akiwa hayupo langoni lakini akashindwa kufunga bao ambalo lingeweza kuwapa Simba morali ya kutafuta bao la kusawazisha.

Dakika tisini zikamalizika na mwamuzi akaongeza dakika 7 ambazo zilimshuhudia Mbuyu Twite akionyeshwa kadi mbili za manjano na kutolewa nje ya uwanja. Kwa matokeo haya Yanga wameendelea kujikita kileleni wakiwa na alama 12 baada ya kushinda michezo yote minne.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JURGEN KLOPP ANAHITAJIKA ANFIELD

Tanzania Sports

Man U kileleni, Arsenal safi