in , , ,

YAFUATAYO NI MAKOSA YA BAKAYOKO

Msimu jana Antonio Conte alikuwa anatumia mfumo wa 3-4-3, mfumo ambao
ulimpa uhuru wa kuwatumia Kante na Matic kama viungo wa kati.

Matic alicheza kama box to box midfielder na alifanikiwa kupiga pasi
za mwisho za magoli zaidi ya saba katika ligi kuu ya England peke
yake.

Baada ya msimu jana kuisha, Antonio Conte aliamua kumuongeza Bakayoko
kutoka Monaco na kumwachia Matic kwenda Manchester United.

Bakayoko alikuja Chelsea kukiwa na matumaini makubwa sana ya yeye
kufanya vizuri kulingana na kiwango chake kizuri alichokionesha akiwa
na Monaco.

Lakini tofauti na matumaini makubwa ya watu wengi, Bakayoko amekuwa
mchezaji ambaye ana kiwango cha chini sana. Amekuwa akionesha makosa
mengi ndani ya mchezo. Yafuatayo ni makosa ya kiufundi ambayo Bakayoko
amekuwa akiyafanya ndani ya uwanja.

Msimu jana Antonio Conte alikuwa anatumia mfumo wa 3-4-3, lakini msimu
huu alibadirika na kuanza kutumia mfumo wa 3-5-2, mfumo huu
unamwezesha kuanza na viungo watatu wa kati, mara nyingi huwa
wanacheza Kante, Bakayoko na Fabregas/Drink-Water. Katika mfumo huu
Bakayoko hucheza kama box to box midfielder.

Eneo ambalo humtaka yeye kutimiza majukumu ya kukaba na kushambulia
kwa pamoja, hutakiwa kurudi nyuma kukaba na kwenda mbele kushambulia.

Lakini kila anapokuwa anaenda kushambulia huwa anamakosa mengi na
anapokuwa anarudi kukaba huwa anafanya makosa.

MAKOSA ANAYOYAFANYA WAKATI WA KUKABA.

Covering, mara nyingi timu inapokuwa inakaba, moja ya wachezaji ambao
huhusika kwa ajili ya kukaba katika eneo la nyuma ni Bakayoko.

Kuna wakati hajui kusimama sehemu sahihi ambayo itamsaidia kutimiza
majukumu yake ya kukaba vizuri, mfano kuna wakati akiwa nyuma, unaweza
kuta beki wa kati ametoka kwenda kumkaba mpinzani hivo huacha nafasi
yake nyuma wazi, ambapo inahitajika mtu aje kuziba nafasi yake (ku
cover), mazingira kama haya Bakayoko huwa anajikuta amesimama sehemu
ambayo hatakiwi kuwepo na kushindwa kwenda kuziba (ku cover) nafasi ya
beki aliyeondoka kwenda kumkaba mpinzani.

Tackles, moja ya kitu ambacho Bakayoko hakifanyi vizuri wakati wa
kukaba ni kufanya tackling na hii ni kwa sababu ya aina yake ya
uchezaji. Mara nyingi hukimbia nyuma ya mpinzani hivo anapojaribu
kufanya tackling akitokea nyuma ya mpinzani hujikuta anafanya
madhambi.

MAKOSA ANAYOYAFANYA WAKATI WA KUSHAMBULIA.

Kushinda kukaa na mpira, mara nyingi anapokuwa anapewa pasi hujikuta
hawezi kutuliza vizuri hali inayofanya kupoteza mipira virahisi, na
kila anapopoteza mipira virahisi husababisha timu yake ipoteze umiliki
wa mpira, na timu inapopoteza umiliki wa mpira inakuwa imevuruga
mipango yake ya kushambulia. Kitu kikubwa ambacho huwa kigumu kwake
hapa ni ule mpira wake wa kwanza anaoupokea kutoka kwa mchezaji
mwenzake wa Chelsea, ambapo hushindwa kuhold vizuri na kujikuta
amepokonywa mpira ule.

Kupiga pasi ambazo hazina macho. Bakayoko anawastani wa kupoteza pasi
kuanzia 7-9 katika mchezo mmoja, na katika mechi iliyopita dhidi ya
Watford kwa dakika 30 alizocheza alipoteza pasi 7. Kitu ambacho ni
kibaya kwa mchezaji ambaye anacheza katika eneo la kiungo kwa sababu
yeye ndiye anayetakiwa kuwa mchezaji ambaye ubunifu wa mashambulizi
yanatokea kwake. Timu haiwezi kuwa na ubunifu wa kutengeneza
mashambulizi kama kiungo wake wa kati anapiga pasi ambazo zinapotea
mara nyingi.

Dhaifu la mwisho la Bakayoko katika jukumu la kushambulia ni umaliziaji hafifu.

Amekuwa anakosa utulivu anapotakiwa kufanya umaliziaji hali ambayo
inamsababisha akose nafasi nyingi za ufungaji wa magoli na wakati
mwingine amekuwa hapigi vizuri pasi za mwisho kwa sababu ya kukosa
ƴutulivu. Mpaka sasa amecheza michezo 35 na akiwa amefunga magoli 3 na
kutoa pasi 3 za mwisho, takwimu ambazo ni za chini ukilinganisha na
eneo analocheza, takwimu ambazo zimemfanya azidiwe na Marcos Alonso na
Cesar Azpilicueta ambao ni mabeki.

Marcos Alonso amecheza michezo 34 na kufunga magoli 7 na kutoa pasi 2
za mwisho, wakati Cesar Azpilicueta amefunga goli 2 na kutoa pasi 6 za
mwisho.

Mara nyingi mashabiki humfurahia mchezaji anapofanya vizuri, hawana
uvumilivu kipindi mchezaji anapokuwa anafanya vibaya. Hivo Bakayoko
anatakiwa afanye jitihada kubwa kurudisha kiwango chake, msimu huu ni
wa kwanza kwake katika ligi kuu ya England ana muda wa kuzoea zaidi na
kufanya vizuri.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

LUIS ENRIQUE NI MTU SAHIHI KWA CHELSEA, ILA CHELSEA SI MAHALA SAHIHI KWAKE

Tanzania Sports

MSIMU MZURI KWA BARCA MPAKA SASA, ILA UNAWEZA KUHARIBIWA NA CHELSEA