in , , ,

Walcott kiwango, kazi kwa Arsenal

*Lampard awafufua Chelsea, QPR haibebeki

*Reading, Southampton na Aston Villa kifoni

Mwaka 2012 umehitimishwa katika soka ya Ligi Kuu England (EPL) kiaina, kubwa likiwa kishindo cha Theo Walcott.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England ambaye kuanzia Januari yupo huru kujadili mkataba na klabu za nje ya nchi, alionesha umahiri wake katika kushambulia na kufunga.

Mwenyewe alifunga mabao matatu kati ya saba timu yake iliyowafunga Newcastle United Jumamosi hii, akicheza nafasi ya ushambuliaji wa kati anayoipigania.

Arsene Wenger anasema ameonesha kuimudu nafasi hiyo, Walcott mwenyewe anasema amefurahi na anahisi kuna makubaliano yatafikiwa hivi karibuni.

Arsenal isipomfunga kwa mkataba mpya au kumuuza Januari hii, ataondoka bure kiangazi kijacho.

Katika mechi hiyo kali kwenye uwanja wa Emirates, magoli mengine mawili ya Arsenal yalifungwa na Olivier Giroud na Lucas Podolski. Yale ya Newcastle yalifungwa na Demba Ba na Sylvain Marveaux.

Ba alikuwa anatajwa kuhamia Arsenal, lakini kumbe analenga kujiunga Chelsea na alitaraji kufanya mazungumzo nao jioni ya Jumapili hii.

Walcott aliwakumbusha washabiki zama za Thierry Henry aliyekuwa uwanjani hapo pia, huku wakilitaja jina lake na kuitaka klabu yao imsainishe haraka mkataba wa muda mrefu.

Kwa ushindi wa Jumamosi, Arsenal wamepanda hadi nafasi ya tano, wakiwa na mechi moja mkononi, ambayo wakishinda wanaweza kutulia nafasi ya nne. Watawavuka Tottenham Hotspurs na kubaki nyuma ya Manchester United, Manchester City na Chelsea wenye mchezo mmoja mkononi pia.

Chelsea chini ya Rafa Benitez wameendelea kufufuka, ambapo katika mechi ya Jumapili hii dhidi ya Everton, nguvu ya kaimu nahodha, Frank Lampard iliwasaidia.

Chelsea waliotangulia kufungwa bao moja, walisawazisha na kuweka la ushindi kupitia kwa Lampard anayetarajiwa kuondoka mwisho 2013 mkataba wake unapomalizika.

Lampard alikuwa majeruhi kwa muda mrefu, na kurejea kwake kumekuja huku nahodha John Terry akirudi benchi kwa sababu hiyo hiyo, na Chelsea kwa muda ilikuwa imenyong’onyea.

Hiki kilikuwa kipigo cha kwanza kwa Everton nyumbani kwao Goodison Park, lakini pia kimepunguza nguvu ya kupigania nafasi ya nne.

Spurs walicheza kwa nguvu dhidi ya Sunderland na kuishia kushinda mabao 2-1 na ndio wanashikilia nafasi ya nne.

IMG_0133

Kikosi hicho cha kocha Mreno Andre Villas-Boas kinasheheni nyota wengi, kwani harakati za usajili wakati wa kiangazi zilikuwa kubwa, hivyo haitarajiwi kusajili wengi katika dirisha hili dogo.

Liverpool wamecheza bila kocha wao Brendan Rodgers kuwa uwanjani, kwani yupo kitandani kwa ugonjwa, lakini waliwasasambua Queen Park Rangers (QPR) mabao 3-0.

Ushindi huo umewapandisha Liverpool hadi nafasi ya tisa, jambo ambalo halikutarajiwa, kutokana na jinsi walivyoanza ligi vibaya.

Moja ya malalamiko ya Rodgers yamekuwa kukosa mshambuliaji wa uhakika, kwani ni Luis Suarez tu anayetambuliwa kwa uandamizi wake dimbani.

Ni yeye pia aliyefunga mabao mawili katika mechi ya Loftus Road Jumapili hii, na lile la tatu likifungwa na Daniel Agger. Tayari mipango imekamilika kumtwaa Daniel Sturridge wa Chelsea kupitia dirisha dogo.

Kama kuna kocha anayeugulia vibaya, ukiacha Harry Redknapp wa QPR, basi ni Paul Lambert wa Aston Villa ambaye baada ya kucharazwa na Chelsea mabao 8-0 , kisha kutunguliwa na Spurs 4-0 ilikuwa aibu kukung’utwa tena na Wigan 3-0. Imebaki pointi moja kutoka eneo la kushuka daraja.

Matokeo mengine mwishoni mwa wiki yalikuwa Swansea kuwalaza Fulham 2-1; Manchester United kushinda kwa mabao mawili bila dhidi ya West Bromwich Albion na Manchester City kuwafunga Norwich City mabao 4-3.

Reading walizinduka usingizini japo wengine wanasema ni kukosa kwao bahati kwa kuwachapa West Ham United 1-0; Stoke City wakaendeleza mazoea yao ya sare dhidi ya Southampton walipotoka 3-3.

Mechi za Jumamosi na Jumapili hii zimezalisha mabao 41, lakini kinachoonekana ni timu nyingi kuwa dhaifu katika ulinzi.

Manchester United, kwa mfano, wamefunga mabao 50, lakini wameruhusu mabao 28 kutinga kwenye nyavu zao.

Katika mechi 20, Fulham wamefungwa mabao 36; Aston Villa 39; Southampton 37 na Reading 37 katika idadi hiyo hiyo ya mechi.

Kwa hali inavyokwenda, haielekei kwamba kuna klabu itakayosogelea rekodi ya Chelsea ya msimu wa 2004/5 ya kuruhusu mabao 15 tu. Hata Chelsea wenyewe hawawezi, maana wameshafungwa mabao 18 katika nusu ya kwanza ya mechi za EPL.

Kubwa linalosubiriwa sasa ni usajili wa dirisha dogo, ambapo kuna wachezaji, makocha na hata wamiliki wanatembea na siri moyoni.

QPR wanashika mkia kwenye msimamo, wakifuatiwa na klabu mbili zilizopanda daraja msimu huu za Reading na Southampton na juu yao wapo Aston Villa, Wigan, Newcastle na Fulham.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Man U waendeleza mchezo wao

Let 2013 be a much better sporting year in Tanzania