in ,

Unai anamuhitaji Ozil au Ramsey?

Kuna vitu vingi sana kwa sasa vinatokea katika klabu ya Arsenal, vitu ambavyo mwisho wa siku vinabakiza maswali mengi sana.

Najua kwa sasa wako katika kipindi cha mpito, kipindi ambacho kinahusisha mabadiliko mengi ndani ya timu.

Baada ya miaka 22 ya utawala wa Arsene Wenger, ililazimika muda umpe nafasi Unai Emery avae viatu vya mzee Wenger.

Mzee ambaye amefanya vingi vikubwa sana ndani ya Arsenal. Huwezi kumdharau kutokana na mwisho wake pale Arsenal.

Sawa mwisho wake ulikuwa mbaya sana pale Arsenal ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambacho alikuwa anahudumu katika timu hii.

Kwenye kipindi chake alifanya vingi, aliwapa nafasi vijana, akawaamini na kwa kiasi kikubwa hawakumwangusha.

Kuna wakati alikuwa anasimama kama baba mzazi kwa baadhi ya wachezaji ambao alikuwa anawaamini sana.

Wakati ambao mashabiki wanarusha makombora kwa mchezaji fulani, Arsene Wenger alisimama kama mlinzi.

Alihakikisha mchezaji husika aliathirike na kitu chochote kibaya, alitaka mchezaji husika afikirie kuhusu kucheza mpira tu.

Moja ya wachezaji ambao walikuwa kipenzi kikubwa cha Arsene Wenger hasa hasa kwenye siku za mwisho za utawala wake walikuwa ni Mesut Ozil na Aaron Ramsey.

Hawa aliwalea sana kama yai, aliwatetea sana na kuwaamini sana. Alikuwa anaamini sana kupitia miguu yao.

Kuna wakati walikuwa wanafanya vibaya uwanjani lakini yeye alisimama kifua mbele kuwakinga na kila mashambulizi yaliyokuwa yanakuja kwao.

Aliwapa nafasi kila muda, na aliwapa majukumu makubwa sana ndani ya uwanja. Kuna wakati Aaron Ramsey akikuwa anaandaliwa kuwa nahodha.

Huyu ndiye alikuwa Arsene Wenger, kocha ambaye alikuwa na malezi ya babu kwa wachezaji wake. Malezi ambayo wachezaji walikosa hamasa ya kushinda.

Wachezaji wengi walibweteka ndani ya mikono ya Arsene Wenger. Hakukuwepo na ile hamasa ya mchezaji kupigana, hata alipokosea hakukemewa.

Nyakati kwa sasa zimebadilika, Arsene Wenger hayupo tena, Unai Emery ndiye kiongozi wa jahazi la Arsenal.

Kiongozi ambaye anaonekana hana masihara hata kidogo, kwake yeye ukicheza vibaya ni jambo la kawaida kukurudisha benchi.

Tangu amekuja wachezaji hawa wawili (Mesut Ozil na Aaron Ramsey) wamekuwa na wakati mgumu sana chini ya Unai Emery.

Hajawapa nafasi kubwa sana, na ni kitu cha kawaida kwake yeye kuwaweka kwenye benchi. Haogopi wala kuhofia kitu chochote.

Ndiyo maana unamuona hana hata haraka ya kumshawishi Aaron Ramsey kusaini mkataba mpya, haogopi kuo doka kwa Aaron Ramsey.

Hana hofu yoyote kuhusu kumweka benchi Mesut Ozil. Utaanzaje kumweka benchi mchezaji anayelipwa zaidi kuliko wachezaji wote kwenye ligi juu ya England ?

Kwake yeye ni jambo la kawaida sana. Tena sana, Mesut Ozil anakaa benchi, Aaron Ramsey anakaa benchi pia.

Lakini wote kwa pamoja wanatuachia swali moja tu, nani anastahili kuendelea kuwepo Arsenal?

Kwangu mimi naona Aaron Ramsey ni mtu sahihi kubaki kwenye kikosi cha Unai Emery , kwanini nasema hivo ?

Unai Emery hutaka timu yake icheze kwa kukabia juu, na inapopoteza mpira kila mchezaji afanye mgandamizo wa kupata mpira (pressing).

Kufanikisha hiki lazima uwe na mchezaji ambaye ana kasi, na mwenye uwezo wa kukimbia umbali mrefu ndani ya uwanja.

Aaron Ramsey ana uwezo mkubwa sana wa kukabia juu pia na kufanya mgandamizo kwa timu pinzani kipindi timu yake imepoteza mpira.

Hachoki, ana nguvu ya kukimbia umbali mrefu ndani ya uwanja. Kitu ambacho hakipo kabisa kwa Mesut Ozil.

Mesut Ozil ni mzuri sana akiwa na mpira kwa kutengeneza nafasi, tofauti na Aaron Ramsey ambaye ana faida kubwa akiwa na mpira na akiwa hana mpira.

Pia Aaron Ramsey ana uwezo wa kuunganisha safu ya ushambuliaji na safu ya kiungo. Kwa kuwa na uwezo wa kutokea katikati kwenda mbele.

Hata timu ukiwa chini Aaron Ramsey ana uwezo mkubwa wa kukimbia kutoka juu kwenda chini ,na kutoka chini kwenda juu.

Hii ni tofauti kabisa na kwa Mesut Ozil. Kwa hiyo kwangu Mimi Aaron Ramsey ana manufaa makubwa kwenye mfumo wa Unai kuzidi Mesut Ozil.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Simba hawakujifunza kwenye mechi ya SOURA na Al Ahly

Tanzania Sports

Kumbe JOSE MOURINHO alishindwa kuishi na wachezaji wa ‘INSTAGRAM’