in , , ,

Tunahitaji Kumbukumbu Sahihi za miaka ya nyuma kwenye soka…

Ofisi za TFF
TANZANIA ni nchi ya watu tunaojua sana kucheza na maneno. Watanzania ni wajenga hoja wazuri sana wa mambo karibu yote yanayohusu maisha yetu, lakini tukija kwenye utekelezaji hamna kitu!
Watanzania watasema sana kuhusu kuinua michezo, nchini lakini linapokuja suala la utekelezaji wake, hawana maandalizi ya soka ya vijana. Hawana mkakati wa shule za soka (soccer academies) lakini wanataka lazima wawafunge Waganda wenye ‘soccer academies’ 140 zilizosajiliwa.
Kwa wanaonifahamu vizuri huko nyumbani, wanafahamu fika kuwa soka haukuwa mchezo wangu wa kwanza, daima volleyball ndio umekuwa mchezo wangu, na hata kufikia kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Volleybal Tanzania (TAVA), na kuwa mwalimu wa ngazi ya kimataifa, hivyo linapokuja suala la soka, ni lazima niwaulize wahusika.
Mara nyingi huwasiliana kwa simu na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah,  Rais wake, Leodeger Tenga, mdau muhimu ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, Leonard Thadeo, Muharam mchume, Sunday Manara, Abdalah Kibaden, John Zambetakis, Patrick Sombe, Ibrahim Mkamba, Muhidin Michuzi na wengi wengine ili kujua ukweli wa mambo, hasa ukitilia maanani kwamba mimi ni ‘wa kuja’ Dar, toka Dodoma.
Watanzania tunajua kweli mambo ya soka ya kimataifa, watakueleza vizuri kuhusu habari za wanasoka wa kimataifa lakini usishangae leo kusoma kwenye gazeti la hapo nyumbani Tanzania kwamba mara ya mwisho Yanga na Simba kukutana, Yanga walishinda 2-1!
Watanzania hawajali usahihi wa habari. Jamani, juzi tu Yanga na Simba wamecheza na Simba kulala 2-0, tumeshasahau!
Mwambie mchezaji wa zamani wa Tanzania akutajie aliocheza nao mechi ya usiku ya kukumbukwa kati ya Tanzania na Kenya ya kombe la Challenge mjini Nairobi mwaka 1983 ambapo Kenya walipelekeshwa mpaka taa kuzimwa uwanjani.
Atamtaja Sunday Manara wakati mchezaji huyo tayari alishakuwa mwenyeji wa miaka saba Uholanzi mwaka huo alikokuwa akicheza soka ya kulipwa tangu mwaka 1976!
Vinginevyo, anaweza kumtaja mchezaji ambaye wakati huo hata kujulikana alikuwa bado, kama Abubakar Salum ‘Sure Boy’ wa Yanga, baba yake Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam ! Unajiuliza, inakuwaje mchezaji mwenyewe aliyeshiriki mechi hakumbuki jambo alilopaswa kukumbuka? Anasahau vipi kwamba anayemtaja hakuwapo naye uwanjani?
Ufumbuzi wa tatizo hili ni kuwa na kumbukumbu za matukio mengi kwenye tovuti ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ili tusiwe watu wa kupapasa papasa kumbukumbu za kisoka za miaka ya nyuma na katika kupapasa papasa huko tukajikuta tunakosea sana.
Hebu fikiria, mtangazaji mmoja wa redio huko nyumbani alimuuliza mchezaji maarufu wa zamani wa Simba kwamba Simba ilishindaje ubingwa wa kwanza wa Afrika Mashariki Januari 1974 jijini Dar es Salaam.
Mchezaji huyo aliyechangia sana ubingwa ule, akamjibu hakumbuki chochote kabisa! Inawezekana hakumbuki hata kuchukua ubingwa huo mwaka huo!
Yule mtangazaji asingekuwa na haja ya kuuliza kama angekuwa na uhakika wa kupata jibu hilo kwenye tovuti.
Mwaka 1974 ni mbali sana; muulize mwana Yanga aliyeshiriki kwa namna moja au nyingine kuiingiza timu hiyo kwenye robo fainali ya kwanza ya mfumo wa ligi ya mabingwa mwaka 1998 timu hiyo iliingiaje hatua hiyo na matokeo ya mechi zake yalikuwaje kwenye ligi hiyo ya nane bora, utachoka.
Muulize hata mwana Simba swali hilo hilo kwa mashindano hayo hayo na hatua hiyo hiyo mwaka 2003,utashangaa. Yote hii ni kwa sababu hatuweki kumbukumbu sahihi, kamili na makini.
Hebu fikiria, kocha Bert Trautmann anafariki dunia na wasifu wake kutolewa. Huyu alifanya kazi nchini mwetu 1975 na waliokuwa dimbani wakati huo kwenye timu ya taifa wanakumbuka sana jinsi alivyokuaa nao bega kwa bega kwenye shughuli ya soka.
Leo hii kumbukumbu za TFF zinasomeka mahali kwamba alikuwapo nchini miaka ya 1960! Maajabu makubwa haya.
Ndiyo maana haishangazi kusoma kwamba timu yetu ya taifa ilipelekwa kwenye fainali pekee ya mataifa ya Afrika enzi zile na kocha mtanzania Joel Bendera, wakati ukweli Bendera alikuwa msaidizi wa kocha Mzungu aliyeitwa Wolk. Nani anajali? Kumbukumbu ziko wapi?
Je wangapi wanamkumbuka yule Mjerumani mtaalamu sana wa soka aliyepuuzwa na FAT akiwa nyumbani Tanzania kutuinua kisoka aliyeitwa Pape?
Tumeshamsahau, ingawa alikuwapo hapo nyumbani Tanzania akisoteshwa na FAT kati kati ya miaka ya 1990 tu! Hatuna kumbukumbu.
Wakati umefika sasa kwa TFF kuanza mkakati mpya wa kukusanya taarifa sahihi za matukio ya zamani ya soka na kutengeneza tovuti yenye kumbukumbu sahihi.
Kuna njia nyingi za kuanzisha mkakati wa kupata matukio sahihi ya nyuma ya soka. TFF inaweza kuanzisha kongamano la wadau  kujadili njia za kupata matukio hayo sahihi kama kwa njia ya kutoa mashindano maalumu ya kuandika matukio mengi yatakayochaguliwa kwa washindi kupewa zawadi.
Yawezekana kuchimba kutoka maktaba za Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC (zamani RTD), Uhuru na Mzalendo, Daily News, Sunday News na HabariLeo na popote taarifa hizo zitakapopatikana.
Inafaa kuanzia sasa TFF iweke kanuni kuzitaka klabu ziweke kumbukumbu za wachezaji wao na mechi zao kama idadi ya mechi mchezaji anazocheza klabuni, magoli kila mchezaji anayofunga kwa mechi za mashindano na za kirafiki.
Kadhalika irekodiwe vyema kadi za njano na nyekundu kwa mechi zote za kirafiki na za mashindano, penati wanazopiga na kupigiwa na kadhalika huku TFF nayo ikiweka yenyewe kumbukumbu hizo kwa mashindano inayosimamia.
Hayo ni kama ligi zote za klabu, kombe la taifa na ngao ya jamii pamoja na mashindano ya marika mbalimbali na mechi za timu zote za taifa za marika yote na ya wanawake.
Ni vizuri TFF ikalipa uzito mkubwa suala hili, kwani dunia ndivyo inavyoenda na ni wazi sasa timu kubwa zitakuwa zikiwafuatilia wachezaji kwa ‘scouting’ na kuangalia kumbukumbu zao kwenye tovuti.
Kukosekana kwa hilo la pili kutachangia kuwaangusha wachezaji wetu. Hebu TFF iyatafakari maoni haya, kuyafanyia kazi kwa kutumia kila mbinu kukusanya kumbukumbu sahihi, angalau za tangu tulipopata uhuru mpaka sasa. Za zamani zitafutwe kutunzwa na za sasa ziwe zikichukuliwa kutunzwa.                                                 
Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Manchester United Ngao ya Jamii

KAMATI KUTANGAZA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF