in , ,

STARS IMETUMIA LESO YA MCHANGA KUTUFUTA MACHOZI

Nyuso zetu zimejaa furaha, furaha ya muda mfupi. Furaha ambayo
imetusahaulisha kila tatizo lililopo katika familia yetu.
Familia yetu ina matatizo mengi sana, matatizo ambayo hayawezi
kuondolewa na furaha ya siku moja

Tunajaribu kujificha nyuma ya shina la mchicha tukiiamini kuwa
hatutoonekana, tunakosea sana kujaribu kujifuta machozi kwa leso ya
mchanga.

Matatizo yetu hayawezi kusahaulika kwa ushindi dhidi ya DR Congo, sawa
ni timu bora kuzidi sisi, ina wachezaji wengi wanaocheza katika ligi za
ulaya na kizuri zaidi inashika nafasi ya tatu kwenye ubora wa CAF.

Tumempiga kofi mbabe, hii haiaminishi tumeshafikia hatua ya kupigana
na kila mbabe. Tusicheke na kufurahia sana mpaka tukasahau
kumtengeneza mtoto atakayekuwa shujaa wa Taifa letu.

Mtoto ambaye atakuwa na malezi mazuri kuanzia chini mpaka atakapokua
mkubwa tayari kwa kukipigana.

Mtoto huyu haji hivi hivi, ila kuna njia ambazo zinatakiwa
kutengenezwa ili yeye apite mpaka awe mbabe kati ya wababe waliopo
Afrika na duniani kwa ujumla

Turudi kwenye azimio la Bagamoyo, ambalo sisi wenyewe tulioona linafaa
kwa sababu lilikuwa na mikakati ambayo ingetusaidia sana katika mpira
wetu.

Timu ya Taifa ya DRC

Miaka kumi na moja (11) tangu azimio hili lifikiwe lakini
hatujafanikiwa kutekeleza hata robo ya vitu ambavyo tuliazimia katika
azimio la Bagamoyo la mwaka 2007

Nilifurahia sana niliposoma kurasa iliyokuwa imeandikwa kuziagiza timu
zote za ligi kuu kuwa na timu za vijana zilizo na umri wa chini ya
miaka 14, 17 na 20.

Nilioona picha kubwa sana katika maendeleo yetu ya mpira kwa sababu
mkondo huu wa kuwa na timu za vijana ulikuwa mkondo ambao ungepitisha
maji ya vipaji vya soka kwa muda mrefu.

Nilijua ni wakati mzuri kwa TFF kuwa na ligi imara na iliyopangiliwa
vizuri ili kuwapa nafasi vijana hawa kushindana. Matumaini
yaliongezeka kwa kiasi kikubwa moyoni mwangu.

Nilijua kabisa mwanzo ungekuwa mgumu sana kwa sababu ya gharama za
uendeshaji wa ligi kama hizi , lakini kuna kitu kilikuja kunifariji
moyoni mwangu, kama TFF waliazimia mpango huu na wakauona mpango huu
una manufaa makubwa basi watasimama kwenye kila hali mpaka pale mambo
yatakapokuwa mazuri.

Hakuna mfanyabiashara asiyependa kuwekeza sehemu ambayo anaona ina
manufaa makubwa kwenye biashara yake. Nilitegemea TFF wangetengeneza
mazingira ya kuziuza ligi ya vijana hata kama ingechukua muda wa miaka
mitano bila kupata mtu wa kuzinunua lakini kuna siku wangefanikiwa,
mipango ya muda mrefu ya kibiashara ilihitajika kufikia hatua hii.

Hatua ambayo isingekamilika kama vilabu visingekuwa na timu hizi za
vijana, timu ambazo zingetunzwa na kulelewa katika misingi mizuri ya
mpira, misingi ambayo ingetuwezesha tupate wachezaji waliotoka katika
mkondo mzuri.

Hatukufanya hivo, tukalipuuzia azimio la Bagamoyo ambalo liliwekwa na
Leodigar Tenga. Kila kiongozi aliyekuja baada ya Tenga aliendelea
kulipuuzia azimio hili.

Tumekuwa na viongozi ambao wanaamini katika wao, hawaamini katika
mipango endelevu imara. Ni ngumu kumuona kiongozi akifanya kitu
endelevu ambacho kilianzishwa na mtangulizi wake.

Miaka ilikimbia FIFA wakatuletea Club Licence , kitu ambacho
kinaendana sana na Azimio la Bagamoyo.

Vitu vilivyokuwepo kwenye azimio la Bagamoyo ndivyo hivo vilivypkuwepo
kwenye Club Licence. Vilabu vilitakiwa kuwa na timu za vijana, viwanja
vya uhakika vya mazoezi na uwanja wa kuchezea, vifaa vya michezo kama
jezi na Gym.

Lakini tulipuuzia, inawezekana ni ngumu kwetu sisi kumiliki Gym
kutokana na uchumi wetu, lakini siyo ngumu kwetu sisi kufanya biashara
na wamiliki wa Gym ili pande zote zinufaike, timu inufaike na mwenye
GYM anufaike kwa kutangaziwa biashara yake.

Akili ya kibiashara haipo ndani ya viongozi wetu ndiyo maana kila kitu
tunakiona ni kigumu kukitimiza kwa kiwango bora.

Wakati tukifurahia ushindi dhidi ya DR Congo tusisahau kuwa mpira wetu
uko gizani tunahitaji taa ya kuliondoa giza hili na taa pekee ni
kurudi katika misingi ya kisasa ya mpira, misingi ambayo itatusaidia
kuzalisha wachezaji imara watakayoisaidia timu yetu ya Taifa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

GHAFLA NIMEPAKUMBUKA GEZA ULOLE NA BUNJU ARENA

Tanzania Sports

WACHEZAJI GANI WANA UHAKIKA WA NAFASI KWENYE XI YA ENGLAND YA KOMBE LA DUNIA?