in , , ,

STARS YALAZIMISHWA SARE

 

 

Timu ya taifa ya Tanzania imelazimishwa sare ya 2-2 dhidi Algeria jioni hii katika Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018.

Stars ilipata mabao yake kupitia kwa Elias Maguli katika dakika ya 43 na Mbwana Samatta katika dakika ya 54 huku mabao yote ya Algeria yakifungwa na Islam Slimani kwenye dakika za 72 na 75.

Taifa Stars waliuanza mchezo huo kwa mfululizo wa mashambulizi na mapema katika dakika ya 2 Mbwana Samatta alipokea pasi nzuri kutoka Thomas Ulimwengu lakini akapiga shuti lililopaa.

Nafasi hiyo ya Samatta ilifuatiwa na nyingine nyingi za Stars huku Algeria wakionekana kudhamiria kupoteza muda kwa kujiangusha makusudi ili kupunguza kasi ya Stars.

Kwenye dakika ya 22 Mbwana Samatta alipokea pasi kutoka kwa Mudathir Yahya na kusogea mbele na mpira kisha kupiga shuti kali lililozuiwa na mwamba wa juu na kutoka nje ya uwanja.

Dakika 7 baadaye mshambuliaji huyo hatari wa TP Mazembe alipokea pasi nyingine nzuri na kumpiga chenga mlinda mlango wa Algeria Rais M’Bolhi kabla ya kupiga shuti zuri la chini lilozuiliwa vizuri na mlinzi Aissa Mandi na kuzaa kona.

Stars wakapata nafasi nyingine ya wazi kwenye dakika ya 35 ya mchezo baada ya Elias Maguli kumpigia mpira mzuri Farid Mussa aliyeukokota kisha kupiga shuti zuri la chini lililopita pembeni ya mwamba na kutoka nje.

Advertisement
Advertisement

Nafasi ya wazi zaidi ikaja kwenye dakika ya 40 ambapo Farid Mussa alitumia kasi yake na kukokota mpira kwa ustadi kisha kuupenyeza kwa Mbwana Samatta ambaye alipiga shuti lililomgonga golikipa na kurudi uwanjani.

Dakika mbili kabla ya kipenga cha mapumziko ndipo Taifa Stars walipofanikiwa kufunga bao lao la kwanza baada ya Elias Maguli kuunganisha krosi ya Haji Mwinyi kwa kichwa safi kilichodunda uwanjani kabla ya kuingia langoni.

Stars wakaenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja. Algeria walionekana kuamka kidogo baada ya kurudi kwenye kipindi cha pili lakini walinzi wa Stars walisimama imara na kuwazuia vyema kabisa.

Mbwana Samatta akaipatia Stars bao la pili kwenye dakika ya 54 baada ya kuwatoka walinzi wa Algeria na kupiga shuti lililomshinda mlinda mlango na kuingia wavuni moja kwa moja.

Baada ya bao hilo Stars walionekana kupunguza kasi ya mashambulizi na Mwalimu Mkwasa akaamua kufanya mabadiliko kwenye dakika ya 63 kwa kuwaingiza Mrisho Ngassa na Said Ndemla waliochukua nafasi za Elias Maguli na Mudathir Yahya.

Kwenye dakika ya 72 Islam Slimani anayekipiga katika klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno akawapatia Algeria bao la kwanza baada ya walinzi wa Stars kuzembea wakijaribu kuweka mtego wa ‘offside’.

Slimani akazima kabisa shangwe za watanzania dakika tatu baadaye baada ya kupokea mpira uliopenyezwa na Ryad Mahrez na akapiga shuti lililomshinda Ali Mustafa na kutinga wavuni na kuyafanya matokeo kuwa 2-2.

Safari ya Stars inaonekana kuingia ugumu baada ya kulazimishwa sare hiyo na Algeria hivyo vijana wa mwalimu Mkwasa watatakiwa kupigana ili kupata ushindi kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumanne.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

FIFA waanza kukata…

Tanzania Sports

TUSIISHIE TU KUJIVUNIA MAFANIKIO YA SAMATTA NA ULIMWENGU