in , , ,

SIMBA ILISTAHILI KUTOLEWA NJE YA MASHINDANO

*Wachezaji walionyesha dalili za kuwa wachovu mapema

VITU viwili vinapokuwa mbali ( at extremes) kwenye kupingana, matokeo ya uhusiano wa vitu hivyo huwa makubwa kwa uzuri au kwa ubaya kutegemea aina ya mahusiano yao. Kwa mfano, mtu  akiwa ana chuki iliyofikia mbali upande fulani (at one extreme) akikosewa jambo na mwingine anayemchukia yeye kwa umbali mkubwa kwa upande mwingine (at another extreme), ugomvi utakaotokea hapo utakuwa ni wa hatari. Lakini kosa kama hilo wakitendeana watu wasiochukiana, yaani kutokubaliana kwao kwa mambo fulani fulani  hakuuendi umbali mrefu pande tofauti, inawezekana hata ugomvi usitokee kabisa na suala husika litamalizika kwa suluhu nyepesi tu.
Simba SC logo
Simba SC logo (Photo credit: Wikipedia)
Simba wametupwa nje ya mashindano ya ligi ya mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 5-0 na mabingwa wa Angola, Recreativo do Libolo, kutokana na mambo yaliyozihusu timu hizo kuwa mbali kwa kila upande. Libolo walikuwa mwisho kwenye upande wa mazuri huku Simba wakiwa mwisho upande wa mabaya. Angalau Libolo wangekuwa umbali mfupi kuelekea mazuri na Simba umbali mfupi kuelekea mabaya, inawezekana Simba isingefungwa mechi zote; 0-1 nyumbani na 4-0 ugenini na huenda hata mshindi angeamuliwa kwa bao la ugenini kama si baada ya dakika 210 kuchezwa au kwa penalti tano tano baada ya sare ya dakika 210.
Hii inatokana na ukweli kwamba si mara ya kwanza timu zetu kucheza na wawakilishiwa Angola wa mashindano ya soka ya bara hili. Mwaka 1993, Simba waliwafunga Atletico Sportive de Aviacao (ASA) ya Angola kwenye nusu fainali ya mashindano ya kombe la CAF wakati ule (sasa kombe la Shirikisho, baada ya kuunganishwa kwa mashindano ya kombe la CAF na kombe la Washindi kuwa kombe moja).Simba ilishinda 3-1 hapa kwa mabao ya Malota Soma na Edward Chumila. Wiki mbili baadaye Simba wa Tanzania walilazimisha suluhu ugenini na kuingia fainali.
Mwaka 2007, Yanga ilicheza na Petroleum de Angola na kushinda 3-0 hapa kwa mabao ya Waangola kujifunga kutokana na krosi ya Shadrack Nsajigwa, jingine akifunga Mrisho Ngassa na jingine Abdi Kassim. Ugenini kipigo cha 2-0 walichopata hakikutosha kuwatupa nje ya mashindano Yanga wa Tanzania.
Kama kabla ya Libolo, timu za Tanzania zilishazitoa mashindanono timu za Angola, basi Libolo ingeitoa timu yetu sasa si kwa kipigo kikubwa hivi lakini kwa bahati mbaya, kama ilivyoelezwa hapo juu, Libolo na Simba walikuwa kwenye ncha tofauti za mstari, ncha ya uzuri kwa Libolo na ya ubaya kwa Simba.
Wakati Libolo ikiwa na wachezaji maarufu, wazoefu na wenye nguvu toka nchi kadhaa kama Angola, Ureno, Brazil na kadhalika, Simba ilikuwa na wachezaji wengi dhaifu wanaochoka kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika na ilikuwa na wachezaji kadhaa wasio na uzoefu wa mechi kubwa kubwa za mashindano kama watoto Haruna Chanongo na Abdallah Seseme na wakubwa wengine ambao hawajawahi kupambana na mikiki mikiki kama hiyo.
Wakati Libolo ikifanya maandalizi ya nguvu ya muda mrefu nchini Ureno yenye malengo mahsusi ya ushiriki wa mechi za kimataifa, Simba ilifanya maandalizi ya wiki chache ya kisanii nchini Oman, yasiyo na malengo thabiti ya kukabili mashindano makubwa ya kimataifa.
Hapa hata TFF imechangia kuiangusha Simba kwa ushabiki wa hali ya juu wa Yanga wa baadhi ya Watendaji wakuu wa Shirikisho hilo. Haiingii akilini kwa Yanga ambayo haikuwa na majukumu ya kimataifa kupewa siku zaidi ya sita za kupumzika baada ya mechi moja mpaka nyingine huku Simba iliyokuwa na majukumu ya kimataifa kuchezeshwa mfululizo; na Tanzania Prisons Mbeya kisha muda mfupi baadaye na Mtibwa Dar halafu kusafiri kwenda Angola kwa Libolo!
Jambo jingine ambalo liliziweka Libolo na Simba kwenye ncha tofauti ni kwa upande mmoja, utulivu waliokuwa nao Libolo wanaomilikiwa kibinafsi na tajiri wao na kwa upande mwingine vurugu kubwa zilizokuwepo Simba wanaomilikiwa na wanachama, wengi wakiwa masikini kama nini, vurugu zilizotokana na matokeo mabaya ya Simba ya mechi za ligi kuu za kuelekea mapambano hayo ya kimataifa. Kwa hiyo, katika kipindi cha mapambano yao mawili, kwa Libolo utulivu ulikuwa 100% na kwa Simba ulikuwa 0%-ncha moja kwa ncha nyingine!
Aidha, Libolo katika kipindi hicho ilikuwa haina matatizo ya kifedha ikipangilia vizuri matumizi yake huku Simba ikiwa na matatizo ya kifedha kwa, pamoja na mambo mengine, kukosa mipango madhubuti ya matumizi ya fedha kutokana na vyanzo vyake vya mapato kuwa vya kuibukaibuka tu.
Kwa siku zijazo, timu zetu zikipata nafasi za uwakilishi wa nchi wa mashindano ya kimataifa zinapaswa zifanye maandalizi ya kutosha ya kushiriki mashindano hayo kwa kufanya yafuatayo miongoni mwa mengine:-
  • Kuhakikisha ina wachezaji wa kutosha wenye uwezo na uzoefu wa mechi za kimataifa. Ikiuza jembe kama Emmanuel Okwi, ihakikishe inanunua jembe la nguvu zaidi la kiwango cha Sunday Mba wa Nigeria.
  • Ipange ratiba ya maandalizi kwamba lini mpaka lini inafanya nini wapi na kwa malengo yapi.
  • Itengeneze bajeti ya uhakika ya maandalizi hayo na ushiriki huo huku vyanzo vya fedha vikibainishwa ambapo fedha nyingine itakayopatikana vinginevyo iwe kama bonasi ya kufanikisha mipango hiyo.
  • Kuhakikisha kwamba kwenye kipindi chote kuanzia cha maandalizi mpaka ushiriki, hakuna migogoro ya kijingajinga.
  • Kulibana Shirikisho la soka nchini kutoiumiza timu wakilishi kwa malengo ya kuivunja nguvu ili ipitwe na timu inayoshabikiwa kwenye ligi ya hapa au kuivuruga ili isifanye vizuri mashindano ya kimataifa isije ikaitambia ile timu inayoshabikiwa.
Naomba nimalize kwa kuthibitisha mambo mawili kuhusu mechi ya marudiano ya Libolo na Simba. Kwanza, Simba wanachoka haraka. Angalia, mpaka dakika ya 77 ambapo zilibaki dakika 13 mpira kuisha, Simba walikuwa wamefungwa 1-0 tu. Lakini ndani ya dakika 12 walifungwa mabao matatu! Huku kama si kuchoka ni nini?
Pili, uzoefu wa mashindano makubwa ni muhimu kwenye ushiriki wa mashindano ya kimataifa kwani wachezaji wa Simba waliong’ara Angola walikuwa wazoefu wa mikikimikiki hiyo kama Mrisho Ngassa na Felix Sunzu.
Kuanzia mwakani tujipange kama ilivyoshauriwa hapa na kwa bahati ligi kuu yetu inamalizika Mei na mashindano ya vilabu barani Afrika huanza Februari inayofuata. Tuna miezi tisa mizima ya kujipanga, tofauti na wenzetu wengi ambao ligi zao huanza mwanzo wa mwaka na kumalizika mwisho wa mwaka kama ilivyokuwa pia hapa kwetu hapo zamani. Hao wengine wana miezi isiyozidi mitatu ya maandalizi.
Naomba tukubali ukweli kwamba kwa hali ilivyokuwa, Simba ilistahili kutolewa mashindanoni na Recreativo do Libolo ya Angola.
Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Zogo kadi nyekundu ya Nani

Arsenal kuwabomoa Swansea