in , , ,

SAID NDEMLA KARIBU TUZIFUNGUE KURASA ZA KITABU CHAKO

Ndemla

Hapana shaka kichwa cha habari ndicho kilikuwa kivutio cha kitabu chako. Kilipambwa na maneno machache ambayo kila mmoja alivutiwa kukinunua.

“Said Ndemla Fundi wa Dimba”. Haya ndiyo yalikuwa maneno yaliyokuwa yamepamba jarada la kitabu chako. Kitabu ambacho kilikuwa na wafuasi wengi. Wengi wetu tulivutiwa kukinunua kitabu chako kutokana na maneno yaliyokuwa juu ya jarada.

Maneno ambayo yalitupa nguvu ya kukifunua kitabu chako kwa ndani. Tulikutana na dibaji bora sana, dibaji ambayo ilikuwa inaelezea umuhimu wa mchezaji mwenye kipaji kikubwa kucheza katika ligi za nje.

Ligi ambazo zina miundombinu bora, ligi ambazo zina ushindani mkubwa mdani ya uwanja, ligi ambazo zinalipa wachezaji vizuri tena bila kuchelewesha mishahara na malupulupu.

Dibaji hii ilijitanabaisha kwa ufundi wa mwandishi wa dibaji hiyo kuwa wewe una ndoto kubwa ya kucheza nje ya nchi kwenye ligi yenye maslahi makubwa kwenye kipaji chako na uchumi wako kwa ujumla.

Nilivutiwa na Dibaji ya kitabu chako kitu ambacho kilinisukuma nifungue ukurasa mwingine, ukurasa ambao ulinikutanisha na sehemu ya kwanza ya kitabu hiki.

Sehemu ambayo ilikuwa ndiyo sehemu pekee iliyokuwepo kwenye kitabu hiki. Sehemu ambayo ilikuwa na ahadi. Ahadi ambayo ilitoka kwenye kinywa cha Said Ndemla , ahadi ya yeye kuandika sehemu ya pili ya kitabu hiki akiwa ughaibuni.

Ahadi ambayo sisi tuliipokea na tuliamini katika miguu yake. Miguu yake ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuhakikisha ahadi hiyo inatimia.

Maombi yetu yalikuwa hayapungui, kila siku goti letu tulilisurubu na kuinamisha vichwa vyetu ili kumuomba mwenyezi Mungu amfungulie njia.

Njia ambazo ingetegemea na jitihada zake pamoja na aina ya wasimamizi wa kipaji chake alionao.

Hata filamu ya yeye kwenda Sweden ilipopotea sisi tulimvumilia , hatukuta kumsakama sana, tulichofanya ni kushangilia pasi zake bora katika michuano ya ligi kuu.

Aliwafanya kina Emmanuel Okwi na John Bocco wasiwe na wasiwasi wa njaa kwa sababu mpishi bora alikuwepo katikati ya dimba. Ubora huo ulizidi kutuaminisha kuwa kesho ya Said Ndemla itakuwa yenye nuru ang’avu.

Hatukutegemea kabisa kuona giza kwenye kesho yake ikizingatia hata yeye alitabainisha kwenye ukurasa wake wa kwanza wa kitabu chake kuwa anachukia umasikini na alikuwa na watu nyuma yake waliokuwa wanamtegemea sana.

Maandishi yake kwenye ukurasa wake wa kwanza wa kitabu chake yalidai kuwa alienda Simba kama daraja la yeye kumsogeza kucheza soka la kulipwa kwenye moja ya ligi bora ulaya.

Sehemu yake ya kwanza ya kitabu chake ilikuwa imejaa hisia kubwa sana, hisia ambazo zilionesha Said Ndemla alikuwa na ndoto kubwa ya kufika sehemu kubwa katika mpira wake.

Siku zote kuota pekee hakutoshi, unahitaji nguvu ya ziada ya kuishi ndoto zako ili uweze kutimiza kitu ambacho ulikuwa unakitamani.

Sehemu ya kwanza ya kitabu cha Said Ndemla alisema Simba ni daraja lakini leo hii anaonekana amejenga makazi ya kudumu na kusahau kabisa anatakiwa kukimbia kwenda mbele na siyo kwa kurudi nyuma.

Hakuna sekunde ambayo inatumika kwa ajili ya jua kusimama ili limsubiri mtu ambaye hajajiandaa kukimbizana na giza lake.

Jua litakuacha, utabaki kwenye giza na jua litakaporudi tena kwenye giza lako utakuwa tayari umeshaukaribisha upofu.

Hutoona umuhimu wa jua tena, mwanga wa jua hutokuwa na faida tena kwa sababu utakuwa kwenye giza ambalo kama ungeshtuka mapema usingelipata.

Ndiyo maana leo hii namkumbusha Said Ndemla kuwa aliposimama siyo sehemu sahihi. Anatakiwa aachane na habari za yeye kutaka kuendelea kukaa Simba kwa sababu hajatimiza ahadi ya kwenye kitabu chake.

Miguu yake ina thamani kubwa ya kupanda ndege, aangalie ni kipi sahihi kwake kutoa machozi akiwa kwenye BMW au kucheka akiwa kwenye Vistz?

Namkumbusha tu kuwa tupo wengi tunaosubiri kitabu chake kikamilike maana alituuzia kitabu chenye dibaji na sehemu ya kwanza pekee.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NAPATA SHIDA KUJUA MGUU WA KUSHOTO NA KULIA WA MWIGULU

Tanzania Sports

Ronaldo tumuelewe tu jamani amesoma alama za nyakati