in , ,

Pistorius atoka jela

 

Mwanariadha bingwa wa mbio za paralimpiki, Oscar Pistorius ameachiwa kutoka jela na sasa atakuwa nyumbani chini ya uangalizi wa karibu.

Mamlaka za sheria za Afrika Kusini zimeeleza kwamba mwanariadha huyo aliyetiwa hatiani kwa kumuua kwa bahati mbaya mpenzi wake, Reeva Steenkamp , hajapunguziwa adhabu, bali kinachofanyika ni kile kilichomo ndani ya sheria.

Ameachiwa karibu mwaka mmoja tangu atupwe jela na sasa atazuiliwa nyumbani mwake, akiwekewa masharti kadhaa, lakini bado familia ya mpenzi wake inaona haki haijatendeka, ikisema muda aliokaa haulingani na kosa la kuua.

Pistorius (28)anatarajiwa kumalizia muda uliobaki wa adhabu yake – miaka mitano – nyumbani kwa mjomba wake jijini Pretoria. Alimpiga risasi Steenkamp (29) kupitia mlango wa maliwato 2013, akisema alidhani alivamiwa na majambazi.

Hata hivyo, upande wa mashitaka haukuridhishwa na uamuzi uliotolewa dhidi ya Pistorius na rufaa yao inatarajiwa kuanza kusikilizwa Novemba mwaka huu. Jamhuri inadai kwamba kwa ushahidi ulivyokuwa, Pistorius alistahili kutiwa hatiani kwa mauaji ya kukusudia.

Je, baada ya kuachiwa na kukaa nyumbani kipi atatakiwa kufanya? Pistorius sasa hatakiwi kushika silaha aina yoyote, kutumia kilevi kama pombe au dawa na maofisa wanaweza kuingia kwake wakati wowote kwa ajili ya kuchukua vipimo.

 

Advertisement
Advertisement

Pistorius bado hayupo huru, kwa sababu haruhusiwi kutoka nyumbani humo wakati wa usiku, anaweza kufanya kazi lakini atafungiwa kifaa cha kielektroniki kuonesha anachofanya na eneo alipo.

Wanasheria wake wanasema kwamba kwenda mazoezini pamoja na kukimbia ni sehemu ya kazi, lakini bado hakuna duru huru zilizothibitisha kwamba ataruhusiwa kufanya hivyo au kuingia tena kwenye michuano ya kimataifa aliyokuwa na shauku nayo.

Pistorius aliondoka kwenye malango ya Gereza la Kgosi Mampuru II Jumatatu Oktoba 19 alikokuwa akishikiliwa. Miguu yake yote miwili ilikatwa na kuwekewa ya bandia, baada ya kuzaliwa akiwa na matatizo.

Pistorius aliondolewa gerezani humo usiku pasipo kutambulika, akapelekwa nyumbani kwa mjomba wake, umbali wa dakika 20 kutoka lilipo gereza, hivyo kwamba askari walifanikiwa kutoonwa na wanahabari ambao walidhani pengine angetolewa Jumanne hii asubuhi au mchana.

Binamu wa Steenkamp, Kim Martin, alisema kwamba wanafikiria kwenda kumtaka hali Pistorius, lakini si sasa, hadi baadaye pale shemeji yao huyo wa zamani atakapokuwa katika hali ya kufaa. Amesema kwamba anadhani bado yuna mawazo mengi juu ya kilichotokea na yanayojiri.

Wazazi wa Steenkamp wamepata kusema kwamba adhabu aliyopewa mkwe wao huyo wa zamani ni ndogo kulinganisha na kosa. Walikuwa wakilia mahakamani pale ushahidi uliokuwa unatolewa jinsi binti yao alivyonyang’anywa uhai.

Kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini, Pistorius alikuwa anatahili kuachiwa na kutumikia kipindi cha adhabu kilichobaki baada ya kutumikia walau moja ya sita ya adhabu aliyokuwa amepewa.
Ndugu wa Pistorius wameeleza kwamba bado hayupo vyema kiafya na kwamba hawadhani kuwa atarejea kwenye riadha katika kipindi cha karibuni. Pistorius alikimbia mita 400 kwenye michuano ya Olimpiki jijini London 2012, akikimbia na watu wenye viungo vilivyokamilika.

Ikiwa upande wa mashitaka utafaulu kwenye rufaa yao baadaye mwezi ujao, Pistorius anaweza kurejeshwa gerezani kwa kupewa adhabu ndefu zaidi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KUTAFUTA BALLON D’OR KWAANZA:

Tanzania Sports

Arsenal wawakung’uta Bayern