in , , ,

Paul Pogba habari ya mji

 

*Anawaniwa na timu tano, City kuwatoa Toure, Nasri, Dzeko

*Sterling kupiga mnada nyumba Liverpool ili ahamie London

 

Dirisha hili la usajili linaonekana kumweka katika chati ya juu sana mwanasoka Mfaransa anayekipiga Juventus, Paul Pogba,22, ambaye anawaniwa na klabu kubwa tano.

 

Kiungo huyo anawaniwa na Manchester City waliosema wapo tayari kuachana na mmoja au wawili wa wachezaji wake watano pamoja na kitita cha fedha ilimradi wampate Pogba.

 

Klabu nyingine zinazopigana vikumbo na Man City kwa mchezaji huyo ni  Real Madrid, Barcelona, Paris Saint-Germain (PSG) na Manchester United. Man United walimsajili Pogba Julai 2009 kutoka Le Harve kabla ya kumwacha aende Juve akiwa mchezaji huru misimu mitatu baadaye.

 

Manchester City wanapanga kuwatoa kwa ofa Yaya Toure, Samir Nasri, Stevan Jovetic, Aleksandar Kolarov au Edin Dzeko katika dili la kumpata Pogba. Dhamira yao ya kumpata Pogba kwa gharama yoyote imewafanya maofisa wa City kusafiri hadi Torino kufanya mazungumzo na Juventus wajue kipi wanataka ili wamwachie Mfaransa huyo.

 

Maofisa hao wamekwenda kujadiliana na wale wa Juventus ikiwa wanataka kiasi gani cha fedha au mchezaji yupo kati ya hao na hata ikibidi wabandikwe wawili na fedha kisha Man City wachukue kifaa chao.

 

Wanaona kwamba Pogba ndiye atakuwa mbadala anayefaa kwa Toure ambaye pia ameonesha nia ya kuondoka kutokana na uhusiano usio mzuri baina yake na klabu. Juve hawana nia ya kumuuza Pogba lakini watasikiliza ofa zilizo kwenye eneo la Euro milioni 100.

 

Inaelezwa pia kwamba ikiwa ni kumtoa,wangependa dili la fedha taslimu badala ya mabadilishano ya watu mithili ya biashara ya zamani ya bidhaa kabla sarafu hazijabuniwa, yaani barter exchange.

 

Wakati hakuna klabu nyingine iliyofika Torino kwa mazungumzo, pengine kwa vile msimu wa usajili ndio kwanza unakaribia, Pogba binafsi amepata kusema kama ni kuhama basi kipaumbele chake ni kucheza Real Madrid au Barcelona, la kama haitawezekana basi nafasi ya tatu anatoa kwa Man City kabla ya PSG. Hapendi Man United, kwani walimwacha wakidai amechoka.

 

Kuna tetesi kwamba baada ya Pogba kusema angependa kucheza Real Madrid, Kocha wa Castilla, ile timu B ya Reald Madrid, Zinedine Zidane, Mfaransa kama Pogba, amewapigia simu watu wa kambi ya mchezaji huyo.

 

Japokuwa Barcelona wamepigwa marufukukusajili kwa mwaka huu na Fifa, wangeweza bado kumsajili na kumwacha kwa mkopo Juve hadi mwaka kesho ndipo wamweke kwenye rejesta yao.

 

Mkurugenzi wa Michezo wa Man City, Txiki Begiristain na Ofisa Mtendaji Mkuu, Ferran Soriano wapo tayari kumpa Pogba mshahara wa kwenye £250,000 kwa wiki ambao anapata Toure, mchezaji anayelipwa zaidi hapo Etihad.

 

City wanaamini kwamba Pogba anaweza kuungana na mshambuliaji wa Wolfsburg, Kevin De Bruyne aliyeuzwa na Chelsea, na mwenye umri wa miaka 23 na kuifanya timu kuwa na nguvu mpya.

 

Patrick De Koster ambaye ni wakala wa De Bruyne amethibitsiha kwamba City wana nia ya kumsajili mchezaji huyo na kwamba angekutana na Mkurugenzi wa Michezo wa Wolfsburg, Klaus Allofs ili kujua iwapo watamuuza au la.

 

Anathibitisha kwamba Manchester City, Bayern Munich na PSG wameshawasiliana naye, lakini si kwa njia rasmi kwa ajili ya kujua uwapo wa mchezaji huyo, lakini hadi sasa hakuna ofa rasmi zilizotolewa.

 

Pamoja na Toure kuwekwa kama daraja la Pogba kuingia City, bado raia huyo wa Ivory Coast anaweza kukataa kuondoka, kwa sababu bado ana mkataba wa kukaa klabuni hapo. Wakala wake, Dimitry Seluk alipata kusema ana uhakika kwa asilimia 90 kwamba Toure ataondoka kiangazi hiki.

Dzeko, Nasri, Jovetic na Kolarov wanachukuliwa na City kama wachezaji wanaoweza pia kuondoka kwa sababu hawahitajiwi sana kwa vile hawakucheza vyema msimu unaomalizika. City pia wanataka kumsajili mshambuliaji wa West Bromwich Albion, Saido Beraniho, 21.

 

STERLING AJIANDAA KUONDOKA LIVERPOOL

Raheem Shaquille Sterling
Raheem Shaquille Sterling

Mwelekeo wa Raheem Sterling, 20, kubaki Liverpool unaonekana kukosa mashiko, kwani mshambuliaji huyo anadaiwa kuamua kuiuza nyumba yake iliyoko Merseyside ambako amekuwa akiishi na familia yake.

 

Baada ya uamuzi huo, sasa amewaagiza mawakala wa nyumba wamtafutie kasri jijini London, ikionesha dalili kwamba anataka kuihama klabu hiyo inayoelekea kukosa nafasi nne za juu za Ligi Kuu na hivyo kukosa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

 

Uamuzi huo wa kuuza nyumba iliyoko Southport na kutafuta nyingine London, kwa mtu aliyesema anataka kucheza soka ya juu na kutwaa makombe kutawavuta hisia Arsenal na Chelsea ili wamsajili. Amepata kuhusishwa na Arsenal naye akasema ni timu nzuri.

 

Sterling alishanya mazungumzo na kocha wake, Brendan Rodgers, lakini amekataa ofa ya mshahara wa pauni 90,000 kwa wiki, akisema hataki fedha bali mahali anapoona panafaa kucheza. Kazi sasa ipo kwa Liverpool kumshawishi akubali kubaki.

 

TETESI NYINGINE ZA USAJILI

Robin van Persie
Robin van Persie

 

 

Bosi wa Man United boss Louis van Gaal is anadaiwa kufikiria kumuuza Robin van Persie, 31, kwa kuwa anaingia kwenye mwaka wa mwisho katika mkataba wake. Inaelezwa kwamba Van Persie amekasirishwa na uamuzi wa kocha huyo kutomchezesha wikiendi iliyopita dhidi ya Crystal Palace.

 

Kusajiliwa kwa mshambuliaji mpya kutoka PSV Eindhoven, Memphis Depay kumezidi kuacha wasiwasi juu ya hatima ya Van Persie na mshambuliaji mwenzake, Radamel Falcao, ambaye hata hivyo ana klabu yake, Monaco, na Old Trafford yupo kwa mkopo tu. Wote wamechemsha msimu huu.

Inter Milan wanatarajiwa kutoa ofa ya pauni milioni 10 katika ada ya uhamisho kwa kiungo wa Man City, Yaya Toure (31). Inter wanafundishwa na bosi wa zamani wa City, Roberto Mancini.

 

Kocha wa West Ham, Sam Allardyce hataki kuendelea kuwa Upton Park, hivyo anatarajiwa kukataa ofa yoyote kutoka kwa klabu hiyo na amesema hana muda wa kufanya mazungumzo na bodi ili abaki baada ya mkataba wake kumalizika kiangazi hiki.

 

Nahodha wa QPR walioshushwa daraja, Joey Barton, 32, amedai kwamba kuanguka kwao kumesababishwa na ‘mayai viza’ wanne kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, wanaoaminika kuwa ni Adel Taarabt, Armand Traore, Mauro Zarate, Mauricio Isla na Eduardo Vargas.

 

Manchester United wanaamini kwamba hatima ya kipa wao namba moja, David De Gea, 24, haitategemea nguvu ya fedha bali wapi anakotaka kuchezea msimu ujao. De Gea amepewa ruhusu ya kwenda kwao Hispania kupumzika. Ni huko anakotakiwa na Real Madrid.

 

Chelsea wanaamini watawazidi nguvu Manchester United na Inter Milan ili kumsajili mchezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ya Brazil (U- 20) Robert Kenedy anayechezea Fluminense. Wapo tayari kutoa pauni milioni tano. Hata hivyo, watatakiwa kumtoa mkopo kwa klabu ya Ulaya ili Kenedy (19) apate sifa ya kupewa kibali cha kazi.

 

Liverpool wanaandaa ofa kwa  Burnley walioshuka daraja ili kumsajili mshambuliaji wao, Danny Ings, 22.

Lazio wa Italia wanafikiria kuanzisha mchakato wa kumpata mshambuliaji wa Liverpool, Fabio Borini, 24.  Liverpool walikuwa wanataka pauni milioni 12 lakini huenda wakapokea pungufu kutokana na mchezaji huyo kutowaridhisha na mchango wake msimu huu.

 

Liverpool wanamfuatilia kwa karibu mlinzi wa Real Sociedad, Inigo Martinez, 23, na wapo tayari kutoa pauni milioni 21.7 zinazotajwa kwenye kifungucha mkataba wake.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Monk challenges Swansea to take sixth

Swansea wawatibulia Arsenal

Barcelona fainali Ulaya