Welbeck, Rooney wawang’arisha England

Wakati Wayne Rooney amefikisha mechi 100 kwa Timu ya Taifa ya England kwa kufunga bao moja, mshambuliaji wa Arsenal, Danny Welbeck ametupia mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Slovenia.

Wakicheza nyumbani Wembley, England walianzia mguu mbaya, wakateswa na vibonde hao kwenye mechi ya kufuzu kwa Euro 2016, wakakubali bao moja dakika ya 57 kwa Jordan Henderson kujifunga lakini Rooney akafunga dakika mbili baadaye kwa penati.

Welbeck ambaye hadi sasa amefunga mabao matano katika mechi nne kwa taifa lake, alicheka na nyavu katika dakika za 66 na 72 mbele ya uwanja uliotapika washabiki zaidi ya 82,000.

Kwa matokeo hayo, baada ya mechi nne England wanaongoza kundi lao kwa pointi 12, wakifuatiwa na Slovenia, Uswisi na Lithuania, kila mmoja akiwa na pointi sita, Estonia wakiwa na nne na San Marino wakiwa na moja tu.

Katika matokeo mengine ya mechi za Jumamosi hii, Luxembourg walilala kwa Ukraine 0-3, Macedonia wakakubali kichapo cha 2-0 mikononi mwa Slovakia wakati Hispania wakichekelea ushindi wa 3-0 dhidi ya Belarus.

Mabao ya Hispania yalifungwa na kiungo wa Real Madrid, Isco aliyetikisa nyavu kiufundi sana wakati mabao mengine yalifungwa na wachezaji wa Barcelona, Sergio Busquets na Pedro anayewaniwa na Arsenal.

San Marino walitoshana nguvu kwa suluhu na Estonia, Uswisi wakawafunga Lithuania 4-0, Austria wakawaliza Urusi 1-0, Moldova wakafungwa 1-0 na Liechtenstein wakati Montenegro na Sweden hapakupatikana mbabe wakatoka 1-1.

Posted under:  

Tags:  ,

Comments