Wachezaji Ivory Coast wapata mamilioni, nyumba

Serikali ya Ivory Coast imeamua kuwazawadia wachezaji wake wa timu ya taifa nyumba na mamilioni ya dola.

Rais Alassane Ouattara alitangaza uamuzi huo kutokana na heshima waliyoiletea nchi wachezaji hao kwa kutwaa ubingwa wa Afrika.

Kila mchezaji miongoni mwa kikosi cha watu 23 anapata dola 52,000 na nyumba yenye thamani hiyo pia baada ya kuwafunga Ghana kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Jumapili iliyopita.

Tembo hao wa Afrika waliwazidi Ghana kwa penati 9-8 katika fainali iliyopigwa nchini Guinea ya Ikweta.

Wajumbe wa shirikisho la soka na benchi la ufundi la timu hiyo nao wamepata zawadi, ambapo kwa ujumla serikali imetoa zaidi ya dola milioni tatu kusherehekea ubingwa huo uliokuja baada ya miaka 22.

Kwa upande wa Ghana, kila mchezaji anapata dola 25,000 kwa kufika fainali, zikitolewa na mdhamini wao, Shirika la Taifa la Petroli linalomilikiwa na serikali.

Hata hivyo, Waziri wa Michezo wa Ghana, Mahama Ayariga amesema kiasi hicho ni kidogo, ikizingatiwa kwamba wachezaji walipata adha kufikia hatua hiyo, ikiwa ni pamoja na kurushiwa chupa kwenye mechi dhidi ya wenyeji kwenye nusu fainali.

“Kwa wale wanaodhani kwamba shirika hili kutoa dola 25,000 kwa kila mchezaji ni kiasi kikubwa, laiti wangekuwa uwanjani pale Malabo siku walipopigwa,” akasema waziri huyo na kuongeza kwamba walistahili zaidi ya kiasi hicho.

Comments