in , , ,

Tunahitaji tuwe na sera ya michezo Tanzania

*Mashindano ya FA  ni muhimu.

*Mashindano ya mashule yaboreshwe

*Wasomi wa taaluma ya michezo washirikishwe katika maamuzi ya michezo

KILIO cha Watanzania wengi kutaka soka ya Tanzania iinuliwe kilizidi pale Cape Verde walipofanikiwa kuingia robo fainali ya AFCON. Wanaolia wanahoji, hivi hawa Cape Verde, moja ya nchi za kiafrika zisizo za soka, wamepandaje ghafla hivi? Kumbuka, hawa ndiyo walioikwamisha Cameroon kuingia kwenye fainali hizi. Usishangae hawa wakibeba ubingwa, wamejipanga si kuanzia sasa bali kuanzia wakati fulani nyuma wakijiwekea malengo wanayoanza kuyatimiza.
Hawa tuliwafunga kwao 1-0 miaka mitatu tu iliyopita! Kwani ni  hawa tu? Togo nayo imetinga robo fainali. Ni wazi ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Nakukumbusha; mwaka 1994, hawa tuliwafunga kwao 1-0, bao la winga mwenye kasi wa wakati huo Akida Makunda. Leo wako wapi? Kuleee juu kabisa kwa kina Nigeria, Ghana, Ivory Coast, Cameroon, Tunisia, Misri na wakubwa wengine wa soka wa bara letu.
Hapo siyo mwisho, Burkina Faso wanaweza kubeba kombe la AFCON mwaka huu kwa soka kubwa lililoenea katika kucheza kitimu, kwa nguvu,kwa bidii na akili. Hawa mwaka 2006 na 2007 tu hapa walifungwa na Taifa Stars yetu ya Marcio Maximo kwenye mechi mbili za nyumbani na ugenini. Nyumbani tuliwapiga 2-1 kwa bao la Nizar Khalfan na la kujifunga na kwao tukawalaza 1-0 kwa bao la “video” la Erasto Nyoni. Leo hii hawa si wenzetu kwa sababu wamekuwa watu wa kupanga mambo yao kimkakati, sisi akili zinaishia kwa Yanga na Simba!
Ni vizuri tuwe na sera ya michezo ili tuwe na dira ya tunakotaka kwenda tukipanga tunaendaje huko na kwa hatua zipi. Ni wazi hii ni siri ya mafanikio ya Togo, Cape Verde, Burkina Faso na kina Comoro, Sychelles, Mauritius na wengine. Hili lilishazungumzwa hapa kwa marefu na mapana ya kutosha.
Kwa tulivyo sasa na mipango yetu hii ya kileo leo kwa ajili ya mafanikio ya leo leo kupata faida ya leo leo, tunaweza angalau kufanya kitu fulani cha maana kwenye soka kama wachezaji wetu wataimarishwa kucheza soka la nguvu lenye ushindani wa hali ya juu huku tukihakikisha wachezaji wengi wanacheza kupata wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa timu ya taifa na kupata wachezaji wengi watakaouzika nje. Kwa sasa kikubwa cha soka kinachofanyika nchini ni ligi kuu na vijiligi vya chini visivyo na msisimko vya timu kupandia kuelekea ligi ligi za juu mpaka ligi  kuu basi. Hatuna mashindano mengine makubwa ya soka ya vilabu.
Kwa mantiki hiyo, kila kocha anatumia kikosi anachokiamini ambacho kwa mfumo anaoutaka yeye kina wachezaji maalum ambapo kwa mfumo wa mwingine, wale anaowaweka benchi ndiyo mali zaidi! Na hao wanaokaa benchi wanaweza wakafanya mambo ya kumfurahisha hata kocha wa timu hiyo lakini zaidi ya kwenye mazoezi hawana nafasi ya kuonyesha vitu vyao kwenye soka la ushindani kwani hawapangwi na mashindano pekee tuliyo nayo ni ligi za madaraja tofauti tu.
Hapa kocha hapaswi kulaumiwa kwani yeye yupo kwa kubeba ubingwa na si kuwafurahisha wachezaji. Matokeo yake kipa namba moja wa sasa wa Yanga, Ali Mustafa “Barthez” alikuwa hachezi kabisa alipokuwa Simba akiwa msaidizi wa kipa wa Simba Juma Kaseja lakini leo anapocheza akiwa Yanga anaonekana mali labda hata kumzidi Kaseja wa sasa wa Simba! Amri Kiemba wa Simba, ambaye kwa sasa nadiriki kusema ndiye kiungo bora wa Tanzania, alishatoswa vibaya sana na Yanga akikosa namba. Aliokotwa okotwa tu na wengine lakini alipopata nafasi ya kucheza cheza leo hii ni lulu. Mifano ni mingi lakini ikitolewa yote hapa, hatutapata nafasi ya kuzungumza mengine.
Suluhisho la kuwezesha wachezaji wa Tanzania wengi kucheza soka la ushindani ni kuwa na mashindano makubwa matatu yanayopaswa kufanyika kwa wakati mmoja ambayo ni ligi kuu ya wakubwa na ligi kuu ya vijana wa timu za ligi kuu wa chini ya umri wa  miaka 21 ambao hawajaingizwa timu za wakubwa. Ligi ya vijana hawa itakwenda pamoja na ligi za kaka zao na bingwa kupatikana mwisho wa msimu. Mashindano ya tatu ni ya F.A ya mtindo wa mtoano ambayo timu zitalazimishwa na mazingira kutumia wachezaji isiyowatumia mara kwa mara ingawa hazitalazimishwa kikanuni kutotumia vikosi vile vile vya ligi kuu.
Kwa mfano,kama Simba inacheza na African Lyon Jumamosi Dar es Salaam kwenye ligi kuu, Jumanne inatakiwa icheze raundi fulani ya kombe la F.A na Mji ya Mpwapwa mjini Mpwapwa, Dodoma kabla ya Alhamisi kucheza na Polisi Morogoro kwenye ligi kuu mjini Morogoro. Hapo lazima itawawajibisha wachezaji wake wasio katika kikosi cha kwanza kwenye mechi za F.A na hapo ndipo kina Ali Mustafa na kina Amri Kiemba wangeonekana wakati ule walikuwa na uwezo mkubwa kiasi gani.
Umuhimu wa mashindano ya F.A ni kupata mechi kali za mtoano za ushindani za timu za madaraja yote mpaka chini kabisa. Mechi za mtoano huchezwa kwa juhudi kubwa kuliko za ligi ambapo timu zinazokata tamaa ya ubingwa, kupata nafasi za juu za uwakilishi kwenye mashindano ya kimataifa na zenye uhakika wa kutoshuka daraja huzubaa. Kwenye ligi pia kuna wakati timu huzubaa zikiamini “ligi bado tutaamka tu” lakini kwenye mashindano ya mtoano,kila timu hupigana kufa na kupona kwani zikizubaa tu, nje. Kwa sasa Tanzania haina mashindano hata mamoja ya mtoano.
Ratiba yetu ikipangwa vizuri bila kuwepo na mapumziko yasiyo na tija yoyote ya miezi miwili mizima baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu yetu kumalizika, tutamudu kuwa na mashindano mengi ya kitaifa na kimataifa ndani ya msimu. Hapo ndipo tutaibua vipaji vingi mno vilivyojificha kupitia mashindano hayo mengi na vipaji hivyo vinaweza angalau kutusogeza mahali fulani katika mipango yetu ya kileo leo. La muhimu ni kupigana kwa nguvu zote kupata udhamini wa kutosha wa mashindano hayo mengi kwani ni gharama kubwa kuwa nayo yote. Tunaomba kutoa hoja.
                              
Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kashfa upangaji matokeo soka ya Ulaya

Burkina Faso na Nigeria fainali AFCON2013