TETESI ZA USAJILI LEO

Chelsea wamsaka Quadrado
*Arsenal wawataka Paulista, Tiote

HARAKATI za usajili kwenye dirisha dogo lililobakiza karibu wiki moja zinaendelea, ambapo Chelsea wanaongeza nguvu kutaka kumsajili winga wa Fiorentina, Juan Cuadrado (26).
Vinara hao wa Ligi Kuu ya England (EPL) walikuwa wametoa dau la pauni milioni 20.6 lakini Fiorentina wakazikataa na sasa Chelsea wanafikiria kumuuza winga Mohamed Salah (22) au mshambuliaji Andre Schurrle (24) ili kwanza kupata fedha za manunuzi lakini pia kuhakikisha wamo ndani ya kanuni za uungwana katika matumizi ya fedha.

Schurrle ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani anatarajiwa kurudi nyumbani kwao kuchezea klabu ya Wolfsburg. Hata hivyo, Kocha wa Fiorentina, Vincenzo Montella anasema hakuna jinsi Cuadrado anavyoweza kuhamia Stamford Bridge.

Kadhalika Chelsea wanapanga kutenga pauni milioni 40 kwa ajili ya kumnunua kiungo Mfaransa anayekipiga Juventus wa Italia, Paul Pogba aliyeondoka Manchester United 2012 akiwa mchezaji huru baada ya kocha Sir Alex Ferguson kumwona hana thamani uwanjani.

Arsenal wameanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa Villarreal, Gabriel Paulista anayedhaniwa kuwa na thamani ya pauni milioni 16. Arsenal wanataka kuimarisha beki yao kwani tangu kuondoka kwa nahodha Thomas Vermaelen kwenda Barcelona hawajaziba pengo hilo vilivyo.

Kadhalika kuumia kwa Mathieu Debuchy atakayekuwa nje kwa miezi mitatu kumeongeza umuhimu wa kusajili beki mwingine. Arsenal wamekamilisha usajili wa kiungo Krystian Bielik kutoka Legia Warsaw.
Arsenal pia wameanza mazungumzo na Newcastle juu ya uwezekano wa kumsajili kiungo mkabaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Cheick Tiote ambaye amekuwa akihusishwa na klabu hiyo kwa muda sasa.
Wigan Athletic wamekataa ofa ya pili ya zaidi ya pauni milioni nne kutoka kwa West Bromwich Albion wanaotaka kumnunua winga wao, Callum McManaman.

Valencia kutoka Hispania wanasigishana na Liverpool katika mpango wa kumsajili kiungo wa Manchester City na England, James Milner.
Manchester United wapo katika wakati mgumu, kwa sababu hadi sasa hawajapokea ofa kutoka kwa klabu yoyote kwa ajili ya kumnunua kiungo wa Brazil, Anderson ambaye ni mzigo kwa klabu yao kutokana na kutocheza lakini analipwa mshahara mnono.

United wameanaza mazungumzo na Cerro Porteno kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao mwenye umri wa miaka 16, raia wa Paraguay, Sergio Diaz.
Swansea wanafikiria kumsajili mshambuliaji wa Blackburn, Jordan Rhodes kwa ajili ya kuziba pengo lililoachwa na mfungaji wao mkubwa, Wilfried Bony aliyehamia Manchester City.
QPR wanataka kumsajili mshambuliaji Mwitaliano, Dani Osvaldo wa Southampton aliye kwa mkopo Inter Milan. Alipelekwa huko baada ya kumpiga kichwa mchezaji mwenzake wa Swansea.

Newcastle wanapambana na Arsenal kuipata saini ya beki mwenye umri wa miaka 21 kutoka klabu ya Ipswich, Tyrone Mings.
Rais wa Sampdoria, Massimo Ferrero amesema wana mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Everton, Samuel Eto’o (33), lakini mchakato umekwama kwa sababu hakuna nayejua nani hasa ni bosi wa Everton.
Mshambuliaji wa West Brom kutoka Ugiriki, Georgios Samaras anatarajiwa kujiunga na klabu ya nchini Saudi Arabia ya Al-Hilal kwa mkopo wa miezi sita ambapo baada ya hapo anaweza kusajiliwa moja kwa moja huko.

Posted under:  

Tags:  , ,

Comments