Pazia lafunguliwa Madola

Michuano ya 20 Jumuiya ya Madola inaanza Jumatano hii jijini Glasgow, Scotland ikishirikisha timu za mataifa 71.
Jumla ya wachezaji 4,947 wanashiriki katika michezo 17 tofauti itakayoendelea hadi kilele chake Agosti 3 mwaka huu na uwanja mkuu kwa mashindano haya ni Celtic Park inamozinduliwa wakati itaungwa Hampden Park.

Haya ndiyo mashindano makiubwa zaidi kufanyika nchini Scotland yakishirikisha michezo mingi. Scotland ilipata kuandaa michuano kama hii 1970 na 1986 iliyofanyika jijini Edinburgh.

Hii ilikuwa nchi ya kwanza kufikiria kuwa wenyeji wa michuano hii, na fikra hiyo iliwajia 2004, ambapo majiji ya Scotland yalialikwa na Baraza la Michezo ya Jumuiya ya Madola ili kuweka dau la kuwa wenyeji, ndipo Glasgow wakatangazwa kuwa wenyeji.

Scotland wanaandaa kwa kuungwa mkono na Serikali ya Uingereza na vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni. Abuja, mji mkuu wa Nigeria nao uliwania kuandaa michuano hii pamoja na Halifax wa Canada. Halifax walijitoa na kubakisha wawaniaji wawili, ndipo Glasgow wakaibuka kidedea.
image

Abuja walipewa nafasi kubwa zaidi ya kuibuka mshindi kwenye uenyeji, kwa kigezo kwamba hakuna taifa la Afrika lililopata kuandaa michuano hii lakini Glasgow wakashinda kutokana na uwasilishaji mzuri wa ombi la kuandaa, wakiweka ulinganisho wa michuano iliyotangulia ya 2002 jijini Manchester na ile ya 2006 ya Melbourne, Australia.

Glasgow walipata kura 47 wakati Abuja waliambulia 24, na mwenyeji hupatikana kwa wingi wa kawaida wa kura.
Baadhi ya majina makubwa yanayotikisa Glasgow mwaka huu ni wanariadha Usain Bolt wa Jamaica, Mo Farah wa England, Shelly-Ann Fraser-Pryce wa Jamaica, mwendesha baiskeli Sir Bradley Wiggins wa England na mpiga mbizi Tom Daley wa England.

Comments