Mwanasoka auawa uwanjani

Mwanasoka wa Cameroon amefariki dunia baada ya kurushiwa kitu kilichompiga kichwani wakati wa mechi jijini Algiers, Algeria.

Mchezaji huyo wa  JS Kabylie, Albert Ebosse (24) alikuwa mmoja wa walengwa waliotupiwa vitu, ikiwa ni pamoja na mawe kutoka kwa washabiki wao kutokana na kutoridhishwa na walivyocheza dhidi ya  USM Alger waliowafunga nyumbani.

Ilitangazwa kwamba Ebosse alifariki dunia baada ya kuchunguzwa alipofikishwa katika Hospitali ya Tizi Ouzou, mashariki mwa Jiji la Algiers. Mchezaji huyo alifunga bao moja, ambapo timu yake ilipoteza kwa 1-2.

Washabiki walianza kurusha vitu kutoka majukwaani walikokuwa wamekaa wakati wachezaji hao wakienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mechi. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Algeria imeagiza uchunguzi wa tukio hilo kuanza.

Wakati haijathibitika ni kitu gani hasa kilimgonga mchezaji huyo, madaktari walisema kwamba alipoteza maisha kwa sababu ya jeraha la kichwani. Klabu ya USM Alger imeeleza kusikitishwa na kifo cha mchezaji wa wapinzani wao, ikisema ni kitu cha kushitua na kushangaza.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou ametoa tamko akilaani vurugu hizo, na kutoa pole kwa familia na rafiki wa mchezaji huyo chipukizi aliyekuwa akifurahia kazi yake kwa amani na utulivu kiasi cha kutoka nje ya nchi yake kwa jinsi anavyopenda soka.

Hayatou ameonya kwamba soka ya Afrika haiwezi kuwa mazalia ya vitendo vya kihuni kwa namna yoyote ile, na kwamba wanatarajia hatua kali na za mfano kwa wengine zitachukuliwa dhidi ya wahusika wa fujo hizo.

Posted under:  

Tags:  , ,

Comments