Man United wapigwa tena Old Trafford


*Watolewa na Sunderland Kombe la Ligi

Madhila ya Manchester United yamezidi kujilundika, baada ya usiku wa Jumatano kuambulia kipigo kingine nyumbani Old Trafford.
United walifungwa na Sunderland walio mkiani mwa Ligi Kuu ya England kwa tofauti ya bao moja kwenye mikwaju ya penati katika nusu fainali ya Kombe la Ligi.

Timu hizo zililazimika kucheza dakika 120 baada ya kuwa zimefungana kwa uwiano wa mabao, ambapo katika mechi ya kwanza Sunderland walishinda 2-1 na leo United wakashinda 2-1 na uwiano kuwa 3-3.

Katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza Sunderland nusura wamalize udhia kwa kupata bao la kusawazisha lakini United wakachomoa sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho.

Kati ya penati 10 zilizopigwa ni tatu tu zilitinga nyavuni, mbili za Sunderland na moja ya Man United.

Danny Welbeck na Phil Jones walipaisha penati zao wakati kipa wa Sunderland, Vito Mannone aliokoa ile ya kinda machachari Adnan Januzaj na ya mwisho ya Rafael hivyo kuwapa vijana wa Gus Poyet nafasi ya kwanza ya fainali tangu 1985.

Darren Fletcher ndiye pekee aliyefunga kwa United wakati wachezaji hodari wa Sunderland, Craig Gardner na Steven Fletcher walikosa, lakini wakasaidiwa na Marcos Alonso na Ki Sung-Yueng waliofunga kabla ya kipa David De Gea kuokoa penati ya Adam Johnson.

Kocha Moyes aliondoka haraka uwanjani akiwa mnyonge wakati wachezaji wake hawakuamini, Wellebeck akiwa anabubujikwa machozi.
Kwa matokeo hayo, Moyes ataendelea kutafuta dawa ya timu yake inayochechemea huku Sunderland wakiwasubiri Manchester City kucheza fainali katika Uwanja wa Wembley Machi 2 mwaka huu.

Man City wametinga fainali kwa mara ya kwanza katika miaka 38 baada ya kuwatoa West Ham kwa jumla ya mabao 9-0 kwenye nusu fainali mbili walizocheza.

 

Posted under:  

Tags:  , , , ,

Comments