Man City, Spurs zasonga mbele

 
Manchester City na Tottenham Hotspur zililazimika kufanya kazi ya zaida usiku wa Jumatano kufuzu robo fainali ya Kombe la Ligi.

Wakati Manchester City walibanwa na Newcastle hadi muda wa ziada, Spurs walipelekeshwa hadi hatua ya penati na Hull.

Newcastle walielekea kupoteza stamina katika muda wa ziada, ambapo walikubali mabao ya Edin Dzeko dakika ya 99 na Alvaro Degredo dakika ya 105 baada ya kuwa suluhu katika dakika 90 za kawaida.

Ulikuwa mchezo mkali na wa kuvutia, ambapo Newcastle walionesha kudhamiria kusonga mbele kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, na mojawapo Shola Ameobi alimlazimisha kipa namba mbili wa City, Costel Pantilimon kufanya kazi ya ziada.

Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini alisema timu yake ilistahili ushindi, ikiwa ni siku chache baada ya kukubali kichapo kutoka Chelsea kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).

Katika mechi nyingine, Spurs walitumia mikwaju ya penati kuwafurusha Hull, baada ya kwenda sare ya mabao 2-2 katika dakika 120.

Kwenye penati, Spurs walifunga nane na Hull saba.

Robo fainali itazikutanisha timu za Leicester dhidi ya Manchester City; Stoke na Manchester United wakati ama Sunderland au Southampton ndio watacheza na Chelsea huku Spurs wakipangwa na West Ham.

Mechi hizo zitachezwa katika wiki inayoanza Desemba 16 mwaka huu.
 

Posted under:  

Tags:  , , ,

Comments