Fifa yaunda Kamati Maalumu ya Qatar

 
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeunda kamati maalumu kwa ajili ya kuangalia nini cha kufanya kwenye mkanganyiko wa mahali na tarehe za Kombe la Dunia 2022 lililopangwa kufanyika Qatar.

Hatua hiyo inakuja baada ya wadau kulalamika wakisema mashindano hayo hayawezi kufanyika majira ya joto kwani jotoridi hufikia nyuzijoto zaidi ya 40 za sentigredi.

Kinachofikiriwa sasa ni kubadilisha majira ya mashindano ili yafanyike wakati wa baridi, lakini yatavuruga ratiba za mashindano mengine ya kimataifa na katika nchi mbalimbali.

Tayari msuguano wa kisheria umeanza, ambapo baadhi ya nchi na kampuni zinafikiria kuishitaki Fifa na kudai fidia za mamilioni ya pauni.

Rais wa Fifa, Sepp Blatter amesema kwamba kamati hiyo itakuwa na kazi ya kujadiliana na wataalamu wa afya, watangazaji, wadhamini na ligi zenye ushawishi mkubwa barani Ulaya.

Tayari klabu zenye ushawishi mkubwa Ulaya zimepingana na Fifa kuhusu mpango wake wa mechi hizo Qatar. Arsene Wenger wa Arsenal anasema tarehe zibaki hizo hizo japokuwa zinaweza kuathiri wachezaji wakati David Moyes wa Manchester United anasema kuhamisha Kombe hilo kutalazimisha kubadilishwa ratiba nyingine nyingi.

Uamuzi wa kuunda kamati hiyo ulitangazwa mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa Fifa uliofanyika Zurich, Uswisi na kusema kiongozi wa kamati hiyo ni Rais wa Shirikisho la Soka la Asia, Sheikh Salman bin Ibrahim al-Khalifa.

Qatar walipewa uenyeji wa mashindano hayo Desemba 2010, lakini mataifa mengine yaliyotaka uenyeji ni pamoja na Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani, ambao wote walishindwa kwenye kura.

Posted under:  

Tags:  , , ,

Comments