in , , ,

NI MENDES ANAYEMUWEKA FALCAO CHELSEA

 

Jorge Mendes ni wakala mashuhuri zaidi kwenye soka duniani. Nguvu yake ya ushawishi na umahiri wake kwenye kazi yake umemfanya kuwa na wateja wenye majina makubwa kwenye soka.

 

Cristiano Ronaldo, Angel Di Maria, Diego Costa na Radamel Falcao ni baadhi ya wachezaji mashuhuri ambao ni wateja wa Mendes.

 

Makocha Jose Mourinho na Luiz Filipe Scolari pia ni wateja wake.

Mendes anatengeneza pesa kubwa mno kupitia wateja wake kwenye mikataba ya uhamisho na hata kwenye malipo wanayolipwa na klabu zao.

 

Vyanzo vya kuaminika vinaarifu kuwa wakala huyu mara nyingine hunufaika kwa takribani asilimia 30 kwenye baadhi ya miamala hiyo tofauti.

Super-agent Jorge Mendes
Super-agent Jorge Mendes

 

Vyombo vya habari vinamtambua kama ‘Super agent’ kutokana na uwezo na mafanikio yake.

 

Uhamisho wa Radamel Falcao ambaye ni mteja wa wakala huyu kwenda Chelsea umewashangaza wengi.

 

Wengi wanashindwa kukitambua kinachompa matumaini Mourinho juu ya uwezo wa Falcao.

 

Mshambuliaji ambaye anaonesha kutokuwa na makali ya kutisha aliyowahi kuwa nayo miaka ya nyuma.

Alifunga mabao manne tu akiwa na Manchester United msimu uliopita. Lakini bado Mourinho amemuongeza kwenye kikosi chake.

 

Wengi walitarajia Mourinho kusajili mshambuliaji ambaye amekuwa akionesha uwezo siku za karibuni.

 

Hii inatokana na ukweli kwamba safu ya ushambuliaji ya Chelsea haikufanya vizuri msimu uliopita kwenye ligi ya England.

 

Chelsea ilifunga mambao 73 ambayo ni machache mno kwa timu inayochukua ubingwa.

 

Mbaya zaidi mshambuliaji wao tegemeo Diego Costa amekuwa akiandamwa na majeruhi ya mara kwa mara tangu alipojiunga na timu hiyo.

 

Ndio maana wengi walitarajia Mourinho angeongeza mshambuliaji wa kuaminika na si Falcao.

Binafsi nashindwa kuamini kuwa Mourinho ana imani na uwezo wa Falcao. Nimezoea kuona Mourinho akitengeneza timu yenye wapachika mabao wa kuaminika zaidi ya mmoja.

 

Alipojiunga na Chelsea mwaka 2004 Mourinho aliikuta timu hiyo ikiwa na washambuliaji kama Hernan Crespo, Adrian Mutu na Eidur Gudjohnsen.

 

Lakini bado akatoa kiasi cha kutosha na kuwasajili Didier Drogba kutoka Olympic Marseile na Mateja Kezman kutoka PSV.

 

Alifanya yote hayo kuhakikisha kikosi chake kinakuwa na wapachika mabao wa kutosha wa kuaminika.

 

Hata alipojiunga na Inter Milan na baadae Real Madrid sikuwahi kuona Mourinho akikubali kuwa na kikosi kisicho na washambuliaji wa kutosha wa kuaminika.

 

Hapa ndipo ninapohisi kuwa nguvu ya Jorge Mendes ‘Super agent’ imehusika kwenye uhamisho wa mkopo wa Falcao kwenda Chelsea.

 

Mwaka 2004 kulikuwepo na mawakala zaidi ya watatu waliokuwa wakishindania nafasi ya kumuwakilisha Jose Mourinho.

 

Mourinho akawaambia kuwa yule ambaye angemkutanisha na Roman Abramovich ili azungumze naye ndiye angekuwa wakala wake.

 

Siku chache baadaye Mendes akamkutanisha Mourinho na Abramovich.

 

Tangu wakati huo Mendes ameonekana kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa Jose Mourinho kwa kuwa alimtimizia ndoto zake za kuifundisha Chelsea.

 

Kuna uwezekano mkubwa kuwa Mendes amehusika kumleta Falcao Chelsea ili apate nafasi nyingine ya kung’ara ili azivutie timu kubwa ikiwemo Chelsea yenyewe kumsajili kwa dau ambalo litamridhisha Mendes.

 

Hii ni baada ya mipango yake kukwama pale Manchester United walipokataa kutumia kipengele cha mkataba kilichowaruhusu kumsajili mchezaji huyo moja kwa moja kwa paundi milioni 42.

 

Mendes anajua wazi kuwa haitawezekana tena mchezaji wake kununuliwa kwa dau kubwa kama alilonunuliwa na Monaco ambalo inasemekana lilikuwa paundi milioni 50.

Ila wakala huyo anajaribu kutengeneza mazingira ya kupata dau fulani la kuridhisha.

Anafanya jitihada za kupata fursa ya kufanya uhamisho wa mwisho wa maana wa mteja wake ili atengeneze pesa.

Ndio maana wakala huyo amemleta Falcao Chelsea.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Barcelona wachakazwa 4-0

EPL mdogo mdogo