Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) juzi limetoa orodha ya awali ya wachezaji 37 wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa mwaka huu 2015. Yaya Toure wa Manchester City ni mmoja kati ya wachezaji 37 walio kwenye orodha hiyo.

Kiungo huyo raia wa Ivory Coast amekuwa akinyakua tuzo hiyo kwa kipindi cha miaka minne mfululizo sasa. Hivyo kwa sasa ananyemelea ya tano. Kuna mashaka kuwa safari hii Toure Yaya hataweza kuendeleza makali yake aliyoyaonyesha kwa miaka minne mfululizo kwenye tuzo hizi.

Wengi wanaamini kuwa Toure mwaka huu hakuwa kwenye kiwango chake tulichokizoea hivyo hataweza kutwaa tuzo hiyo. Je kati ya wachezaji wengine 36 wanaoiwania tuzo hiyo ni nani wa kumvua taji hilo? Hii hapa ni orodha ya wachezaji wanne ambao wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumpiku Toure kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na viwango walivyoonyesha mwaka huu.

PIERRE EMERICK AUBAMEYANG
PIERRE EMERICK AUBAMEYANG

PIERRE EMERICK AUBAMEYANG – Huyu ndiye nyota anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kumpiku Toure kwenye tuzo za mwaka huu. Aubameyang raia wa Gabon amekuwa kwenye kiwango cha juu mno mwaka huu. Kwenye msimu uliopita uliomalizika Mei mwaka huu Aubameyang alikuwa kinara wa mabao na pasi za mabao ndani ya klabu ya Borussia Dortmund. Mafanikio hayo yakamfanya kuwemo kwenye kikosi bora cha Bundesliga cha msimu huo wa 2014-15. Kwenye msimu huu ulioanza mwezi Agosti ameifungia Dortmund kwenye kila mchezo kati ya michezo 8 ya Bundesliga akiwa na jumla ya mabao 10.

STEPHANE MBIA
STEPHANE MBIA

STEPHANE MBIA – Pengine Mbia si mmoja kati ya wachezaji wanaopewa nafasi ya kunyakua tuzo hii. Lakini ikumbukwe nyota huyu kutoka Cameroon alikuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Sevilla waliotwaa taji la Ligi ya Europa kwa msimu wa pili mfululizo Mei mwaka huu. Alicheza michezo 13 kati ya michezo 15 waliyocheza Sevilla kwenye michuano hiyo. Kiwango alichoonyesha kilimfanya aingie kwenye kikosi cha msimu cha Ligi ya Europa kwa msimu wa pili mfululizo. Kwa sasa ni mmoja kati ya wachezaji muhimu wa Trabzonspor  ya Uturuki baada ya kujiunga nao miezi mitatu iliyopita akiachana na Sevilla.

 

 

ANDRE AYEW
ANDRE AYEW

Ayew ni mmoja kati ya wachezaji gumzo kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu ambapo anakipiga ndani ya klabu ya Swansea City aliyojiunga nayo Juni mwaka huu akitokea Marseille ya Ufaransa. Nyota huyu kutoka Ghana tayari ameifungia Swansea mabao manne kwenye michezo nane ya Ligi Kuu ya England. Amekuwa aking’ara hata kwenye michezo migumu akizifunga timu kama Chelsea, Manchester United na Tottenham. Kuizoea EPL mapema na kuonyesha kiwango cha kustaajabisha kulimfanya atajwe na Chama cha Soka cha England kuwa mchezaji bora wa EPL wa mwezi Agosti mwaka huu.

Advertisement
Advertisement

 

BASEM MORSI – Mchezaji huyu wa Zamalek ya Misri ni mmoja kati ya nyota gumzo wa Afrika wanaopiga soka lao ndani ya bara hilo. Msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Misri uliomalizika mwezi Agosti mwaka huu alikuwa mfungaji bora namba mbili wa ligi hiyo akifunga jumla ya mabao 18 na kuiwezesha Zamalek kutwaa taji la michuano hiyo. Kwenye timu ya taifa ya Misri pia Morsi ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo. Kwenye michezo ya Kundi G ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 ameshaifungia Misri mabao manne, moja kwenye mchezo dhidi ya Tanzania na matatu (hat-trick) dhidi ya Chad.

Je kuna atakayemvua Yaya Toure ufalme wa tuzo ya uchezaji bora wa Afrika kati ya wachezaji hawa wanne? Kama yupo ni nani? Tuvute subira, Disemba 22 mwaka huu mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa na tutakuwa tumepata majibu kamili.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MFUKO wa Pensheni wa PSPF, umezidi kupenya

Mourinho alimwa faini