in

Milima na Mabonde Soka ya Uingereza

Mengi yametokea kwenye msimu huu wa Ligi Kuu na Ligi ya Taifa ya Soka nchini Uingereza na hakika ni sawa na milima na mabonde.
Matukio ya kila namna yalihusisha klabu na timu zao zinazoingia dimbani, waamuzi, chama cha soka, wamiliki bila kusahau kwa namna ya pekee makocha na wachezaji wao.

Hawa ndio wanaopeperusha bendera ya klabu husika uwanjani; kuwapa raha au sononeko washabiki wao na hatimaye ndio mara nyingi hupongezwa au kutupiwa lawama kwa mwenendo wa timu.

Kama ilivyo kwa baadhi ya mashindano na ligi kwingine duniani, hii ya Uingereza huhitimishwa kwa kupata wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya kimataifa, lakini timu tatu zinazofanya vibaya hushuka daraja na nafasi zao kuchukuliwa na nyingine tatu kutoka daraja la chini.
Katikati ya kupanda na kushuka daraja, mambo mengi hutokea, vikiwamo vibweka aina aina, ambapo vyombo vya habari havibaki nyuma kuvidaka na kuujuza umma.
Kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), timu tatu zinazomaliza zikiwa juu kwenye msimamo wa ligi hupata nafasi moja kwa moja kuingia mashindano ya kimataifa.
Timu inayoshika nafasi ya nne hulazimika kuingia kwenye hatua za mchujo kabla ya inayofanikiwa kuungana na zile tatu kwenye hatua za makundi.
Chelsea kwa hali ilivyokuwa hadi mwanzoni mwa wiki, ingeweza kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa njia mbili.
Ya kwanza ni ya wote – kumaliza kwenye nafasi nne za juu, lakini sasa haiwezi kwani kwa pointi ilizo nazo imegota katika nafasi ya sita hata ikishinda, kushindwa au kutoka sare kwenye mchezo wake wa mwisho Jumapili dhidi ya Blackburn.
Kete ya pili iliyobaki mkononi mwake ni kuishinda Bayern Munich ya Ujerumani katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye mechi itakayofayika mjini Munich, Ujerumani Mei 19 mwaka huu.
Vyovyote itakavyokuwa, kuna timu mbili tu hadi sasa zenye uhakika wa kushiriki michuano hiyo ya kimataifa, na zote ni za Jiji la Manchester – Manchester City na Manchester United, zinazoshika nafasi ya kwanza na ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa mtiririko huo. Hizi zinafungana kwa pointi, kinachosubiriwa ni tofauti ya uwiano wa mabao hiyo Jumapili siku pazia la Ligi Kuu ya Uingereza linapofungwa.
Ushindi au uwiano mzuri wa mabao kwa Manchester City utamaanisha kwamba itatwaa taji la Ligi Kuu ya Barclays na hayo yatajulikana baada ya mechi yake inayofanyika nyumbani dimba la Etihad dhidi ya QPR.
Ikiwa hivyo, City ambayo haijatwaa kombe hilo kwa miaka 44, itawapokonya kombe hilo mahasimu na majirani wao – United. Mabingwa watetezi hao wanamaliza msimu ugenini kwa kukipiga na Sunderland.

Washika bunduki wa London, Arsenal, ambao kwa muda sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi itajihakkishia ushiriki wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ikiwa watashinda mchezo wake wa mwisho ugenini dhidi ya West Brom inayofundishwa na Kocha mpya wa Timu ya Taifa ya Uingereza, Roy Hodgson.
Ama kwa upande wake, washindani wengine wakubwa kwenye ligi hii, Tottenham watajihakikishia nafasi ya nne kama wataishinda mechi yao inayofanyika nyumbani dhidi ya timu ngumu ya Fulham.
Klabu za England zina nafasi tatu kwenye Europa League zinazokwenda kwa washindi wa Kombe la FA ambao ni Chelsea; mabingwa wa Kombe la Carling – Liverpool na timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Ushindi wa Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei 19 utamaanisha nini? Ni kwamba klabu hiyo ya Stamford Bridge itaingia moja kwa moja kwenye hatua za makundi za ligi hiyo msimu ujao.
Hiyo haitakuwa bure, bali kwa gharama ya kuipokonya fursa timu itakayokuwa imeshika nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya England, timu ambayo sasa itapelekwa kushiriki Europa League.
Ama ushindi wa Chelsea kwenye Kombe la FA unamaanisha kwamba ikiwa haitatwaa kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani wataingia kwenye Europa League kama washindi wa washindi wa kombe la FA.
Liverpool ilikuwa timu ya kwanza nchini Uingereza kufuzu ushiriki wa ligi barani Ulaya kwa kushinda Kombe la Carling. Liverpool ilifanikiwa pia kufika fainali ya Kombe la FA, lakini ukiacha hayo, haikuwa na msimu mzuri, huku ikishindwa kuonyesha cheche mbele ya mashabiki wake nyumbani Anfield, kabla ya kuwatuliza Jumanne Mei 8 kwa kuikung’uta Chelsea 4 – 1 katika mchezo wa Ligi Kuu.
Nafasi nyingine zilizotarajiwa kupatikana ‘zimeyeyuka’, kwani Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limetoa nafasi tatu kwa Norway, Finland na Uholanzi kupitia kapu lake la Kuzingatia ‘Fair Play’. Hizo ni nafasi zinazotolewa na shirikisho hilo kwa vyama vya soka vya nchi kutokana na mazingatio hayo, navyo huzitoa kwa klabu zenye hadhi hiyo lakini ambazo hazikufanikiwa kupata nafasi ya ushiriki kwenye mashindano ya Uefa.
Timu tatu zinazoshika mkia kwenye Ligi Kuu zinashishwa daraja kwenda kwenye ligi ijulikanayo kama Champions.
Timu ya kwanza kujisogeza kwenye kushuka daraja ni Wolverhampton Wanderers iliyopoteza rasmi matumaini ya kubaki Ligi Kuu tangu Aprili 22 mwaka huu, baada ya kufungwa mabao 2-0 na Manchester City. Blackburn Rovers iliungana nayo Mei 7 pale ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa timu isiyotabirika ya Wigan.
Timu nyingine iliyo katika hali ngumu ni Bolton, ambayo kwa uwiano wake wa mabao, itashushwa daraja isipokuwa kama itaishinda Stoke kwenye mechi yake ya mwisho huku ikiomba QPR ifungwe na Manchester City.
Ikiwa QPR itatoka sare na City, itabidi Bolton ishinde kwa idadi ya mabao tisa au zaidi ili ivuke idadi iliyo nayo QPR na hivyo kukiepuka kikombe cha kushuka daraja.
Aston Villa haipo mbali sana na eneo la hatari, lakini uwiano wake wa mabao unaiacha salama, kwani idadi yenyewe ni 17 ikilinganishwa na Bolton.

Ligi ya Taifa

Tukiingia kwenye Ligi ya Soka ya Taifa, maarufu kama Championship, mambo si haba, kwani pamekuwa na minyukano si kidogo.
Hii ni ligi inayoshirikisha timu 24, lakini ni tatu tu kati ya hizo zinazopanda kuungaa na vigogo kwenye Ligi Kuu. Timu mbili za kwanza zinaingia moja kwa moja, ile ya kwanza ikiwa ni bingwa, huku timu ya tatu hadi ya sita huingia kwenye mchujo ili kupata timu moja itakayoungana na zile mbili za kwanza.
Reading walikuwa timu ya kwanza kusherehekea kupanda daraja hadi Ligi Kuu, na walifanya hivyo wakiwa na michezo miwili mkononi, na kutwaa ubingwa siku nne baadaye.
Walijihakikishia kurejea Ligi Kuu Aprili 17 baada ya kuifunga Nottingham Forest bao 1-0 na wakiwa wametulia, wakatwaa kombe baada ya wapinzani wao wa karibu, Southampton kufungwa mabao 2-1 na Middlesbrough.
Hata hivyo, Southampton walikuja kutwaa nafasi ya pili, hivyo kujihakikishia kuingia Ligi Kuu moja kwa moja baada ya kuipa kipondo timu ya Coventry kwa mabao 4-0 katika mechi ya mwisho wa msimu.
Wapiganaji wengine waliopata kuwa katika Ligi Kuu, West Ham United wamekuwa wakihaha kufa na kupona kufanya marejeo hadi kufikia fainali ya mtoani baada ya kuichakaza Cardiff jumla ya mabao 5-0 kwenye mechi ya kwanza na ile ya marudiano ya nusu fainali.
Katika nusu fainali nyingine, Blackpool iliyokuwa na goli moja kibindoni kabla ya kuingia kwenye mchezo wake wa Jumatano dhidi ya Birmingham City, ilikata tiketi ya kucheza fainali Jumamosi na West Ham, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Birmingham. Ilikuwa inahitaji sare yoyote ile au ushindi kufika fainali.
Kama ilivyo kwenye Ligi Kuu, timu tatu za chini ya msimamo wa Ligi ya Taifa zinashuka daraja na kwenda kucheza kwenye Ligi Daraja la Kwanza.
Kati ya 24 zilizoshiriki msimu huu, Doncaster Rovers walikuwa wa kwanza kuaga michuano hii yenye ushindani mkubwa baada ya kufungwa mabao 4-3 na wanyonge wenzao Portsmouth Aprili 14.
Kama wasemavyo wa sikio la kufa halisikii dawa, Portsmouth na Coventry City waliungana na Doncaster Rovers kwa safari ya Ligi Daraja la Kwanza Aprili 21. Hali hiyo ilidhihirika baada ya Doncaster Rovers kuamua kufa na mtu kwa kuwafunga Coventry City 2-0 na Derby kuwachapa Portsmouth 2-1.

LIGI DARAJA LA KWANZA

Charlton Athletic walifanikiwa kupanda daraja baada ya kuifunga Carlisle Aprili 14 mwaka huu na kutwaa taji la ligi hiyo wiki moja tu baadaye kwa kuifunga Wycombe mabao 2-1.
Nafasi ya pili kwa timu ya kupanda moja kwa moja ilichukuliwa na Sheffield Wednesday Mei 5 baada ya ushindi wa mabao 2-0 mfungwaji akiwa ni yule yule tena – Wycombe katika uwanja wa Hillsborough.
Ushindi huo wa Sheffield Wednesday uliwasukumiza wapinzani wao, Sheffield United kuingia kwenye mechi za mchujo, ambapo imepangwa kupepetana na timu inayoshika nafasi ya sita, Stevenage . katika nusu fainali nyingine, Huddersfield Town na Milton Keynes Dons zinakwaruzana kutafuta wa kuingia fainali.
Timu nne tayari zimefurushwa kwenye ligi hii na kwenda Ligi Daraja la Pili. Rochdale ilikuwa ya kwanza kuanguka Aprili 21 baada ya kufungwa mabao 2-1 na wenzao waliokuwa wakichechemea, Chesterfield.

Exeter City, Chesterfield na Wycombe Wanderers ziliungana na Rochdale kwenye safari hiyo chungu n azote zilithibitishiwa tiketi ya usafiri wa kwenda huko Aprili 28. Hiyo ilikuwa baada ya Exeter City wanaopenda kujiita Grecians kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Carlisle, huku Chesterfield ikiangukia pua kwa kukubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Yeovil na Wycombe ikiridhia magoli mawili ya dakika za mwisho mwisho kutoka kwa Notts County hivyo kupoteza mchezo kwa mabao 4-3.

LIGI DARAJA LA PILI

Mshikemshike wa ligi hii ulishuhudia Macclesfield wakishushwa daraja Aprili 28 mwaka huu wakati
Swindon Town wakipokea tuzo na kupanda Ligi Daraja la Kwanza Aprili 21 licha ya kufungwa mabao 3-1 na Gillingham. Swindon walikuja kujihakikishia kombe baada ya kuwafyatua Port Vale mabao 5-0 wiki moja baadaye.
Waliokuwa wakishikilia nafasi ya pili, Shrewsbury Town walipanda daraja baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Dagenham & Redbridge Aprili 28. Nafasi ya tatu ilikwenda kwa timu ya Crawley Town na hivyo kujihakikishia kupanda daraja moja kwa moja kwa kuifunga
Accrington bao 1-0 Mei 5.
Katika mechi za mchujo kupata timu moja ya kuungana na hizo tatu kupanda daraja, Southend United inachuana na Crewe Alexandra, huku Torquay United ikitoana jasho na Cheltenham Town.
Timu mbili zilizokuwa zikiburuza mkia tayari zimetumwa kwenye ligi ya chini yake, ambayo sasa inajulikana kwa jina la Blue Square Bet Premier. Moja ya timu zilizoshushwa daraja ni Macclesfield Town, ambayo Aprili 28 mwaka huu ilikuwa siku yake ya mwisho ya miaka 15 ya ushiriki wa Ligi ya Soka. Habari hiyo mbaya ililetwa na kufungwa na Burton mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika nyumbani. Mei 5 ilihitimisha ushiriki wa Hereford United kwenye ligi hii, licha ya ushindi wake wa mabao 3-2 dhidi ya Torquay. Walishachelewa, kwani walitakiwa washinde mechi nyingi zaidi.

BLUE SQUARE BET PREMIER
Mashindano haya yamepewa jina la Blue Square Bet Premier kwa sababu za udhamini tu, lakini jina lake hasa ni Conference National.
Kama zilivyo ligi zilizotanguliwa kusimuliwa, inashirikisha timu za England na Wales.
Timu ya Fleetwood Town ndiyo iliyoibuka kidedea msimu huu na kupandishwa moja kwa moja kwenye Ligi ya Soka. Ilikata tiketi hiyo Aprili 14 baada ya kujihakikishia ubingwa pale wapinzani wao wa karibu, Wrexham walipotoka sare ya mabao 2-2 na Grimsby.
Kwa msingi huo, Fleetwood Town itacheza Ligi Daraja la Pili msimu ujao. Huko haitakwenda yenyewe, kwa sababu kuna timu zilizopata kucheza huko zinachuana kwenye fainali ya mtoano, nazo ni
York City na Luton Town. Hapo atapatikana mshindi wa kusindikizana na Fleetwood.
Timu nne za chini ya msimamo zimeshashushwa na nafasi zake zitachukuliwa na mabingwa na washindi wa mechi za mchujo kwenye fainali za Blue Square Bet madaraja ya Kaskazini na Kusini.
Bath City walikuwa wa kwanza katika madaraja matano ya juu kuanguka. Hiyo ilikuwa baada ya
Newport County waliyokuwa wakiifukuzia kwa karibu, kuifunga York mabao 2-1 Aprili 3.
Wanyonge hao walifuatwa na Kettering Town Aprili 7, baada ya kukandikwa mabao 3-0 na Mansfield. Wiki moja baadaye Darlington nao walianguka baada ya sare yao ya mabao 2-2 dhidi ya Bath.
Hayes & Yeading walijikatia tiketi ya kung’oka mashindanoni bila kupenda Aprili 21, licha ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Lincoln.
Vinara wa Blue Square Bet kwa kanda ya Kusini, Woking waling’aa Aprili 14 baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Maidenhead. Dartford inakabiliana na Welling United kwenye mchujo wa fainali Mei 13.
Hyde ilikuwa imepandishwa kwa kofia ya ubingwa wake wa Blue Square Bet kwa kanda ya Kaskazini Aprili 21 baada ya kuitungua Boston mabao 4-1. Gainsborough inaivaa Nuneaton kwenye fainali Mei 13.

LIGI KUU YA SCOTLAND
Ligi Kuu ya Scotland (SPL) iligawanyika nusu baada ya timu zote kucheza mechi 33, ambapo timu sita za juu na sita za chini zikichezeana kwenye ‘nusu zao’.
Ni hivi, baada ya mechi hizo, timu ziligawanyika kwa ubora na udhaifu au kwa vigogo na vibonde, hivyo kwamba zile sita za chini hazingeweza kwa jinsi yoyote kutwaa pointi na kupanda hadi nafasi sita za juu, kama ambavyo zile sita za juu zilishajiimarisha hivyo kutokuwa na wasiwasi wa kupoteza nafasi zao.
Mabingwa wa Scotland ni Celtic wenye pointi 90, wakiwazidi wanaoshikilia nafasi ya pili kwa pointi 20!
Rangers ndio wa pili, wakiwa na pointi 70 kibindoni. Licha ya timu 18 kushiriki Ligi Kuu ya Scotland tangu ianzishwe (timu shiriki kwa msimu ni 12), ni Celtic na Rangers tu zilizopata kutwaa taji hilo.
Lakini wakati Rangers ikisakata vyema kandanda dimbani, hali ya klabu hiyo kiuchumi si njema, kwani inatatizwa na masuala ya fedha, jambo lililosababisha kuanzishwa taratibu za kuiweka chini ya kabidhi wasii, taratibu za ufilisi zikitarajiwa kuchukuliwa, taratibu ambazo hazijajulikana zitaisha lini na kwa vipi.
Ni katika mwanga huo, Rangers imekwanza na inavyoonekana haitaweza kushiriki, hata kama ina tiketi, michuano ya Uefa kwa msimu ujao.
Ilikuwa inategema ingeondoka vipi kwenye mtanziko huo wa ufilisi, ikiwa chini ya taratibu za kisheria na iwapo ingefanikiwa kumaliza matatizo yake, kulipa madeni na kurejea kwenye uendeshaji wa klabu kama kawaida inavyotakiwa kwa klabu za soka za Scotland.
Palikuwapo matumaini makubwa kwamba klabu ingeweza kuondokana na matatizo hayo kabla ya Machi 31 mwaka huu.
Hata hivyo, akaunti za klabu hiyo haziwezi kukaguliwa na kufungwa na wakaguzi wa hesabu katika hali ya kukidhi vigezo vya wasimamizi wa soka.
Hii ni kwa sababu wanataka kuridhishwa ni kwa vipi klabu hiyo itakidhi matakwa yao kwa kuthibitisha kwamba patakuwapo ugharamiaji wa shughuli za kila siku za klabu hadi mwishoni mwa msimu ujao wa ligi.
Kutokana na ukweli kwamba hadi Machi 31 mwaka huu kabidhi wasii hakuwa akijua nani angeichukua na kuimiliki klabu, kwa hiyo hili halingeweza kupata uthibitisho ipasavyo.
Kana kwamba hiyo haitoshi, lipo jambo la tatu, nalo ni kwamba, kwa mujibu wa kanuni za Uefa, Rangers ilitakiwa iwe imeshaweka amana au kulipa madeni yote ya kodi yaliyokuwapo Desemba 31, 2011. Madeni haya kwa Rangers yanakadiriwa kuwa zaidi ya Pauni milioni tano (£5m). Kabidhi wasii hangeweza kutimiza na kuthibitisha hili.
Jambo la nne ni kwamba, klabu ilitakiwa iwe imewalipa au kuelewana na wakopeshaji wake wote kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa ambayo ilikuwa Machi 31 mwaka huu, jambo ambalo halikufanyika.
Lakini, msimamizi wa klabu hiyo kwa sasa, Paul Clark, alisema wazi Machi 7 kwamba matakwa ya sheria na kanuni hayakuwa yanaelekea kufikiwa.
Rangers wanapojaribu kupata suluhu ya matatizo yao, Celtic wenyewe wanachekelea, wakiendelea na sherehe za ubingwa wao waliowapokonya watani wao – Rangers.
Hili ni taji la kwanza kwa Celtic katika kipindi cha miaka minne. Ilitakata kwa kuitandka Kilmarnock mabao 6-0 Aprili 7.
Wakati Rangers wakiwa na uhakika wa kumaliza wakiwa nafasi ya pili kwa vile wana pointi 70 na wanaowafuatia, Motherwell, wana pointi 62, basi nafasi yake katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya inakwenda kwa hao wanaoshika nafasi ya tatu, watakaoingia na Celtic katika raundi ya tatu ya kufuzu.
Kawaida ni kwamba timu zinazomaliza zikiwa nafasi ya tatu na ya nne hufuzu kwa Europa League pamoja na waliotwaa kombe – lakini ngekewa iliyoikuta Motherwell inamaanisha kwamba timu zitakazoshika nafasi ya nne na ya tano zitafuzu.
Hearts au Hibernian kutegemeana na atakayemshinda mwenzake, wataingia hatua za mtoano kwa ajili ya Europa League huku Dundee United wanaoshika nafasi ya nne wakiingia raundi ya tatu ya kufuzu na timu itakayoshika nafasi ya tano itaingia raundi ya pili ya mchakato wa kufuzu.
Dundee United ilijihakikishia nafasi kwenye Europa League baada ya kuifunga Celtic bao 1-0 Mei 6 wakati Hearts inatarajiwa kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tano, isipokuwa kama itafungwa na Celtic katika mechi ya mwisho ya msimu huu na wakati huo huo St Johnstone iifunge Rangers.
Hata hivyo, wakimaliza ligi wakiwa nafasi ya sita, Saints watafuzu kwa Europa League ikiwa Hearts itatwaa kombe.
Kwa mujibu wa kanuni, timu inayokuwa ya mwisho kwenye msimamo wa ligi inashushwa kwenda Daraja la Kwanza, hata kama Rangers itafilisiwa. Timu iliyoshika mkia safari hii ni Dunfermline ‘The Pars’ waliohakikishia kuondoka Ligi Kuu Mei 7 baada ya kufungwa na Hibernian inayoshika nafasi ya 11 kwa mabao 4-0.

LIGI DARAJA LA KWANZA SCOTLAND

Ross County ndio mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza nchini Scotland, hivyo wamemefanikiwa kuingia Ligi Kuu ya Scotland (SPL).
Vijana hao wa Highland walijihakikishia nafasi hiyo Aprili 10 baada ya Dundee kushindwa kuwafunga vibonde wa ligi hiyo, Queen of the South ambao Aprili 28 walikata tiketi ya kushuka daraja baada ya kupigishwa kwata ya mabao 3-1 na Raith Rovers.
Ayr Club, timu inayoshika nafasi ya tisa kati ya timu 10 za ligi hiyo itaingia kwenye michezo ya mtoano na timu tatu za Ligi Daraja la Pili, kujua kama itabaki Ligi Daraja la Kwanza au itaondoka.

LIGI DARAJA LA PILI SCOTLAND
Katika Ligi Daraja la Pili nchini Scotland, msimu unaomalizika umeshuhudia Cowdenbeath wakifanya vizuri na kutawazwa wafalme wapya wa soka Aprili 21 kwa kuwafunga Forfar mabao 2-0.
Timu zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nne – Arbroath, Dumbarton na Airdrie United zinaingia kwenye mechi za mtoano na Ayr United ya Ligi Daraja la Kwanza.
Ama kwa upande wa kushuka daraja, rungu limewashukia Stirling Albion, na uhakika wa kushuka waliupata tangu Aprili 28, walipofungwa na Dumbarton mabao 2-1. Jirani zao walioshika nafasi ya tisa nao itabidi wajitetee kwa kuingia mechi za mchujo na timu tatu za Ligi Daraja la Tatu.

LIGI DARAJA LA TATU SCOTLAND

Jitihada za Alloa Atletic zimelipa, kwani timu hiyo imetwaa ubingwa na kupanda kutoka Ligi Daraja la Tatu ilikokuwa ikicheza.
Ilichanja mbuga Aprili 7 mwaka huu baada ya kuichachafya Elgin mabao 8-1. Ili kupata timu ya pili itakayopanda, timu za Queen’s Park, Stranraer na Elgin City zitamenyana kwa njia za mtoano
Pamoja na timu ya Albion Rovers inayocheza Ligi Daraja la Pili.
Hakuna timu inayoshushwa kutoka daraja hili, japokuwa East Stirling ndiyo iliyomaliza msimu ikiwa ya mwisho kwenye msimamo.
[email protected]

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

TAVA Yawanoa Makocha wa Wavu Mikoani

Milima na Mabonde Kwenye Soka ya Uingereza