in

Mfahamu mchezaji mwenye uraia wa nchi nyingi

Marvin Park

Wakati kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane alipoambiwa kuwapa nafasi wachezaji chipukizi walioko klabuni hapo wengi walijiuliza ni nani na nani watafurukuta kupenya katika nafasi hiyo. 

Hata hivyo FIFA inaruhusu mchezaji kuwakilisha nchi mbili tofauti kwa utaratibu maalumu

Ukweli ni kwamba Real Madrid wapo kwenye mkakati wa kujenga timu mpya baada ya kuona kikosi chao chenye mafanikio kikizidi kushuka uwezo. 

Mastaa wa timu hiyo umri wao unawatupa mkono hivyo njia mbadala ni kuhakikisha chipukizi wakipewa nafasi. Rais wa Real Madrid Florentino Perez na Ofisa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Jose Angel Sanchez walimwagiza Zidane kuhakikisha anafanya mabadiliko kwa kuwapa nafasi makinda kama njia mbadala ya klabu hiyo kupunguza gharama za manunuzi ya wachezaji. Pia kukabiliana na mdororo wa uchumi unaosababishwa na janga la ugonjwa wa Corona. 

Miongoni mwa nyota waliotajwa ni Vinicius Junior, Andriy Lunin, Rodrygo Goes, Attube na Fede Valverde ambao walishaanza kucheza mechi kadhaa za timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali ya La Liga, Cope del Rey na Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Kana kwamba haitoshi, Zidane ameibuka na nyota wengine chipukizi wa Castilla kama vile Fran Garcia, Sergio Arribas, Marvin Park na beki wa kati Chust ambao kwa nyakati tofauti wamepewa nafasi za kukaa benchi kwenye mechi za wakubwa ama kupangwa kucheza kwa dakika chache ili kupata uzoefu. 

Lakini jina linalovutia wengi kwa sasa ni Marvin Park ambaye amepewa nafasi mara kadhaa katika mechi za La Liga. Klabu ya Real Madrid yenyewe ilishangazwa na kijana huyo na hata haikuamini kama kweli Marvin Park anaweza kuwa raia wa nchi nne duniani.

Kwa sasa tunaweza kusema Zidane ni kama amesajili mchezaji mpya katika kikosi chake. Kwenye dirisha dogo la usajili wa mwezi Januari, Real Madrid haikusajili mchezaji yeyote na ilielezwa kuwa kocha wao Zinedine Zidane hakuomba maboresho kwenye kikosi chake. 

KWANINI RAIA WA NCHI NNE?

Marvin Park anaweza kuwa raia wa nchi 4. Katika nchi hizo zote anaweza kuziwakilisha katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA iwapo zitamtaka. 

Hata hivyo FIFA inaruhusu mchezaji kuwakilisha nchi mbili tofauti kwa utaratibu maalumu. Kwa mfano mchezaji ambaye kabla ya kufikisha miaka 21 amewakilisha timu za taifa za vijana anaweza kuchagua nchi ya kuchezea katika kikosi cha wakubwa. 

Hapo ndipo wapo wachezaji ambao wamekuwa wakichezea nchi fulani barani Ulaya na kuamua kurudi nchi zenye asili yao. Wan Bissaka, Frederick Kanoute na wengineo.

Iko hivi, Marvin Park baba yake ni raia wa Nigeria na Mama yake ni raia wa Korea kusini. Hadi hapo Marvin Park ana haki ya kuzichezea timu za taifa za za Nigeria na Korea kusini kwa sababu ndiko walikozaliwa wazazi wake. 

Vilevile Marvin alianzia malezi ya kandanda nchini Uingereza na baadaye nchini Hispania. Lakini hati yake ya kusafiria anayotumia ni ya Hispania. Sasa kwanini anatumia hati ya kusafiria ya Hispania? Marvin Park alizaliwa jijini Mallorca nchini Hispania miaka 20 iliyopita. 

Wakati Real Madrid ilipofanya jaribio la kwanza kumsajili Marvin Park walishindwa kuamini kama kinda huyo alipokuwa na miaka 16 ni raia wa Hispania. Sababu kubwa ilitokana na jina lake kamili lililopo katika kitambulisho chake, Marvin Olawale Akinlabi Park. 

Taarifa zinafafanua kuwa nyota huyo wa Real Madrid ilibainika kuwa alikuwa mtoto wa baba mwenye asili na uraia wa Nigeria aitwaye Akeem Olawale na mama yake mwenye asili na uraia wa Korea kusini aitwaye Hye Sook Park.

Maofisa wote wa Real Madrid waliokuwepo hotelini jijini Mallorca walipigwa na butwaa walionana kwa mara ya kwanza na Marvin Park na baba yake Olawale.

Wakati kaka yake Marvin alipoanza kucheza soka, inasemekana Marvin akiwa na miaka mitano aliangusha kilio kutokana na kuchukia siku ya kwanza kuhudhuria mchezo huo. Hata hivyo miaka michache baadaye wazazi wake walimpeleka katika shule ya soka ya Ciutat de Palma, iliyokuwa mtaani kwao.

Haikuchukua muda mrefu kwa wataalamu wa mpira wa miguu kubaini kipaji cha Marvin. Ndipo mwaka 2009 Marvin Park alilazimika kuondoka jijini Mallorca kwenda kujiunga na timu ya Tranmere Rovers ya Uingereza kwa miaka mitatu pamoja na kuendelea na masomo yake akiwa huko.

Baadaye alirejea Mallorca kujiunga tena Ciutat de Palma, kabla ya kwenda kujiunga na La Salle na kuhamia Penya Arrabal, ambako alionwa na msaka vipaji wa zamani wa Real Madrid, Carlos Paniza na kuwapigia simu mabosi wake juu ya nyota huyo.

Wazazi wake na wataalamu wa michezo wanamzungumzia kijana huyo kuwa mwenye aibu, na daima wamemwita kwa jina la Paniza yaani winga wa kimya kimya. 

Baada ya kujiunga Real Madrid alikuwa na tabia ya kumpigia simu mama yake na kulia mara kwa mara akiwa kambini Valdebebas, ambako alikuwa chini ya kocha Alvaro Benito na baadaye Raul Gonzalez.

MTINDO WA KUCHEZA

Marvin anasifika kwa kasi na ufundi wa hali ya juu, lakini anakabiliwa na tatizo na ukosefu wa nguvu za kutosha. Wakala wake na mchezaji wa zamani wa Real Madrid Joyce Moreno amebaini hali inayomkabili mteja wake hivyo amemshauri kuhakikisha anaongeza nguvu kwa kufanya mazoezi ya kujenga misuli na mwili wake.

Tangu alipojiunga Real Madrid ameboresha uwezo wake kiufundi na ubora katika kufanya maamuzi anapokuwa uwanjani, ingawa bado ameshindwa kuondoakana na aibu.

Marvin alicheza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Hispania wakati Real Madrid ilipomenyana na Real Sociedad msimu huu. Kisha akapewa nafasi kucheza kwenye mchezo mwingine dhidi ya Huesca na akapangwa kikosi cha kwanza kwenye mchezo dhidi ya Getafe ambao Real Madrid walishinda kwa mabao 2-0.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Kanu

Nyota wa Afrika wameyeyuka ‘Top Five’ Ulaya

SSC

Mafanikio ya Simba ni kilio cha Taifa Stars..