in , , ,

MAZURI YA 1992 YAMESHASAHULIKA, TUNAISHI MABAYA YA 2012

Huwezi kuizungumzia historia ya Arsenal bila kumtaja Ian Wright.
Mshambuliaji ambaye aliweka nadhiri ya kuitumikia Arsenal kwa nguvu
zote, akiamini kuipa mafanikio Arsenal kwa nguvu na kupambana ni
tiketi yake ya kwenda mbiguni.

Aliamini katika ibada iliyokuwa inafanyika Highbury kipindi kile, na
kizuri zaidi alicheza kipindi ambacho mchungaji wa kanisa la Highbury
alikuwa Mzee wa upako wa ulinzi George Graham.

Yeye aliamini kupitia kujilinda zaidi kama njia sahihi ya kwenda
mbinguni, alijenga ukuta imara chini ya kina Tony Adams, Paul Merson
huyu anayempiga vita Wenger kwenye mitandao ya kijamii alifanya kazi
bora kwenye kiungo cha kujilinda ndiyo maana haoni tatizo kumwekea
kidole kwenye mboni ya jicho la Wenger.

George Graham aliweza kwa kiasi kikubwa kuifanya timu ya Arsenal iwe
ya kupigana, kipindi chake ilikuwa ngumu kupigwa goli tano kama za
jana.

Unakumbuka mwaka 1992 mwezi wa pili kama huu tuliopo sisi, akiwa na
timu ambayo sifa yake ni kujilinda alifanikiwa kumfunga Sheffield
Wednesday goli 7?

Kipindi kile kikosi kilikuwa na wanaume achana na wavulana waliopo
sasa hivi. Paul Merson, Ian Wright, Alan Smith walikuwa wanautumia
uanaume wao kupata matokeo.

Hata Wenger alipokuja alikuta kuna wanaume na yeye akaingia kwenye
mwenendo huo huo wa kutumia wanaume na akaamua kusajili wanaume kama
kina Viera, Henry ili kuungana na wanaume wengine waliokuwepo pale
kina Denis Bergkamp.

Lakini baada ya kizazi cha wanaume kina Henry, Gilberto Silva, Pires,
Viera, Arsene Wenger aliamua kuwaamini wavulana kwenye kikosi chake.

Wavulana ambao wamezidi kundharirisha kila uchwao na kumvua vazi la
heshima alilonalo .

Mwezi kama huu wa pili mwaka 2012 walienda kutalii pale San Siro
wakakutana na waongoza watalii watukutu, ambao hutumia fimbo
kuwaelekeza watalii ambao ni wagumu kuelewa.

Massimiliano Allegri akiwa na vijana wake kina Kevin Boateng, Zlatan
ambaye alikuwa kwenye ubora wake, Robbino waliipiga goli nne Arsenal.

Na hali kama hii imekuwa kawaida kwa Arsenal kupokea vipigo vizito
kutoka kwa timu ambazo ni kubwa na hii ni kwa sababu wameshayasahau ya
mwaka 1992 na wanayaaishi ya mwaka 2012.

Ya Mwaka 1992 yalikuwa yana ubora wake maana timu ilikuwa inapigana
kwa nguvu na kujilinda vyema kwa sababu ilikuwa na wanaume, lakini ya
mwaka 2012 timu ilikuwa haipigani kwa nguvu na kujilinda vyema kwa
sababu ya wavulana waliojaa kwenye timu.

Wavulana hawa hawa ndiyo waliotia aibu usiku wa jana pale Allianz
Arena. Tena hawakuwa na kumbukumbu kama mwaka 2006 kuna wanaume
walipigana mpaka kufika fainali tena wakikumbana na vizingiti vigumu .

Utaanzaje kuilinganisha Arsenal ya 2006 iliyokuwa na wanaume kama
Viera ambaye hata kabla hujamkalibia unampa shikamo.

Sura yake tu ilidhihilisha ni mwanaume akiyekuwa anaaga kwa mke wake
kuwa anaenda kazini, achana na hawa Wavulana kina Coquelin ambao
wanapiga pasi 6 kwenye mechi nzima.

Bergkamp hakuweza kuzibwa ubunifu wake kama ukivyozibwa jana wa Ozil.
Ilikuwa ngumu kwa kina Campbell kufanya makosa ya kivulana kama
aliyokuwa anafanya Paulista juzi.

Naamini hata Wenger akiangalia CD za michezo ya timu ya mwaka 2006
huwa anatamani siku zirudi nyuma.

[email protected]

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE MECHI YA BAYERN MUNICH NA ARSENAL

Tanzania Sports

KWA HERI GEOFREY BONY NDAJE , NGOJA NILIFUTE CHOZI LANGU