in , ,

MASWALI MUHIMU KUHUSU KESI YA WAMBURA NA TFF

HIVI karibuni kumetoka hukumu ya makamu wa Raisi wa Shirikisho la soka nchini (TFF, Michael Richard Wambura, ambaye alikuwa anakabiliwa na makosa matatu.

Kosa la kwanza ni kupokea fedha za shirikisho kwa malipo yasiyo halali. Kosa la pili ni kughushi barua ya kuelekeza malipo ya kampuni ya Jeck system Limited. Kosa la tatu ni kushusha hadhi ya shirikisho kwa alichokifanya kwenye makosa namba moja na mbili.

Kuna vitu ningependa tuviangalie kwa pamoja kuanzia jinsi kesi ilivyoanza mpaka hukumu ilivyotolewa. Michel Richard Wambura anahukumiwa kwa kosa la kwanza ambalo ni kupokea fedha za shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) yasiyo halali.

Ukiangalia katiba ya TFF iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2013 kwenye kanuni za maadili kifungu cha 73(1) kinamhukumu moja kwa moja Michael Richard Wambura.

Hapa kwa kanuni za kimaadili ya TFF zitakuwa zinamhukumu moja kwa moja Michael Richard Wambura. Swali la kujiuliza, Michael Richard Wambura amepatikana na hatia ya kupokea pesa za shirikisho kwa malipo yasiyo halali,ambalo kwa mujibu wa sheria za nchi ni kosa la jinai dhidi ya Jamhuri.

Sheria ya Makosa ya jinai Sura ya 16 ya sheria za Tanzania iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 inataja makosa ambayo ni dhidi ya Jamhuri pamoja na adhabu zake.

Sasa Jamhuri ni nini? Sheria hiyo katika sura yake ya pili inatoa maana ya Jamhuri kuwa “refers not only to all persons within Mainland Tanzania but also to the persons inhabiting or using any particular place, or any number of those persons, and also to such indeterminate persons as may happen to be affected by the conduct in respect to which such expression is used”

Kwa tafsiri ya lugha ya Kiswahili isiyo rasmi Jinai ni kosa au makosa yanayofanywa na mtu/watu/taasisi kupitia watendaji wake, kinyume cha sheria au taratibu zilizoainisha makosa mabalimbali. Kwa mfano makosa yote yaliyoainishwa katika sheria ya kanuni za adhabu Sura ya 16.

Sasa katika kosa la kwanza la Michael Richard Wambura, ni kupokea fedha za shirikisho ya malipo yasiyo halali, hii moja kwa moja ni kosa la jinai.

Kosa ambalo linatambulika na sheria za nchi kama ilivyoainishwa katika sheria ya sura ya 16. Katika hilo tumwachie Mwendesha Mashataka mkuu wa Serikali alitafutie ufumbuzi dhidi ya Michael Wambura kwa sababu mambo ya soka hayapelekwi mahakamni.

Kosa la pili alilopatikana nalo Michael Richard Wambura ni la kughushi barua ya kuelekeza malipo ya kampuni la Jeck System Limited yafanyike kupitia yeye.

Hatua hiyo ni kinyume na kanuni za maadili ya TFF, kifungu cha 73(7) cha kanuni ya maadili ya mwaka 2013. Kosa hili kwa mujibu kwa sheria za nchi ni la jinai.

Kama inavyojulikana kwa sheria ya Jamhuri kosa la jinai linatambulika kama nilivyoelezea huko juu. Hili nalo liko mikononi mwa mwendesha mashtaka Mkuu wa serikali kulifanyia kazi. Hapa Shirikisho la soka TFF wamefungua njia.

Kosa la tatu na la mwisho kwa mujibu wa Kamati ya maadili ya TFF linasema Michael Richard Wambura ni kushusha hadhi ya shirikisho kwa alichokifanya kwenye makosa namba 1 na 2. Hii ni kinyume na kifungu cha 50(1) cha makosa ya jinai.

Katika sheria za nchi kosa hili linachukuliwa kama kosa la ‘Defamation’ ambalo kwa tafsiri ambayo isiyo rasmi linajulikana kama “Kudhalilisha”.

Sheria mpya ya huduma za habari ya mwaka 2016 (The Media services Act, 2016) ambayo imefuta sheria ya Magazeti (The Newspapers Act, No.3 of 1976) imeainisha kosa hili katika sura ya tano.

Kwa mujibu wa Ibara ya 35 katika kifungu kidogo cha 1 cha sheria ya Huduma za habari imefafanua kuwa “Defamation” ni jambo lolote ambalo likichapishwa na kusambazwa linaweza kuharibu hadhi ya mtu, au utu wake au kuibua chuki dhidi yake au kuharibu kazi au fani ya mtu huyo. Ni jambo la kudhalilisha.”

Nanukuu: Section 35(1) “any matter which, if published, is likely to injure the reputation of any person by exposing him to hatred, contempt or ridicule, or likely to damage any person in his profession or trade by an injury to his reputation, is defamatory matter”.

Hivyo basi kudhalilishwa ni hali inayojitokeza kwa mtu yoyote pale ambapo jambo hilo limechapwa na kusambazwa dhidi yake na kusababisha kuharibu hadhi ya mtu huyo, utu wake au kuibua chuki dhidi yake au hata kuharibu kazi au fani ya mtu huyo.

Kwa mujibu wa kifungu tajwa hapo juu mtu yeyote anayelalamika kuwa amedhalilishwa ni lazima ithibitike/athibitishe mbele ya mahakama.

Kimsingi makosa mawili ya mwanzo ya Michael Richard Wambura yamedhalilisha shirikisho la mpira Tanzania ( TFF) pamoja na wapenda mpira.

Kwa upande wa Michel Richard Wambura anatakiwa atujibu maswali yafuatayo; Ni kweli aliomba mkopo wa kifedha kutoka kwa kampuni la Jerkers System Limited bila idhini ya kamati ya utendaji?

Na kama jibu ni ndiyo kampuni ya Jerkers System Limited linajihusisha na utoaji wa mkopo? Sheria za mikopo zinaruhusu taasisi ipi itoe mikopo?

Kwanini malipo yafanyike kipindi ambacho yeye alikuwa madarakani na kipindi ambacho kinachosemekana marafiki zake (Rais Jamal Malinzi) walipokuwa madarakani? Kwanini kipindi cha Raisi Leodegar Chilla Tenga malipo hayakufanyika?

Mathalani ile barua JKC/SONT/TFF/2014 ya tarehe 13/01/2014 inayoonesha Michael Wambura ameidhinishwa na kampuni ya Jeck System Limited, kwanini inakanwa na mke wa marehemu (kwa sasa ndiye msimamizi mkuu wa mirathi) ambaye alikuwa mmiliki wa kampuni hiyo?

Wakati tukisubiri majibu ya Wambura tunatakiwa pia tupate majibu ya TFF kwenye maswali yafuatayo; Mosi, kwa mujibu wa kanuni za maadili namba 48 ya TFF ya mwaka 2013 inaainisha kuwa barua ya wito inatakiwa ipelekwe siku tatu kabla ya siku ya kusikilizwa kwa kesi. Je ni kweli walipeleka barua siku moja kabla ya kesi kusikilizwa, kama ni kweli hawaoni kuwa walifanya makosa hivyo kuvunja kanuni za maadili ya TFF?

Kwa mujibu wa kanuni ya 58 ya maadili ya TFF ya mwaka 2013 inaainisha kuwa mtuhumiwa anapofika mbele ya kamati anatakiwa apewe siku za kukusanya ushahidi na mashahidi wa kesi husika, lakini kwa mujibu wa mwanasheria wa Michael Richard Wambura hii kanuni haikufuatwa, tunatakiwa tujue ni kwanini haikufutwa?

Michael Richard Wambura kahukumiwa bila kujitetea mbele ya kamati, kwanini kamati haikumpa nafasi ya kujitetea? Kuna ufafanuzi wa matumizi ya bilioni 3 ndani ya miezi saba, kuna haja ya TFF kutoka nje na kuonesha matumizi ya pesa hizo kama ni kweli.

Kaimu katibu mkuu wa TFF ni kiongozi wa chama cha makocha Tanzania (TAFCA). Kwa mujibu wa kanuni anaingia moja kwa moja kama mjumbe wa Kamati Kuu ya TFF, ambapo ukiwa mjumbe wa kamati kuu hutakiwi kuwa mwajiriwa wa shirikisho la soka, hivyo kaimu katibu mkuu wa TFF anakosa sifa za kuajiriwa. Vilevile TFF inatakiwa ije mbele yetu na kututhibitishia kuwa Kaimu Katibu mkuu yupo kama mtu anayejitolea kama ilivyo kwa Afisa Habari?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UNITED WANAPATA WANACHOSTAHILI ILA NI LAZIMA MOURINHO ABADILIKE

Tanzania Sports

TIMU ZIPI ZINA NAFASI KUBWA YA KUTINGA NUSU FAINALI YA LIGI YA MABINGWA?