in , , ,

Man United, City doro

 

*Spurs wawafumua Bournemouth 5-1
*Klopp bado hajapata dawa Liverpool

 

Mechi ya watani wa jadi wa Manchester iliyotarajiwa kuwa kali imepoteza mvuto, ambapo Manchester United na Manchester City walikwenda suluhu.

Wakicheza kwenye dimba la Old Trafford katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL) wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kutengeneza nafasi, huku walinzi Marcos Rojo wa United na Nicolas Otamendi wa City wakicheza vyema.

United walilifikia lango la wapinzani wao na kukaribia kufunga mara mbili, ambapo Jesse Lingard aligonga mtambaa wa panya huku kipa wa City, Joe Hart akiokoa mpira wa Chris Smalling uliokaribia kwenda wavuni.

Nahodha wa United, Wayne Rooney aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa, akifikisha umri wa miaka 30, alikuwa na siku mbaya zaidi uwanjani, akikosea zaidi katika kutoa pasi, akipata mpira mara chache sana na kupoteza mpira mara nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote wa United.

Wachambuzi wa masuala ya soka wanaona kwamba sasa ni wakati wa mchezaji huyo kuondoshwa kwenye kucheza kama mshambuliaji wa kati ili acheze nyuma, namba 10, kwani hana tena makali ya awali.

United walitarajiwa wang’are wakiwa na wachezaji wao, Anthony Martial, Memphis Depay na Rooney huku washabiki wa City wakiwaangalia kwa makini wachezaji waliowagharimu pauni zaidi ya milioni 100, Raheem Sterling (£49m) aliyetoka Liverpool na Kevin de Bruyne (£55m) kutoka Wolfsburg.

Hata hivyo, Sterling alicheza dakika 55 tu kisha kocha Manuel Pellegrini akamtoa na kumwingiza Jesus Navas baada ya kuonekana hakuwa katika kiwango kikubwa cha uchezaji. Nusura awasababishie Man City hasara ya penati alipomchezea vibaya Ander Herrera lakini mwamuzi Mark Clattenburg akapuuza maombi ya washabiki wa Old Trafford.

Kwa sare hiyo, City wamerejea kileleni baada ya kuwaachia Arsenal kwa karibu saa 24 hivi. Wamefungana na Arsenal kwa pointi 22 lakini wanawazidi kwa mabao sita.

 

SPURS WAWAFUMUA BOURNEMOUTH
Harry Kane na hat-trick
Harry Kane na hat-trick

 

Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspur waliwafungia kazi Bournemouth kwa kuwafunga mabao 5-1, baada ya kuwa nyuma kwa bao moja bila, bao lililofungwa katika dakika ya kwanza tu ya mchezo na Matt Ritchie.

Harry Kane aliyekuwa na ufanisi mkubwa msimu uliopita na kuanza vibaya msimu huu, alifufuka na kufunga mabao matatu kwenye mechi ya Jumapili hii, ikiwa ni pamoja na bao la kusawzisha kwa penati baada ya kuangushwa na kipa Artur Boruc.

Mabao mengine ya Spurs yalifungwa na Mousa Dembele na Erik Lamela. Kikosi cha Spurs hadi sasa hawajapoteza hata mechi moja na sasa vijana hao wa Mauricio Pochettino wamepanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Bournemouth kukubali kichapo cha mabao matano, kingine kikiwa ni kutoka kwa Manchester City. Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu tu, inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi nane na nakisi ya uwiano wa mabao 10 na wana pointi nane tu.

 

LIVERPOOL BADO KUPATA DAWA YA USHINDI
 Philippe Coutinho wa Liverpool
Philippe Coutinho wa Liverpool

 

Liverpool wamekamatwa na Southampton kwa kwenda sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza ya ligi nyumbani kwa kocha Jurgen Klopp anayetafuta dawa ya kuwarejesha Reds katika mwendo wa ushindi.

Ilibidi Liver wasubiri hadi dakika ya 77 kupata bao kupitia kwa Christian Benteke aliyesajiliwa kiangazi kilichopita kutoka Aston Villa, akifunga kwa kichwa akipokea mpira wa James Milner.

Hata hivyo, dakika nne kabla ya mechi kumalizika, Sadio Mane aliwasawazishia Saints baada ya mpira wa kichwa wa Gaston Ramirez kutemwa na kipa Simon Mignolet. Mane alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika za lala salama, akiwa amepata kadi mbili za njano. Wenyeji walitawala mchezo kwa asilimia 61.

Sare hiyo inawafikisha Liverpool katika nafasi ya tisa wakati Saints wapo nafasi ya nane, wote wakiwa na pointi 14 bali wakitofautiana kwa mabao. Hii ni mechi ya tatu kwa Klopp tangu aingie Liverpool na zote amepata sare.

Klopp anayekabiliwa na majeruhi; Danny Ings na Daniel Sturridge – hivyo aliamua kumwanzisha Divock Origi katika ushambuliaji wa kati. Hata hivyo, nafasi ya Origi ilichukuliwa na Benteke katika dakika ya 45. Origin alimudu kugusa mpira mara 10 tu katika muda wote uwanjani, ikiwa ni chache kuliko mchezaji mwingine yeyote wa timu hizo mbili.

Southampton wameshikilia rekodi yao ya kutopoteza mechi ya ugenini, lakini kocha Ronald Koeman alisema kwamba timu yake haikufanya vyema alivyotaka. Virgil van Dijk wa Southampton alikuwa nyota wa mchezo, akitoa pasi 42 na nusura afunge bao, lakini mpira wake wa kichwa ukaparazwa na kipa Mignolet.

 

SUNDERLAND WAFUFUKIA KWA NEWCASTLE
Fabricio Coloccini alitolewa kwa kadi nyekundu
Fabricio Coloccini alitolewa kwa kadi nyekundu

 

Hatimaye Sunderland wamepata ushindi waliouhitaji chini ya kocha mpya Sam Allerdyice , baada ya kuwafunga watani wao wa jadi, Newcastle 3-0.

Ushindi huo umewaondoa Sunderland kwenye nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi, kwani sasa wamefikisha pointi sita na wanashika anfasi ya 18. Kwa watani hao wa jadi wa Wear-Tyne huu ni ushindi wa sita mfululizo wa Sunderland.

Newcastle walitawala dakika 45 za kwanza, lakini walianza kuelekea pabaya baada ya mlinzi na nahodha wao, Fabricio Coloccini kupewa kadi nyekundu kutokana na kumsukuma Steven Fletcher aliyekuwa akielekea kufunga bao. Wenyeji hao walipewa penati iliyofungwa na Adam Johnson dakika ya 45. Mabao mengine ya Sunderland yalifungwa na Billy Jones na Fletcher.

Washabiki wa Newcastle walikasirishwa na uamuzi wa Robert Madley, wakidai kwamba haikuwa haki kutolewa nje. Kocha wa Sunderland, Allardyce naye alieleza kwamba ni vyema kanuni zikabadilishwa ili ikitolewa penati basi mchezaji aliyecheza faulo asitolewe nje.

Baada ya kukamilika kwa mzunguko wa 10, Man City na Arsenal wanaongoza kwa pointi 22, wakifuatiwa na West Ham na Man United wenye pointi 20 kila mmoja huku Leicester wakiwa na pointi 19 na Spurs wanazo 17.

Aston Villa wanashika nafasi ya mwisho wakiwa na pointi nne na tayari wamemfukuza kocha wao, Tim Sherwood aliyeishika kwa miezi minane tu.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Sherwood afukuzwa Villa

Tanzania Sports

USAJILI UPI UMEKUWA WA MAFANIKIO ZAIDI?