in

Mambo 10 yanayomkabili kocha mpya wa Yanga

Mabingwa wa soka wa zamani nchini klabu ya Yanga inatarajia kuanza kunolewa na Kocha  mpya, Cedric Kaze raia wa Burundi. Yanga wamelazimika kusaka kocha mpya baada ya  kumtimua Zlatko Krmpotic kutokana na sababu za kiufundi. Licha ya ukubwa wa klabu hiyo  kwa sasa imepitia vipindi tofauti vyenye taswira chanya na hasi. Baada ya kuondolewa kocha  mkuu, Yanga iliendelea kuwa chini ya kocha Juma Mwambusi ambaye alishirikiana na Said  Maulid kusimamia kikosi hicho katika mechi za kirafiki. Ujio wa kocha mpya una maana kubwa  mashabiki wa Yanga, na yafuatayo ni mambo kumi yanayomkabilia kocha mpya. 

1. Kusambaratisha ufalme wa klabu ya Simba Ligi Kuu 

Hakuna jambo linalowaumiza kichwa mashabiki wa Yanga na viongozi wao kama namna ya  kupata majibu sahihi kwa swali; ni vipi wanaweza kubomoa ufalme wa Simba katika Ligi kuu  Tanzania Bara. Makocha waliopata kuzinoa yanga tangu msimu wa 2017/2-18 hawajafanikiwa  kubomoa umwamba wa Simba. Simba ni mabingwa wa soka misimu mitatu mfululizo; 2017- 2018, 2018-2019, 2019-2020. Kwa kipindi chote hicho mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiishi  kinyonge mbele ya wale wa Simba. Ni kama vile Simba wamejimilikisha LigiKuu Tanzania Bara  kwani hakuna timu iliyofanikiwa kutikisa kwenye mbio za ubingwa. Kwahiyo kocha anayenoa  Yanga anatakiwa kuleta ubingwa wa Ligi Kuu, nje ya hapo atakuwa kwenye nafasi finyu  kuendelea kukinoa kikosi hicho.  

2. Yanga kumfunga mtani kadiri wanavyojisikia 

Tanzania Sports
Kocha mpya wa Yanga akiwa na mtendaji mkuu wa Yanga

Pambano la mwisho Yanga walifungwa mabao 4-1 na Simba. Ushindi wa Simba ulikuwa ni kama  bile kisasi cha kufungwa 1-0 na Yanga ambapo mfungaji alikuwa Mghana Bernard Morrison.  Kipigo cha mabao 4-1 bado kinawapa wakati mgumu sana Yanga. Ni namna gani wataweza  kupindua meza angalau wao washinde zaidi ya idadi hiyo. Ikumbuke Simba inayo historia ya  kuifunga Yanga mabao 5 wakati ikiwa chini ya mshambuliaji mkali Emmanuel Okwi. Hiki ni  kibarua kingine cha kocha mpya wa Yanga, ni lazima ahakikishe anawachapa Simba mabao ya  kutosha. 

3. Kuhimili presha kubwa ya Yanga  

Katika ulimwengu wa soka wapo wachezaji wanaweza kutamba katika timu ndogo lakini  wakashindwa kung’ara ndani ya jezi za Simba na Yanga. Ipo hivyo hivyo kwa baadhi ya makocha  ambao wamekuwa wakitamba kwenye timu mbalimbali lakini wanapopewa kazi ya kuzinoa  Simba au Yanga wanafeli. Presha ya timu hizo mara nyingi zimesababisha makocha hao  kutupiwa virago na namna ambayo mashabiki wengi wanashindwa kuelewa kinachomtokea  licha ya sifa kuwa alikuwa mahiri mahali kwingine. Kwa vile Yanga na Simba zimeweka viwango  vya ushindani kwahiyo kila mmoja anatakiwa kumshinda mwenzake kudhihirisha utemi wake  kwenye kandanda. Kocha anatakiwa kuhimili presha inayomkabili ili aweze kuipatia ushindi  Yanga. Kocha mpya anatakiwa kuelewa Yanga wana matamanio mengi, hivyo presha hii itakuwa  dhidi yake.

4. Yanga wanataka ubingwa sio kusindikiza 

Kiu kubwa ya mashabiki wa Yanga na viongozi wao ni kuona klabu yao inachukua ubingwa.  Ndiyo, kuna raha yake ya kuchukua ubingwa mbele ya mtani wao Simba. Kabla ya Simba  kuibuka wababe misimu mitatu mfululizo kama ilivyokuwa Yanga ya Yusuf Manji, sasa  wanataka kurejesha utamu wa ubingwa. Kocha mpya anatakiwa kulielewa jambo hili kuwa ujio  wake Yanga ni kutakiwa kuleta ubingwa tu. Mashabiki wanaweza kumsamehe kocha wao mpya  ikiwa ataifunga Simba tu, hata kama atakosa ubingwa. Kumchapa mtani na kutwaa ubingwa  itakuwa bonsai ya aina yake. 

5. Washambuliaji kutupia mabao 

Msimamo wa wafungaji wanaoongoza Ligi Kuu hakuna jina la mshambuliaji wa Yanga. Hadi  sasa kinara wa kupachika mabao ni mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube ambaye amecheka  na nyavu mara tano, akifuatiwa na Meddie Kagere mwenye mabao manne na Chriss Mugalu  mwenye mabao matatu naye akitokea Simba. Kwahiyo ndani ya wafungaji watatu wanaongoza  kwa sasa, wawili wanatoka Simba. Hili nalo linawakera mashabiki wa Yanga. Ni namna gani  kocha mpya atawafanya washambuliaji wa Yanga waweze kupachika mabao ya kutosha ili  ilikuwapa raha mashabiki wao? Je, mshambuliaji moya Saidi Ntibazonkiza atawapa furaha  wanajangwani? 

6. Soka la burudani na shangwe kila kona 

Zlatko alilaumiwa kwa kuwa na mbinu mbovu za mechi na kuifanya Yanga icheze bila  kuwaburudisha mashabiki wao. Mbinu za kocha aliyetimuliwa zilianzia safu ya ulinzi. Zlatko  alihakikisha safu ya ulinzi ilikuwa ngumu kufungika hivyo wao kutaka kupata ushindi. Hata  hivyo safu ya ushambuliaji haikupewa mbinu mbadala za kupachika mabao ya kutosha. Muundo  wa kuitengeneza mabao haukuwa mzuri kwa maana ya washambuliaji kupata mbinu za  kiuffundi. Hali hiyo ilisababisha timu iwe inapata ushindi mwembamba mno. Kocha mpya  anakabiliwa na kibarua cha kuwapa burudani na ushindi mashabiki wa Yanga. 

7. Atafanyaje kumziba mdomo Morrison? 

Mashabiki wa Yanga wana hasira na winga Bernard Morrison ambaye amehamia Simba. Yanga  wanaamini Morrison amehama timu yao kihuni na hakufanya adabu, hali ambayo ni kawaida  kwa wale walioumizwa na jambo. Mashabiki wa Yanga wanataka kumwonesha Morrison kuwa  timu yao ni kabambe na inaweza kufanya maajabu kuliko anavyodhani. Yote hayo yanategemea  kocha mpya wa Yanga ambaye anatazamwa kwa jicho la ‘kumdiba mdomo’ Morrison kwa  namna yoyote ile kila watakapokutana kwenye mechi za Ligi Kuu. Ni namna gani kocha mpya  wa Yanga ataweza kuwafurahisha mashabiki na kuwatuliza hasira zao dhidi ya Morrison? Huo  ni mtihani mwingine.  

8. Kuwaridhisha mastaa kikosi cha kwanza 

Yanga kuna mastaa wengi ambao wanatafuta namba katika kikosi cha kwanza. Wapo Tuisila  Kisinda, Calinhos, Sarpong, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke,Fei Toto, Haruna Niyonzoma na  Tonombe Mukoko kwa kuwataja wachache. Nyota karibu wote Yanga wanataka kupangwa 

kikosi cha kwanza. Wote wanaamini wanao uwezo wa kupata namba kikosi cha kwanza. Je, ni  namna gani kocha mpya wa Yanga atafanikiwa kuwaridhisha nyota wa klabu hiyo? Ni nani  atakuwa kikosi cha kwanza na nani ataridhia kuwekwa benchi? Hilo ni jukumu la kocha mpya  ambaye atatakiwa kuamua nani awe kikosi cha kwanza au pili. 

9. Ni nyota wazawa au wageni watatoboa? 

Iko hivi. Kuna mastaa waazawa wanaamini hawajazidiwa uwezo na wachezaji wa kigeni. Deus  Kaseke aliwahi kunukuliwa na gazeti moja la michezo nchini akisema haoni mchezaji mwenye  uwezo wa kumweka benchi. Kaseke alikuwa anawasilisha ujumbe kuwa kiwango chake na uwezo  wake ni wa juu zaidi hivyo hakuna mchezaji wa kigeni atayesababisha kocha amtupe benchi.  Sasa kocha mpya anatakiwa kuhakikisha anawapa nafasi nyota wote, lakini je ataegemea kwa  mastaa wa kigeni au wazawa? Hilo nalo litaeleza mwelekeo wa kocha mpya.  

10.Nani awe namba moja golini? 

Jukumu lingine la kocha mpya ni kuamua nani awe kipa namba moja wa Yanga. Katika klabu  hiyo wapo makipa watatu; Ramadhani Kabwili na Metacha Mnata ambao ni watanzania na  Mkenya Farouk Shikalo? Ni nani anastahili kupangwa langoni? Je, kocha mpya atakuja na jibu  gani katika nafasi hiyo ambayo imekuwa ikiwagawa mashabiki?

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Roy Keane

Roy Keane atawavusha ‘Class of 92’?

Tanzania Sports

Kikosi Bora Kwa Raundi Tano VPL