in , , ,

LIGI KUU BARA: SIMBA YAUA TANO, YANGA YADONDOKA TENA

 

Wekundu wa Msimbazi Simba SC wameichakaza Mgambo JKT kwa jumla ya mabao matano kwa moja kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jioni ya leo.

Ni Hamis Kiiza aliyefunga mawili huku mengine yakiwekwa wavuni na Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajib na Dani Lyanga. Mgambo walipata bao lao la kufutia machozi kupitia kwa Fully Maganga kwenye dakika za mwisho za mchezo.

Simba waliuanza mchezo huo kwa mashambulizi ya kasi ambayo hayakuchelewa kuwapa matunda pale ambapo kinara mwenza wa mabao Hamis Kiiza alipowapatia bao la kuongoza baada ya kupokea pasi stadi kutoka kwa kiungo chipukizi Ibrahim Ajib.

Kiiza akapata nafasi ya kuiongezea Simba bao la pili kupitia mkwaju wa penati lakini mshambuliaji huyo akapiga shuti dhaifu lililozuiliwa kirahisi na mlinda mlango wa Mgambo JKT katika dakika ya 14 ya mchezo.

Dakika ya 28 ya mchezo ilimshuhudia kiungo mzoefu Mwinyi Kazimoto akiiandikia Simba bao la pili kupitia shuti kali lililotinga wavuni licha ya jitihada za mlinda mlango Mudathir Khamisi kujaribu kuzuia.

Dakika chache baadae Ibrahim Ajib akagongesha mwamba kupitia mpira wa adhabu kabla ya kufanya kazi nyingine nzuri mnamo dakika ya 42 ya mchezo na kuipatia Simba bao la tatu baada ya kuwachambua walinzi wa mgambo na mlinda mlango wao.

Ndani ya kipindi cha pili Wekundu hao waliendeleza makali yao lakini hawakuweza kupata bao la ziada mbaka kufikia dakika ya 62 ambapo mwalimu Jackson Mayanja alifanya mabadiliko kwa kumtoa Hija Ugando na kumuingiza Said Ndemla. Dakika 10 baadae Ajib pia akafanyiwa mabadiliko na kumpisha Dani Lyanga.

Lyanga akaipatia Simba bao la nne mnamo dakika ya 77 zikiwa ni dakika tano baada ya kuingia akichukua nafasi ya Ajib. Hamis Kiiza ndiye aliyefunga karamu hiyo ya mabao mnamo dakika ya 83 akimalizia kazi ya Hassan Kessy. Mshambuliaji huyo raia wa Uganda sasa amefikisha mabao 14 akifungana na kinara mwenzie wa mabao Amisi Tambwe wa Yanga.

Maafande wa Mgambo walipata bao lao la kufutia machozi dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika kupitia kwa Fully Maganga aliyepiga shuti kali na kumtungua Vicent Angban.

Huko jijini Mbeya katika dimba la Sokoine vinara wa Ligi Kuu Bara Dar-es-salaam Young Africans walishikiliwa na wenyeji Prisons kwa kulazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili. Yanga ndio waliotangulia kupata bao katika dakika ya 35 ya mchezo kupitia kwa Amisi Tambwe aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua.

Tanzania Prisons wakarudisha bao hilo dakika tano kabla ya kupulizwa kwa kipenga cha mapumziko kwa bao lililofungwa na Juma Jeremiah aliyeruka juu na kumuacha chini Vicent Bossou akikosa namna ya kumzuia.

Vijana wa Jangwani walishindwa tena vita ya mipira ya hewani katika dakika ya 62 ya mchezo pale Mohamed Mkopi alipoifungia Prisons bao la kuongoza kwa kichwa safi kilichomshinda mlinda mlango Deo Munishi na kutinga wavuni.

Kufuatia bao hilo la kuongoza wenyeji Prisons wakajaribu kulinda zaidi na kutumia mbinu za kupoteza muda huku Yanga wakifanikiwa kutengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo hazikuweza kuwapatia mapema bao la kusawazisha.

Yanga wakapata bao lao la kusawazisha ndani ya dakika ya 85 ya mchezo kupitia mkwaju wa penati uliowekwa wavuni na Simon Msuva kufuatia mlinzi wa Prisons kuizuia kwa mkono pasi ya chini iliyopigwa na kiungo Haruna Niyonzima ndani ya eneo la hatari. Bao hilo la Msuva ndilo lililowanusuru Yanga na kuwapatia alama moja.

Kufuatia matokeo ya michezo hiyo miwili Yanga wanaendelea kubaki kileleni mwa msimamo wakiwa na alama 40 huku wakifukuzwa kwa karibu na watani wao Simba SC waliokusanya alama 39 sawa na Azam FC wanaoshika nafasi ya tatu ambao hata hivyo wana michezo miwili mkononi.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MOURINHO NA UJIO WA PEP GUARDIOLA LIGI YA ENGLAND JULAI

Tanzania Sports

LA LIGA WIKIENDI HII