in , , ,

KUKOSEKANA KWA NEYMAR KWENYE MICHEZO YA KIRAFIKI NI FAIDA KWA BRAZIL

Neymar, licha ya umahiri wake, ni mchezaji mwenye rekodi ya maana ya utovu wa nidhamu uwanjani. Mshambuliaji huyo aliye nje kutokana na majeraha ana kiwango kidogo mno cha uvumilivu timu yake inapozidiwa ama kupoteza mchezo. Akiwa na timu ya taifa ya wakubwa ya Brazil amewahi kupoteza mchezo mmoja tu ndani ya dakika za mchezo.

Hiyo ilikuwa kwenye Kombe la Amerika (Copa America) 2015 ambapo timu yake ililala kwa 1-0 dhidi ya Colombia. Kipigo cha mikwaju ya penati dhidi ya Paraguay kwenye Kombe la Amerika 2011 kinakaa kama sare kwenye rekodi hii. Neymar alishindwa kuzuia hasira baada ya kupoteza dhidi ya Colombia 2015. Alifanya vurugu ambapo mwamuzi Enrique Osses hakusita kumzawadia kadi nyekundu.

Nyekundu hiyo ilimuweka nje kwenye michezo miwili ya kwanza ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2018. Alirudi kwenye mchezo wa raundi ya tatu. Akapata kadi za manjano kwenye mchezo wa raundi ya nne na ule wa raundi ya tano na hivyo akalazimika kukosa mchezo wa raundi ya sita.

Kadi nyingine za manjano kwenye michezo ya raundi ya nane na ya tisa zilimuweka nje kwenye mchezo wa raundi ya kumi. Na endapo kungekuwa na raundi ya 19, nyota huyo wa PSG angeikosa pia kwa kuwa alipata kadi za manjano zaidi kwenye raundi ya 15 na ya 18. Kwa ujumla alikusanya kadi 6 za manjano kwenye michezo 14 ya kufuzu Kombe la Dunia.

Haya ni mashaka makubwa kwa Brazil kuelekea Kombe la Dunia miezi michache ijayo. Mwalimu Tite anatakiwa kuyafahamu na kujiandaa kukabiliana na mashaka haya. Wapinzani watakuwa wakifahamu vyema udhaifu huu wa Neymar na kuamua kujaribu kumuudhi kwa makusudi ili atende utovu wa nidhamu kwa rafu ama vurugu.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa Neymar atakosa uvumilivu na tahadhari kama ilivyo kawaida yake na hivyo kujikuta akipata adhabu na kukosa michezo muhimu. Sio mbaya kwa Tite kumtambua mbadala wa uhakika wa Neymar kabla ya safari ya Urusi. Na hapo ndipo inapokuja faida ya kukosekana kwake kwenye michezo ya kirafiki dhidi ya Urusi (leo Ijumaa) na dhidi ya Ujerumani (Jumanne).

Kwa vyovyote vile Tite angependa kuona nyota wake wote wakali wakicheza pamoja kwa mara ya kwanza tangu Novemba. Hata hivyo ni vizuri kocha huyu wa zamani wa Corinthians anapata ulazima wa kutafuta jibu la swali; ‘Itakuwaje Neymar akikosekana kwenye mchezo fulani mgumu na muhimu huko Urusi?’.

Itakuwaje iwapo Neymar atakosekana kwenye mchezo wa raundi ya 16 bora? Itakuwaje akiwa nje kwenye mchezo wa robo fainali? Nani atacheza vyema akitokea pembeni upande wa kushoto? Kuna machaguo mawili ya wazi. Ni Philippe Coutinho wa Barcelona na Douglas Costa wa Juventus. Hawa ndio waliojaribiwa kwenye michezo ya kufuzu aliyoikosa Neymar.

Kumchezesha Coutinho kwenye nafasi hii kunamaanisha kumrejesha kwenye nafasi yake ya asili, ya kushambulia kutokea upande wa kushoto. Ni mchezaji wa kiwango cha juu mno lakini pengine angefaa zaidi kucheza kama kiungo mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji. Huenda Tite atapendelea zaidi kumchezesha kwenye nafasi hiyo.

Douglas Costa ndiye anayeonekana kufaa zaidi akitokea pembeni kutokana na uwezo wake wa ajabu wa kukokota mpira, kasi na umahiri wa kupiga krosi. Inaundwa safu kali ya mashambulizi ambapo pembeni yake upande kulia anakuwepo Coutinho kama kiungo mshambuliaji wa kati. Kuna uwezekano mkubwa kuwa Tite atawapanga hivi kwenye mchezo wa Ijumaa dhidi ya Urusi.

Hata hivyo kwenye mchezo wa Jumanne dhidi ya Ujerumani upo uwezekano kuwa hatawapanga namna hiyo. Hiyo ni kwa kuwa atahitaji wachezaji wenye uwezo wa kuzima mipango ya wapinzani kwenye eneo la katikati ambalo lina wachezaji mahiri kwenye kikosi cha mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia.

Kutokuwepo kwa Neymar kwenye michezo hii ya kirafiki ni baraka iliyojificha kwa timu ya taifa ya Brazil. Tite atumie nafasi hii kjiridhisha na namna atakavyounda timu imara isiyo na mchezaji ghali zaidi duniani. Majeraha ya Neymar ni faida kwa Brazil angalau kwa sasa.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Naiona Taswira ya Township Rollers kwenye kivuli cha Wolayta Dicha

Tanzania Sports

Dondoo za kombe la Dunia….