in , ,

Kimbunga cha kushuka daraja EPL

 

Hakuna klabu inayopenda kushuka daraja, lakini kila mwisho wa msimu lazima timu tatu ziondoke ili nyingine tatu zipande Ligi Kuu ya England (EPL).

 

Msimu huu hauna tofauti, na hadi leo hii, timu zilizo kwenye mstari wa kushuka daraja ni Burnley, Queen Park Rangers (QPR) na sunderland.

Hata hivyo, hiyo haina maana kwamba hawa ndio watakaoshuka, kwani katika mechi tatu (Sunderland nne) zilizobaki kumalizika EPL zinaweza kujiokoa kwenye eneo hilo.

 

Timu zenye uhakika kabisa wa kubaki EPL ni zile zilizo kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya 10, huku zile zinazofuata – Everton, Crystal Palace na West Bromwich Albion wakiwa hawana shida  kwani wanahitaji pointi chache tu.

 

Tatizo kubwa ni kuanzia walio mkiani hadi nafasi ya 14, na hapa tuangalie nani yupo katika mazingira yapi na kipi kinatarajiwa.

Timu saba zina matatizo makubwa, na kwa mwenendo ulivyo kuna kila dalili kwamba Burnley na QPR wameshajielekeza kibla, wanasubiri muda tu.

 

Kimsingi timu hizo saba ndizo tarajali kwa ushukaji daraja na kosa moja tu linaweza kusababisha zikajikuta msimu ujao zikiwa kwenye Championships, yaani Ligi Daraja la Pili ya hapa.

 

Suala hili la kushuka daraja si ajabu likaamuliwa siku ya mwisho wa msimu ikiwa walio mkiani watajitutumua na kufanikiwa, kama ambavyo ubingwa wa Hispania unaweza kuamuliwa siku ya mwisho, ambapo Barcelona na Real Madrid wanakabana koo.

 

Msisimko wa nani angekuwa ubingwa kwenye ligi hii ulishaenda na maji baada ya timu na kocha mwerevu zaidi kuutwaa ubingwa huku wakiwa na mechi tatu mkononi, kwa hiyo walau vita ya kuepuka kimbunga cha kushuka daraja inatakiwa kutupa msisimko, hata kama kidogo.

 

ASTON VILLA

 

Aston Villa wapo nafasi ya 14 wakiwa na pointi 35 na wamebakiza mechi dhidi ya West Ham, Southampton na wanyonge Burnley.

Katika mechi tano zilizopita, walishinda mbili, kufungwa mbili na sare moja. Walifungwa na timu kubwa za Manchester.

 

Kwa mechi zilizobaki kuna kila dalili kwamba watabaki juu, maana kocha mpya amebadili mwelekeo wao na wanafunga mabao nyumbani na ugenini.

 

NEWCASTLE

 

Newcastle wapo nafasi ya 15 wakiwa na pointi sawa na Villa. Wamekuwa na mdororo usio wa kawaida kiasi cha washabiki kuandamana.

 

Wamebakiza mechi dhidi ya West Brom, wanyonge QPR na West Ham.

 

Newcastle wanaonekana kupoteza mwelekeo kabisa, wakifungwa mechi kama maji yanayoingia baharini, huku kocha wao, John Carver akidai ndiye bora zaidi EPL, wakati anashika mkia kwa rekodi ya kushinda mechi.

 

Wamepoteza mechi zao zote tano zilizopita dhidi ya Leicester, Swansea, Tottenham Hotspur na Liverpool.

 

Uwezekano wao wa kubaki EPL au kushuka ni nusu kwa nusu. Wana matatizo; washabiki wanamchukia mmiliki, Mike Ashley, kocha anawalaumu wachezaji wake kuwa wanacheza hovyo na timu imepoteza mechi zao nane zilizopita.

 

Chini ya Alan Pardew aliyehamia Palace, walivuna pointi 27 katika mechi 20, lakini Carver amepoteza mechi 11, sare mbili na ushindi mara mbili tu, yaani asilimia 13 tu ya mechi zote. Hii ni hali mbaya.

Hata hivyo si kosa la Carver, na kwa kuwa wana mechi dhidi ya QPR walio hoi na West Ham ambao hawapati wala kupoteza chochote wakishinda huenda wakabaki juu.

 

LEICESTER

 

Leicester wanashika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 34 na wamebakiza mechi dhidi ya Southampton na wenzao wanaowania kukiepuka kikombe – Sunderland na QPR.

 

Katika mechi tano zilizopita, wameshinda nne na kupoteza moja tu dhidi ya Chelsea. Katika mechi sita zilizopita wameshinda tano, hivyo kuna dalili nzuri kwao kubaki ikiwa wataendelea na asilimia hiyo ya ushindi.

Leicester ni kana kwamba wamenyanyua vichwa vyao kutoka mchangani na kuanza kutembea au kukimbia wakati Aston Villa kimsingi wanatakiwa wakiepuke kikombe hiki baada ya kuhuishwa na Tim Sherwood.

 

Walifanya vyema mwezi Aprili hivyo kwamba kocha wao, Nigel Pearson ametajwa kuwa kocha bora wa mwezi huo, licha ya kumtukana mwandishi kwamba ni mjinga na mbuni kutokana na swali alilomuuliza.

 

HULL

 

Tunakuja kwa Hull walio nafasi ya 17 na pointi 34 na wamebakiza mechi dhidi ya Burnley walio mkiani, Spurs na Manchester United siku ya mwisho ya msimu.

 

Katika mechi zao tano zilizopita wameshinda mechi mbili na kupoteza tatu. Ni vigumu kusema kwamba watabaki au la, itategemea na mechi hizo zilizobaki, lakini Steve Bruce amefanya jitihada ikiwa ni pamoja na kuwakong’ota Liverpool. Wameshajiandaa kwa maisha ya daraja la chini kwa kuwaambia wachezaji wajiandae kupunguzwa mishahara, vinginevyo wapambane wabaki.

 

SUNDERLAND

 

Sunderland wamo kwenye boti inayozama, na kwa sababu wapo nafasi ya 18 wakiwa na pointi 33 hata kama wana mechi nne zilizobaki, kikubwa ni kupata ushindi kujiondoa chini ya mstari.

Wamebakisha mechi dhidi ya Everton, Arsenal na Chelsea, zote timu nzuri na vibonde wenzao, Leicester.

 

Katika mechi tano zilizopita, Sunderland wameshinda mmbili, kwenda sare moja na kufungwa mbili.

Sunderland wana rekodi nzuri dhidi ya Chelsea, kwani walipata kuwachabanga nyumbani kwao Stamford Bridge na mechi ya kwanza waliwabana kwa suluhu.

 

Walimfuta kazi Gus Poyet walipoona meli inazama na kumkabidhi Dick Advocaat ambaye katika kazi ya ukocha ya miaka mingi hajapata kushuka daraja na timu. Advocaat anasema anaamini kwa asilimia 100 kwamba hawatashuka daraja na ameahidiwa kupewa mkataba wa kazi, maana kwa sasa alichoagizwa ni kunasua timu wasishuke daraja.

 

QUEEN PARK RANGERS

 

QPR wapo nafasi ya 19 na pointi zao 27, ambapo kocha wao, Harry Redknapp aliwakimbia alipoona mambo yanakwenda mrama, lakini akadai alikuwa akienda kufanyiwa upasuaji wa goti.

Baadaye alikiri kwamba moja ya sababu za kuondoka ni kwamba baadhi ya watu hawakuwa wakimpenda na walitaka akwame, akaamua kuanguka kabla ya kuangushwa.

 

Wamebakiza mechi dhidi ya Manchester City,

Newcastle na Leicester. Katika mechi zao tano zilizopita wameshinda moja, sare mbili na kufungwa mbili.

 

Je, wakiwa chini ya kocha pekee mweusi EPL, Chris Ramsey watabaki juu? Si rahisi, kwa sababu kuna uwezekano wakashuka daraja hata wakishinda mechi zote tatu zilizobaki, maana na wengine hawakai tu, wanatafuta ushindi.

 

Uwezekano wa kushinda mechi zilizobaki ni mdogo, kwani tangu kuanza ligi hawajapata kushinda mechi mbili mfululizo.

 

Ili wabaki EPL watatakiwa kushinda mechi dhidi ya Man City pale Etihad. Kumbuka, mara ya mwisho kuwafunga City kwenye ligi ilikuwa kule Maine Road, enzi hizo waziri mkuu alikuwa Tony Blair. Sasa keshapita Gordon Brown na sasa David Cameron kamaliza miaka mitano.

 

Wenyewe wanajua kwamba wanashuka, Ramsey atapewa mwaka mmoja zaidi klabuni ili asaidie kuwarejesha EPL kutoka Championships msimu ujao.

 

Atatakiwa kusuka upya ukuta wa timu, kwani katika mechi 35 wamefungwa mabao 61 msimu huu. Timu iliyo kwenye hali hii ni ile inayoshuka daraja

 

BURNLEY

 

Burnley wanaburuta mkia katika nafasi ya 20 wakiwa na pointi 26. Ni shida kuwa mkiani na wamebakiza mechi dhidi ya Hull, Stoke na Aston Villa.

 

Kwenye mechi zao tano zilizopita, Burnley waliopanda daraja msimu huu wamefungwa nne na kwenda suluhu moja. Hawa bora waanze kupaki mizigo yao kwa safari hata kama mechi ya mwisho walifungwa kwa tabu 1-0 na Manchester City. Ili walau wawe na matumaini ya kubaki Ligi Kuu, Burnley wanatakiwa washinde mechi zote tatu zilizobaki na kuomba mchanganyiko wa matokeo kwingineko, kitu ambacho ni kama muujiza.

 

Kocha Sean Dyche anaonekana kuwa mtu mzui na timu imepambana lakini tatizo hawafungi mabao ya kutosha, na bila hivyo hushindi, ndiyo maana wamekuwa wa mwisho.

 

Mechi zao nne za mwisho wamepoteza kwa bao moja kwa sifuri, laiti wangekuwa wanafunga mabao hawangekuwa hapo. Wanaye mshambuliaji matata, Danny Ings, anayetakiwa na timu zilizo kwenye nne bora, lakini ndio hivyo, wanaaga.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

LIGI YA EUROPA

Benteke kumbadili Sturridge Liverpool?