in

Karibu Kim lakini Taifa Stars imebadilika

Poulsen

Shirikisho la Soka nchini Tanzania, TFF limemteua Kim Poulsen raia wa Denmark kuwa kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars) ikiwa ni mara ya pili kukabidhiwa kuinoa timu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho hilo imesema Poulsen amesaini mkataba wa miaka mitatu kufundisha Taifa Stars ambayo hivi sasa iko katika kinyang’anyirio cha kutafuta nafasi ya kuchea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON pamoja na Fainali za Kombe la Dunia ambazo zote zitafanyika mwaka 2022 katika nchi za Cameroon na Qatar.

Poulsen amewahi kuwa kuinoa Taifa Stars kati ya mwaka 2012-2013 ambapo kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya vijana, Serengeti Boys iliyokuwa inaundwa na chipukizi kama vile Zuberi Ada, Dikcson Job, Ramadhani Kabwili, Ali Ng’anzi huku akisaidiwa na Bakari Shime

Kocha huyo anachukua nafasi ya Ettiene Ndayiragije raia wa Burundi ambaye hivi karibuni alifikia mwafaka na TFF kuvunja mkataba wake mara baada ya kukiongoza kikosi cha Taifa Stars kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani maarufu kama CHAN.

Ujio wa Poulsen unatarajiwa kuwa na sura nyingi ambazo kila upande utaona namna ambavyo mwalimu huyo anastahili au hakustahili. Pengine ujio huu unadhihirisha kuwa TFF kukiri walikosea kumwondoa katika nafasi yake awali. Poulsen aliondolewa mara baada ya uongozi mpya wa TFF chini ya Jamal Malinzi.

Wapo wengine ambao wanaamini Poulsen alitakiwa kukabidhiwa timu za vijana aendeleze kuibua vipaji kuanzia miaka 17 hadi 20. Wanaamini kuwa Kim ana kipaji cha kuvumbua na kuwanoa wachezaji chipukizi na hivyo angekuwa na tija zaidi kwa kuzalisha wachezaji wapya kuliko kukinoa kikosi cha wakubwa.

Tunafahamu kuwa Kim Poulsen alikuwepo katika soka Tanzania miaka takribani sita iliyopita. Hata hivyo mwaka 2012-2013 si sawa na mwaka 2021 katika kandanda kwa Tanzania. yapo mabadiliko mengi katika kipindi ambacho hakuwepo nchini kama kocha.

Kuibuka kwa wachezaji wapya, ushindani miongoni mwa wachezaji na timu hali ambayo inaibua ubora wa wachezaji na ufundi wao kuongezeka zaidi. vilevile wachezaji wa kigeni wammetoa mchango mkubwa kwa wachezaji wazawa hali ambayo inaleta ushindani kupata namba na kuonesha kiwango bora ambacho mwalimu anatarajia. Kingine aina ya wachezaji imeongezeka kuliko wakati ambao alikuwa anafundisha soka Tanzania.

Angaizo langu kwa kocha Kim Poulsen ni kwamba asije kufanya makosa kama rafiki yangu Marcio Maximo alipokuja kuwanoa mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga  kwa kumleta mshambuliaji Jaja kwa mawazo ya kucheza soka la zama zake na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba. Soka la sasa Tanzania lina washambuliaji wachache wa kiwango cha kama John Bocco,Mbwana Samatta na Ditram Nchimbi.

Lakini tumejaliwa kuwa na viungo na mawinga hodari kama Deus Kaseke,Baraka Majogoro,Yusuf Mhilu,Said Ndemla,Frank Domayo,Ramadhani Rajab,Mzamiru Yassin na mabeki hodari kama Bakari Mwanyeto,Edward Charles,Shomari Kapombe, Mustapha Yassin na wengineo.

Hivyo basi Kim anaingia katika soka letu kwa sasa likiwa na wimbi la wachezaji ambao wanacheza mechi chache za Ligi Kuu na kukosa ufanisi katika kazi yao.

Kim anakuja kuinoa Taifa Stars ambayo inatarajiwa kunufaika na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ambao wanashiriki mashindano ya kimataifa lakini wana mtihani mkubwa mbele yao waende wapi ikiwa Taifa Stars nafasi zao ni finyu? Hili tunatarajia Kim Poulsen atalipatia ufumbuzi.

Jambo lingine ninalojiuliza, Kim ambaye ni kocha mkimya sana, atatumia mbinu gani kuhamasisha mashabiki wa soka nchini kuipenda timu yao ya Taifa Stars kama zama za Marcio Maximio? Huu ni mtihani ambao utapaswa kuvukwa kwa matokeo mazuri na hamasa kwa mashabiki. Kinyume cha hapo presha kwake itakuwa kubwa zaidi.

Je TFF wanakiri makosa yao?

Kwa viongozi wetu wa TFF walitakiwa kujieleza zaidi tangu walipomwondoa Kim Poulsen katika nafasi yake. hawakupata nafasi ya kujibu kuwa wana mipango mikubwa ambao labda Kim asingeliweza kwa wakati ule. Hata hivyo tangu kuondoka Kim Poulsen tulifanikiwa kufuzu Fainali za AFCON tukiwa na kocha Emmanuel Amunike raia wa Nigeria, kisha tukafuzu CHAN tukiongozwa kwenye fainali hizo na Ettiene Ndayiragije.

Pengine mafanikio hayo tunaweza kumtambia Kim Poulsen, lakini lazima viongozi wetu watujibu maswali machache. Je, sababu zilizomuondoa Kim Poulsen zimerekebishwa mpaka arudishwe au kuna uhitaji kiasi gani wa huduma yake Taifa Stars?

Je, kwanini tumrudishe Kim, tumekosa makocha wengine wenye uwezo mkubwa kumzidi? Kim aliondolewa Taifa Stars na sasa anarudishwa akiwa na lipi jipya?

Vilevile je, tunataraji ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa mbinu za kocha ambaye hajafundisha soka la ushindani miaka ya karibuni? Ni muhimu TFF watuambie ni kwa vipi Kim Poulsen amefanikiwa katika kazi yake baada ya kuondoka Tanzania na kuwa sifa ya kurudishwa tena kwenye kikosi hicho.

Je, Tanzania tunashindwa kupiga hatua kwenye kandanda kwa sababu ya makocha au mipango yetu haizalishwi wala kuzalisha wanakandanda wenye kuleta mafanikio?

Hadi sasa malengo makubwa yaliyomo TFF ni kufuzu AFCON na Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022. Mambo hayo mawili ndiyo yanaweza kutufukisha huko tukiwa na Kim Poulsen? Kama jibu ni ndiyo, maana yake hata Fainali za mwaka 2014 na 2018 tungeweza kufuzu kama tungelibaki na kocha huyo.

Nimalize kwa kumkaribisha tena Kim, kuwa sisi watanzania bado tunaongoza kwa kupenda mchezo wa soka hapa Afrika mashariki, kwahiyo kupata matokeo mabaya kutasababisha kushusha ari ya mashabiki.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SSC

Mafanikio ya Simba ni kilio cha Taifa Stars..

Tanzania Sports

Kina Ajib hawaoni wivu kwa kina Chama ?