in

Je wanasoka Tanzania wanafeli sababu ya lugha?

Kwa miaka mingi pamekuwa na mjadala kuhusu uwezo wa kuzungumza lugha fulani kuwa kigezo cha mafanikio. Inaaminika kuzungumza lugha ya Kiingereza inamsaidia mwanamichezo kujiuza,kutambulika,kununuliwa na kupata mafanikio kwenye eneo lako. Hiyo ni dhana iliyojengeka miongoni mwa watu mbalimbali, wanamichezo wenyewe na mashabiki wao.

Wakati mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani maarufu kama CHAN, mjadala uliopo ni kuhusiana na lugha kwa wachezaji wa Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla wake. Katika mjadala wa sasa walengwa ni wachezaji wa Tanzania ambao wanatajwa kutokuwa mahiri wa kuzungumza lugha fulani.

Inafahamika kuwa suala la uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali limezungumziwa na wataalamu kuwa na manufaa zaidi kwa mtu husika. Mathalani mtu mmoja anaweza kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha za Kimpoto, Kimatengo, Kingoni, Kiswahili, Kiingereza, Kisukuma, Kireno, Kihispania, Kifaransa na kadhalika.

Rafiki yangu mmoja ni mwanadiplomasia ambaye anao uwezo wa kuzungumza lugha za Kimataifa kama Kireno, Kiingereza, Kihispania, Kiswahili, pamoja na zile za makabila za kama vile Kingoni na Kimatengo na Kinyanja. Hapo kuna lugha za kikabila na kimataifa. Wapo wenye uwezo wa kzungumza lugha moja tu Kiswahili hibyo hawajui zingine za makabila.

Turudi kwenye michuano ya soka inayoendelea nchini Cameron inayohusisha timu za taifa za wachezaji wa ndani ya bara la Afrika. Baadahi ya mashabiki na wana michezo wengine wanawasifia wachezaji wa Burundi na Rwanda, jinsi walivyo mahiri kuzungumza lugha tatu za Kifaransa, Kiswahili na Kiingereza.

Wanasema wachezaji hawa wanasimama kama mifano ya vijana wengi kutoka kwenye nchi za Afrika mashariki wenye uwezo wa kuzungtumza lugha tatu kwa umahiri. Warundi na Wanyarwanda wanasifika kwa kujiamini na wana uwezo wa kujiuza popote duniani katika talanta zao ambazo wanazo.

Aidha, baadhi wanashauri kuwa tungeweka mkazo zaidi kujifunza kile ambacho hatukifahamu na kile ambacho tunakifahamu kidogo. Wanasisitiza kuwa dunia ya sasa kung’ang’ania na kukipa kipaumbele kile unachokijua tu ni hatari. Kwamba ni lazima kutoa kipaumbele kwa lugha ambayo hatuifahamu vema ili kupata mafanikio.

Huo ndio msingi wa hoja yangu ya leo, kwamba kutokana na mjadala na maoni ya mashabiki na baadhi ya wanamichezo tunatakiwa kuzingatia lugha ya Kiingereza ili kupata mafanikio. Hoja inayoibuliwa hapo ni kwamba wachezaji wa Ligi Kuu wa Kitanzania ili wafanikiwe wanatakiwa kuzungumza lugha zingine ikiwemo Kifaransa na Kiingereza. Yaani ili Yassin Mustafa anunuliwe kwenye soka la kulipwa lazima awe mahiri katika lugha za kimataifa. Au Baraka Majogoro akitaka kwenda kucheza Ulaya anatakiwa kukijua kiingereza.

Baada ya kusema hilo tugeukie upande mwingine, je ni kweli kwamba suala la lugha likwaza maendeleo ya wachezaji wa kitanzania? Mrisho Ngassa alikwenda kufanya majaribio West Ham. Ni mchezaji pekee wa kwanza wa kitanzania kucheza dhidi ya Manchester United katika mchezo wa kirafiki nchini Canada. Nizar Khalfani alikuwa nyota katika Ligi Kuu Canada na alikuwa maarufu huko.

Haruna Moshi alikwenda Sweden, wakati Henry Joseph Shindika alikwenda kukipiga nchini Norway. Seleman Matola alikwenda kukipiga Supersport United, wakati Simon Msuva alisajiliwa na Difaa El Jadida kabla ya kununuliwa na Wydad Casablanca. Himid Mao alisajiliwa na ENPPI ya Misri. Elias Maguli anakipiga FC Plutinum ya Zimbabwe. Rashid Mandawa alikwenda kucheza soka Botswana. Manyika Peter na baadhi ya wanasoka wa Tanzania walijazana Ligi Kuu Kenya.

Nataka kusema kama lugha ndiyo kikwazo, imekuwa Simon Msuva ambaye hazungumzi Kiarabu lakini amepenya Ligi Kuu Morocco? Hali kadhalika kwa Himid Mao aliyeko nchini Misri na wanakandanda wengine waliokwenda baadhi katika nchi za Ulaya.

Katika suala hilo hilo tunaweza kuwatazama wachezaji wengine wa nje kama vile Dani Alves ambaye ni nyota aliyecheza klabu za Juventus, Barcelona, Sevilla na PSG anazungumza zaidi lugha ya Kireno na Kihispaia. Hakukijua vizuri kiingereza.

Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane hakijui Kiingereza kwa ufasaha lakini anazungumza Kitaliano, Kihispania na Kifaransa. Amepata mafanikio kwenye soka si kwa sababu ya lugha hizo bali kwa kuwa alikuwa na kipaji cha kucheza soka. Pili amepata mafanikio akiwa kocha bila kujua lugha ya kiingereza.

Tanzania Sports
Zinedine Zidane

Jamaica ni taifa ambalo linataliwa na Uingereza hadi leo katika mifumo yake kwa mtindo wa Ufalme. Kama suala la lugha lingekuwa kigezo basi tungeona wanasoka wengi wa Reggae Boys wakitamba ulimwenguni. Canada vile vile na mataifa mengine kama Afrika kusini na kwingineko.

Wapo wachezaji ambao hawajui kabisa kutamka maneno ya lugha ya Kiingereza lakini wamefanikiwa. Wengi wa wachezaji wanaotoka Amerika kusini hawakijui Kiingereza, lakini wanazidi kutoboa kila kukicha si kwa sababu ua nchi zao pekee bali uwezo wao wa kusakata kandanda.

Edgar David galacha wa soka wa Uholanzi alisifika kwa kujua lugha nyingi. Angeweza kuzungumza Kiholanzi, Kihispania,Kitaliano na Kiingereza vyovyote alivyojisikia siku hiyo lakini hilo haliwezi kusemwa kilikuwa kigezo cha yeye kufanikiwa kuzichezea Juventus,Barcelona na nyinginezo.

Kipaji cha mwanasoka hakiwezi kumnyima nafasi ya kutamba. Kama anacho kipaji maalumu au cha kipekee lazima atawindwa kwa udi na uvumba. Mbwana Samatta alinunuliwa na Genk kwa sababu waliamini kipaji chake kitakuwa na manufaa klabu kwao na wangepata fedha nyingi kwenye mauzo.

Samatta alicheza kwa mafanikio Genk kisha akauzwa kwenda Aston Villa hali ambayo imewapa nafasi Genk kunufaishwa na mauzo ya nyota huyo. Kilichouzwa ni kipaji chake sio uwezo wake wa kuzungumza lugha ya Kiingereza au Kifaransa.

Tunakubaliana kwa namna kuijua lugha ya Kiingereza ni jambo muhimu lakini sio kitu kinachomfanya mchezaji anunuliwe na timu za Ulaya au kwenye soka la kulipwa. Wapo w achezaji wananunuliwa na klabu mbalimbali barani Afrika kutoka Brazil lakini hawakijui Kiingereza, bali wanazungumza Kireno. Kinachowaleta ni uwezo wao wa kucheza soka.

Kama wachezaji wa kitanzania watakuwa na vipaji maradhawa naamini hakuna timu itaacha kuwanunua. Katika dunia hii imeshuhudia kipaji cha Dwight Yorke aliyetokea huko visiwani Trinidad&Tobago akitamba katika jezi za Manchester United. Kilichomfikisha hapo ni kipaji chake sio uwezo wa kuzungumza Kiingereza. Kwa mchezaji suala la uwezo wa kuzungumza lugha ni bonsai tu ya maisha yake.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
soufiane rahimi

Sofiane Rahimi ni ‘hirizi’ ya Morocco

Azamfc

Tadeo Lwanga na Jonas Mkude waanze pamoja…