in

Je, klabu zinaweza kuvunja utaratibu kwa mchezaji pendwa?

Sergio Ramos

KWENYE eneo la kusimamia msimamo wa kusaini mikataba mpya huwa ninapenda mwenendo wa aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger. Kocha huyu alikuwa miongoni mwa binadamu wa ajabu ambaye alikuwa tayari kusimamia utaratibu wa klabu yake kuliko kuyumbishwa na mchezaji. 

Lakini vile vile alikuwa tayari kusimamia msimamo wake kuliko kuyumbishwa na mashabiki. Mwingine ni Alex Ferguson ambaye kwa namna moja ama nyingine anafanana kimaamuzi na Wenger. 

Tofauti ya makocha hawa ni kwamba Ferguson amejulikana hata hadharani ‘ugomvi’ wake na wachezaji. Wenger hakuwa mtu wa namna hiyo. Kwa mfano sakata la usajili wa David Beckham kwenda Real Madrid, ama vitimbi vya Roy Keane hadi kuondoka Manchester United kulikuwa na mkono na ghadhabu za wazi za Ferguson.

Kwa upande wa viongozi huwa ninapenda kuwafuatilia Florentino Perez jinsi anavyosimamia msimamo wa klabu na ile binafsi. Kuna wakati misimamo yake inaathiri ufanisi wa klabu ndiyo maana amewahi kuachia ngazi huko nyuma kupisha wengine kabla ya kurudi madarakani na sera yake Galacticos. 

Wasomaji wa TanzaniaSports wanatakiwa kufahamu kuwa Perez amewahi kusimamia maamuzi magumu ya usajili wa Luis Figo kutoka Barcelona kwenda Real Madrid lakini akasimamia pia kumwondoa nyota huyo mara baada ya kufikisha miaka 30, pamoja na nyota kadhaa waliotumikia na kuondolewa klabuni chini ya uongozi wake.

Kwa utaratibu wa klabu ya Real; Madrid mchezaji mwenye umri zaidi ya miaka 30 huwa anaongezewa mkataba wa mwaka mmoja tu. Hilo ndilo lililowakuta mastaa kibao wa Real Madrid, licha ya baadhi kuondoka wenyewe akiwemo Cristiano Rpnaldo alioyeuzwa kwenda Juventus Turin ya Italia. Na sasa zamu hii imekuja kwa marafiki wawili Sergio Ramos na rafiki yake Lucas Vazquez pamoja na kiungo veterani Luka Modric.

Kwa wasomaji wa Tanzaniasports iko hivi, Sergio Ramos ana miaka 34 kwa sasa. Luka Modric ana miaka 35, na hali kadhalika Lucas Vazquez anaelekea huko. Mikataba ya wachezaji hawa wote watatu inaelekea ukingoni. Modric, Ramos na Vazquez wote wanatumikia misimu ya mwisho na huenda wakawa wachezaji wa Madrid au wakaondoka. 

Mjadala mkubwa tulionao leo hii ni Sergio Ramos kukataa ofa ya mwaka mmoja kubaki Real Madrid. Kwamba Real Madrid inataka kulinda utaratibu wake wa kutoa mkataba wa mwaka mmoja kwa mchezaji ambaye amepita miaka 30. Lakini Ramos anahitaji mkataba wa miaka miwili kinyume cha utaratibu wa klabu. 

Lucas Vazquez naye hajazungumza suala la mktaba mpya na haonekani kuwa ataendelea kubaki klabuni hapo. Luka Modric alishabainisha hamu ya kubaki klabuni hapo chini ya Zinedine Zidane. 

Endapo Lucas Vazquez ataondoka klabuni hapo litakuwa pigo kubwa sana kwa Zidane kwa sababu yeye ni miongoni mwa ‘askari waaminifu’ katika kikosi chake. Lucas Vazquez amekuwa akitumwa kucheza namba nyingi tofauti. Kuanzia winga wa kulia, kushoto na beki wa kulia. 

Msimu wa 2020/2021 Lucas Vazquez amekuwa mbadala wa nafasi ya beki wa kulia akiwa amecheza mechi kadhaa kuziba pengo la Carvajal. Pia anatumika kama mchezaji wa kupunguza dakika za kucheza kwa Dani Carvajal. 

Benchi la ufundi linamlinda Carvajal dhidi ya majeraha hivyo Lucas ndiye tegemeo lao katika nafasi ya beki wa kulia. Kwa mantiki hiyo anakuwa mchezaji muhimu kikosini, lakini cha ajabu Real Madrid haijaongeza mshahara katika ofa mpya. Yaani Lucaz Vazquez ameletewa ofa ya aina ileile na mshahara uleule anaopata sasa, hali ambayo imesababisha agome kusaini mkataba huo.

Modric alianza msimu kwa kusuasua lakini amerejea kwenye kiwango chake na kuonesha cheche zilizopa ushindi Real Madrid. Cheche hizo zimesababisha mjadala tena kama Real Madrid watamruhusu aondoke ama abakizwe klabuni. Lakini Modric akibaki Real Madrid naye atakumbana na kanuni ileile ya mchezaji aliyevusha miaka 30 kupewa mkataba wa mwaka mmoja. 

Kama Ramos atashindwana na Real Madrid (hali ambayo inaashiria bado itakuwa vigumu kubaki) ni wazi hata Modriuc ataruhusiwa kuondoka klabuni. Changamoto inayokuja ni nani atapokea majukumu ya Ramos kikosini? Na vile viweje klabu ivunje utaratibu wake sababu ya nyota hao? 

Hapo ndipo ulipo mtihani kwa vilabu kuamua kuvunja utaratibu wao ama kuchukua maamuzi magumu dhidi ya wachezaji pendwa. Ferguson aliruhusu miamba kama Ruud Van Nistelroy,David Beckham, Gabreil Heinze na Roy Keane kuondoka klabuni, kama ilivyokuwa kwa Arsene Wenger alivyowaachia Theiry Henry,Patrick Vieira,Matheiu Flamini,Ashley Cole, Robin van Persie na wengine kwenda timu zingine. 

Takwimu za utafiti wa vyombo vya habari nchini Hispania zinaonesha hadi sasa takribani mashabiki 700,000 wanatajwa kupiga kura ya maoni kuamua kama Ramos abakie klabuni ama akubaliwe kuondoka. Asilimia 62 ya mashabiki wanasema utaratibu wa klabu lazia ufuatwe na endapo kapteni wao Sergio Ramos anataka kubaki lazima akubaliane nao.  

Halafu kuna mashabiki wengine asilimia 38 wanapendekeza utaratibu wa klabu uvunjwe ili kupata nafasi ya kumbakiza Sergio Ramos. Yaani badala ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja wampe ule wa miaka miwili anaotaka. 

Lakini je, nini kitatokea kama Ramos atashikilia msimamo wake kutoendelea Real Madrid? Hilo ndilo swali wanaloulizana mashabiki wa klabu hiyo licha ya kukubaliana kuwa utaratibu ufuatwe ama uvunjwe lakini wanaamini bado nahodha huyo ni mchezaji muhimu kikosini. 

Hata hivyo kura za maoni zinaonesha asilimia 37 wanaamini nyota huyo ataondoka klabuni hapo, lakini asilimia 34 ya mashabiki wanaamini atabakia klabuni kwa utaratibu wa mkataba wa mwaka mmoja. Asilimia 29 wanaamini atapewa mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja. 

Swali lingine linalotamba sasa; je nani yuko sahihi kati ya Klabu na Sergio Ramos? Kwamba klabu kushikilia utaratibu wake ama Ramos kushikilia msimamo wake? Asilimia ya 76 ya kura za maoni wanaamini Real Madrid iko sahihi kusimamia utaratibu wake. 

Asilimia 75 ya mashabiki wanaamini kuwa Sergio Ramos hana mbadala, kwamba lazima klabu ichukue hatua kwa kuhakikisha nyota huyo haondoki. Lakini asilimia 37 wanaamini wapo nyota wawili wanaweza kuchukua mikoba yake, David Alaba, Dayot Upamecano na Pau Torres.

Hapo ndipo ulipo mtihani, klabu inaweza kuvunja utaratibu wake ili kumpendelea nyota wao? Tusubiri na kuona.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Sven Vandenbroeck

Tusisahau kukisifu kichwa cha Sven Vandenbroeck

Shikalo

Kwanini Shikalo ni bora kuzidi Metacha ?