in , , ,

Jamal Malinzi, Usiniulize alipo Yohana Nkomola

Karibu, karibu kwenye hii barua, barua ambayo kwangu mimi niya yangu ni kukupa pole na hongera. Sina nia nyingine mzee wangu. Pole kwa matatizo ambayo uliyapata.

Kuna wakati nilitumia muda wangu kuja kukutembelea wakati ukiwa na matatizo hii ni kuonesha thamani yako ilivyo kubwa sana kwenye mpira wetu hapa Tanzania. Nakupa tena pole kwa yote ambayo yalikukuta.

Najua jana yako imebaki na kumbukumbu, kumbukumbu ambazo huwezi kuzifuta, kumbukumbu ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuja na nguvu kubwa sana kwenye maisha yako hasa baada ya kufanikiwa kurudi tena uraiani. Hongera kwa hilo.

Hongera kwa sababu leo yako ni imara zaidi kwa sababu ya ugumu wa jana yako. Hongera kwa sababu leo yako ni ya tahadhali zaidi baada ya kujikwaa kwa bahati mbaya jana. Hongera kwa kuongeza umakini na tahadhali kwenye kila hatua ya leo.

Mzee wangu wakati haupo uraiani nchi yetu ilishuhudia uhuru wa mpira, uhuru ambao tuliupata baada ya kukaa miaka 39 bila kwenda AFCON, lakini mwaka jana tulifanikiwa kwenda AFCON. Najua unatamani kujua kiwango na matokeo ya timu yetu ya taifa kwenye michuano hiyo ya AFCON.

Mzee Malinzi, hongera kwa sababu wewe pia ni moja ya watu ambao walitengeneza njia..

Matokeo na kiwango cha timu yetu ya taifa kwenye michuano ile siyo jambo kubwa sana kwetu sisi. Ukubwa wa jambo letu ni sisi kuiona timu yetu ya taifa ya Tanzania “taifa stars” kuiona ukiwa kwenye michuano hii mikubwa baada ya miaka 30!

Hongera sana mzee Malinzi, hongera kwa sababu wewe pia ni moja ya watu ambao walitengeneza njia iliyoweza kutufikisha kwenye michuano hii ya AFCON. Mafanikio haya yalianzia kwenye nyayo zako.

Ulituaminisha kwenye kutembea kwa kwenda mbele, tuliamini kupitia wewe kila kitu kinawezekana baada ya wewe kutuletea michuano ya AFCON kwa vijana walio chini ya Umri wa miaka 17 hapa nchini. Hongera sana kwa hilo mzee wangu.

Pole kwa kushindwa kushuhudia ukiwa uwanjani wakati michuano uliyoipigania ije Tanzania ikiwa inafanyika kwenye ardhi yako ya dhahabu. Pole lakini nakupongeza kwa mapambano yako.

Mapambano ambayo yalianzia kwenye maandalizi ya kuandaa timu za vijana, timu ambazo ulizichuja, ukaziweka kambi kwenye shule ya Alliance school ya jijini Mwanza.

Vijana waliweza kupata nafasi ya kusoma huku wakiwa wanafundishwa mpira kwa kuandaliwa kwa ajili ya kucheza mechi za kufuzu kwenda kwenye michuano ya Afcon ya vijana walio chini ya miaka 17.

Ndani ya maono yako tulifanikiwa kwenda Gabon, ulitengeneza kikosi ambacho kilikuwa na vijana ambao walifanikisha tufike Gabon kwenye michuano ya vijana ya AFCON walio chini ya miaka 17, hii ilikuwa mwaka 2018.

Mwaka ambao ulibeba kikosi imara. Hofu yangu ni wewe utakapotaka kuanza kuniuliza ni wapi walipo baadhi ya wachezaji mahiri kwa kipindi hicho.

Usitie shaka Ramadhani Kabwili yuko Yanga, mpaka sasa hivi anajaribu kujipenyeza kuwa golikipa namba moja, anaonekana kama kashiba sana, uzito wa ugali ndani ya tumbo lake unamfanya aendelee kuwa golikipa namba 3 wa Yanga .

Unamkumbuka yuko aliyebatizwa jina la Marcelo? Nickson Kibabange? Yule kwa sasa yuko na kaka yake Simon Msuva timu moja huko Morocco, sema kuna watu nasikia wanataka kumfanya kuwa mrithi wa Gadiel Michael pale Jangwani. Wengi tunaombea mpango huu usifanikiwe!

Yule Dickson Job ndiyo anatengenezwa kuwa nahodha ajaye wa Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania. Ana kila sifa ya kuwa kiongozi na yuko sehemu nzuri ambako ndiko kulipo kile chuo kikuu cha soka hapa nchini.

Hofu yangu ni kwa Kelvin Naftal Sijui alipo, angalau Ally Ng’anzi namuona pale Alliance FC akiwa mchezaji wa kutumainiwa wa Alliance FC, huyu maisha yake hapo Alliance FC siyo marefu sana, amebakiza muda mfupi asogee karibu kwenye jiji la biashara hapa nchini.

Karibu sana tena mzee wangu, naogopa sana swali la yuko wapi Yohana Nkomola. Mshambuliaji ambaye alitabiriwa kuwa ndiye mrithi wa kina Mbwana Samatta?

Mzee wangu Jamal Malinzi, kwangu mimi mara ya mwisho kumuona Yohana Nkomola ni kipindi kile yuko Yanga SC, mpaka muda huu Sijui alipo, natamani sana nijue alipo, jibu la sehemu alipo nitakuletea kwenye barua inayofuata, barua ambayo itakuwa na majibu ya wapi walipo hata wenzake na Kelvin John ambao walicheza AFCON ya vijana walio chini ya miaka 17 2019 hapa nyumbani?

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ndemla ana kipaji, kwanini makocha humweka benchi ?

Tanzania Sports

Villa watarudia makali?