in , , ,

ILI TUFANIKIWE KISOKA MALINZI NENDA HIVI……

 

BAADA ya kuchaguliwa kuiongoza TFF akiwa rais wa pili wa Shirikisho hilo la soka la Tanzania baada ya Leodgar Tenga aliyemaliza vipindi viwili, Jamal Malinzi ameanza kwa kupanga safu zake za utendaji katika uongozi wa soka ndani ya nchi yenye mfumo wa kuangalia vitu vingi si kwa sifa za utendaji wa mtu bali kwa misingi ya huyu ni nani kwetu na yule ni nani kwa wale!

Nchini Tanzania mtu anaweza kuwa na sifa zilizotukuka za kupeleka mbele jambo lenye manufaa kwa umma, akaanza kulipeleka mbele jambo hilo huku kila mtu akiyaona mabadiliko chanya lakini akapotezwa kwa sababu tu amefanya jambo la kumkera mtu au la kukera kikundi fulani cha watu! Haijalishi weledi wa mtu huyo, atatoswa tu na kuwekwa kwenye nafasi yake mtu ambaye uwezo wake ni wa chini mno ili mradi tu yuko tayari kuramba viatu vya wafanya maamuzi!

Jamal Malinzi ameanza kulaumiwa na wadau wengi kwamba ameanza kuonesha kuwa mtu wa visasi kwa kuanza mchakato wa kusitisha ajira ya Katibu Mkuu Angetile Osiah kwa kumpa likizo ya malipo hadi mwisho wa mkataba wake. Lawama hizi za wadau hazimtendei haki Malinzi kwani anachokifanya si kisasi bali kujenga timu ya watendaji ndani ya TFF watakaofanya kazi bila migogoro, kwa kuaminiana, bila kuwindana na bila kukosa kujiamini miongoni mwao.

Kama mtu wazi wazi alishiriki, kwa njia halali na za ujanja ujanja, kukupinga usigombee uongozi halafu unapenya kwa juhudi kubwa kisha unagombea na kushinda, utafanyaje kazi bila chuki na migongano na aliyeshiriki kukujengea ukuta usigombe uongozi? (Kama ni kweli) Ni sahihi kuachana na mtu huyo ili ukianza kazi, taasisi ifanye kazi tu na isifanye kazi ya kuchukuliana hatua na kutatua migogoro huku mambo yakiwa hayaendi. Mtu aliyekupinga unaweza kumbadili msimamo na kumjumuisha kundini kama utendaji wake ni wa hali ya juu isivyomithilika, uliojaa ubunifu mkubwa wa kujenga na hakuna mwingine mwenye uwezo wake.

Tunachotaka kuweka sawa hapa ni kwamba tumpe huru Malinzi apange safu zake kadri atakavyoona inafaa si kwa ‘ushkaji’ bali kwa kuzingatia uwezo na ubunifu wa atakaowaweka kundini kufanya kazi naye. Ni kweli asiwatupe hata waliompinga kama wana sifa za ziada za kuinua soka yetu.

Kimsingi, ahadi alizotoa wakati akijinadi kwa uchaguzi uliomuingiza madarakani, zinavutia sana. Ahadi za soka ya vijana, shule za kanda za soka, kuimarisha kamati ya ufundi kwa kuigawa katika majukumu tofauti,mafunzo kwa wataalam wa soka (makocha) wa kitanzania, mafunzo kwa waamuzi na wataalam wa kazi husika tu kushiriki kuamua kuhusu tuhuma za watendaji wa kazi hiyo kama uamuzi wa soka, miongoni mwaahadi nyingine, ni mipango yenye tija ya kuendeleza soka yetu.

Ili mipango hiyo mizuri ilete tija iliyokusudiwa, lazima iwe katika maandishi-MPANGO WA TFF WA MAENDELEO YA SOKA TANZANIA. Ndani ya mpango huo kuwe na mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Ndani ya kila mpango kuwe na mikakati ya kuufanikisha ambapo chini yake kunakuwa na shughuli za kufanyika kufanikisha mikakati hiyo, nani wa kuishghulikia na muda wa kukamilisha shughuli hizo.

Kwa mfano, Mpango:- Soka ya vijana wa umri tofauti. Mkakati 1: Kuhakikisha kila klabu inakuwa na timu za watoto wa chini ya miaka 14, 17 na 21. Shughuli za kufanya:- (1) kukutana na wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa mkakati huu, muda wa utekelezaji: mpaka Januari 31, 2014. Watekelezaji ni…. (2) TFF kufuatilia utekelezaji, muda wa utekelezaji: endelevu. Watekelezaji ni… (3) kuandaa mashindano ya umri tofauti: Muda wa utekelezaji, kuanzia Julai 1, 2015. Watekelezaji ni…. nk .

Mkakati 2: kujifunza toka kwa wengine jinsi wanavyofanikisha mpango huu.Shughuli za kufanya: (1) kufadhili matembezi nje ya nchi, hasa Ulaya, ya mafunzo ya viongozi wa klabu za soka za Tanzania: muda wa utekelezaji: mpaka Julai1, 2014. Watekelezaji ni…. (2) TFF kuwezesha mafunzo hapa nchini toka kwa wataalam toka nje: Muda wa utekelezaji,kuanzia Februari 1,2014. Watekelezaji ni…. nk. Mipango yote kutokana na ahadi za rais Malinzi na mawazo mazuri ya wadau wengine, yawemo kwenye mpango huo ulioandikwa unaojumuisha hayo yote.

Huu ni mfano tu. Kama ushauri huu ukikubalika, TFF itafute wataalam waliosomea na waliobobea katika kutayarisha mipango hiyo kwani hili ni suala la kitaaluma. Wawapate wataalam hao, waingie nao mkataba wa kuwatengenezea mipango hiyo ya vipindi maalum kama miaka mitatu mitatu ambapo kila baada ya muda huo, tathmini ya utekelezaji inayojumuisha utekelezaji, mafanikio na mikwamo hujadiliwa na TFF kujipanga upya kwa mpango mpya wa miaka mitatu inayofuata.

Ni kwa njia hii tu, rais Malinzi na timu yake ya uongozi watafanikiwa kuendeleza mbele soka yetu kwani kila jambo litafanyika kwa kumbukumbu, likionesha wajibu wa kila mdau wa soka kiutekelezaji na likipangiwa muda wa kuanza na/au kukamilisha utekelezaji. Hapo tutakwenda.

Kama tungeenda hivyo tangu awali, uongozi wa rais Tenga usingemaliza miaka minane kwa kujenga mifumo ya utawala tu. Ujenzi wa mifumo hiyo ungepewa muda wa kukamilika na mpira ungepata muda wa kuchezwa kulingana na mahitaji ya sasa ya dunia ya soka ya leo.

Aidha, njia hii itafanya shughuli za uendelezaji wa soka yetu zikawa endelevu kwani uongozi mmoja ukitoka madarakani utakabidhi mpango huo kwa uongozi unaofuata. Hivi ndivyo kina Burkina Faso, Ethiopia, Cape Verde na wengine waliokuwa chini yetu walivyotuacha kwani sisi tumekuwa watu wakuanza vitu vipya kila uongozi mpya unapoingia madarakani. El Maamry, Mohammed Mussa, Muhidin Ndolanga, Tenga na kadhalika walirithi ofisi katika kuonesha kwamba waliowatangulia walikuwa hawajui kitu na kuvunja yote, kuanza upya!

Kwa utaratibu huu tulioushauri hapa, kwenye kampeni za siku za usoni tutasikia ubunifu wa wagombea wa kuhakikisha utekelezaji wa mipango itakayokuwepo badala ya hali iliyojitokeza kwenye kampeni zilizopita ambapo kila mgombea alitoa ahadi zake, utadhani alikuwa anaomba uongozi kwenye taasisi yake binafsi! Hii haikustaajabisha kwani mipango ya TFF ya maendeleo ya soka haikuwepo.

Kwa hiyo ili tuendelee kisoka Malinzi anapaswa aende hivyo. Aachane kabisa na kipaumbele cha Yanga na Simba kwani akishaingia kwenye mtego wa yeye na watu wake kuisaidia mojawapo na kuiumiza nyingine ili ipatikane furaha ya baadhi ya watu, moja kwa moja tutakuwa hatuendi kwa kasi ya wenzetu wenye “Yanga na Simba” zao pia. Kuingia kwenye mtego huo kutamaanisha kupindisha kanuni, kufanya upendeleo, kuwajengea watu mazingira ya ushindi na baya kuliko yote upeo wetu wa soka utaishia hapa hapa kwa Yanga na Simba badala ya kupanuka kufikiria CHAN, AFCON, nafasi za kombe la dunia na kutengeneza wachezaji wengi wa kulipwa Ulaya.

Rais wa TFF Jamal Malinzi, tafadhali uwe mtu wa mipango mizuri iliyoandikwa ya kuendeleza soka yetu. Tafadhali sana nenda hivyo ukiwa na ukali fulani wa kuhimiza utekelezaji sahihi ndani ya muda uliopangwa wa mipango mbalimbali ndani ya Mpango wa TFF wa Maendeleo ya Soka Tanzania.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

MWANASOKA BORA WA AFRIKA

Arsenal bado wamsaka Benzema