in , , ,

HUENDA BALE ANAONYESHA THAMANI YAKE

 

Septemba 2013 Real Madrid walikamilisha uhamisho wa Gareth Bale kutoka Tottenham kwa dau la paundi milioni 85. Dau hili linasimama kama dau ghali zaidi la uhamisho kwenye historia ya mpira wa miguu.

Wadau wengi wa soka wakiwemo makocha na wachezaji maarufu walikuwa na mawazo kuwa Bale hakuwa na thamani ya kuuzwa kwa pesa ile. Mchezaji wa zamani wa Real Madrid Raul Gonzalez aliwahi kusema kuwa paundi milioni 85 ni pesa nyingi mno kuzitoa kwa ajili ya Gareth Bale.

Mawazo ya Raul yanafanana na mawazo ya wadau wengi wa mpira wa miguu ulimwenguni. Sidhani kama kuna yeyote anayekubali kuamini kuwa Bale alikuwa na thamani ya kuvunja rekodi ya uhamisho iliyowekwa na Cristiano Ronaldo mwaka 2009.

Nafikiri kusajiliwa kwa pesa ile kulimpa shinikizo Gareth Bale la kutaka kuonyesha kuwa kweli alistahili kununuliwa kwa dau kubwa kiasi kile. Kwenye msimu wake wa kwanza akiwa na Real Madrid Gareth Bale alifanikiwa kufunga mabao 15 na kutengeneza mengine 12 kwenye Ligi Kuu ya Hispania.

Akatoa mchango mkubwa Real Madrid walipotwaa Kombe la Mfalme la Hispania na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2014. Kwenye kila fainali ya michuano hiyo miwili Bale aliifungia Real Madrid bao muhimu.

Baadae Gareth Bale alikuwa shujaa wa Real Madrid alipotoa mchango mkubwa timu hiyo ikitwaa taji la Klabu Bingwa Dunia la FIFA Disemba 2014. Bale aliifungia Real Madrid bao kwenye michezo yote miwili aliyocheza ukiwemo mchezo wa fainali.

Hayo yote hayakutosha kudhihirisha kuwa Gareth Bale alikuwa na thamani ya kununuliwa kwa dau lile ambalo Real Madrid walilitoa kumnunua. Pengine ni kwa sababu kulikuwa na wachezaji wengine waliokuwa na mchango mkubwa Real Madrid ikifikia mafanikio yale.

Cristiano Ronaldo, Angel Di Maria na Sergio Ramos walikuwa na mchango mkubwa zaidi ya Gareth Bale kwenye mafanikio ya Real Madrid msimu ule. Hivyo bado Gareth Bale hakuwa ameonyesha thamani yake.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Wales anakaribia kuipeleka Wales kwenye  michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (Uefa Euro) 2016. Wales inaongoza Kundi B ikiwa na alama 18 mbele ya Ubelgiji wenye alama 17. Kila timu imebakiza michezo miwili kwenye kundi hili.

Wales wanahitaji sare moja tu kutoka kwenye mechi mbili zilizobakia ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano mikubwa ya kimataifa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958 waliposhiriki Kombe la Dunia.

Mchango wa Gareth Bale kwenye timu ya taifa ya Wales kwenye michezo ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Ulaya ni mkubwa mno. Ameifungia timu hiyo mabao 6 kwenye michezo 8 mbaka sasa kwenye mechi hizo za kufuzu.

Tarehe 1o Oktoba mwaka huu Wales watakipiga dhidi ya Bosnia. Kwenye mchezo huo Bale anahitaji kuiongoza Wales kupata sare tu itakayowawezesha kufuzu moja kwa moja kwenye hatua za makundi za Michuano ya Uefa Euro 2016.

Gareth Bale atakuwa shujaa kwa kuiwezesha Wales kucheza michuano mikubwa. Wachezaji wakubwa kama George Best na Ryan Giggs walishindwa kuziwezesha timu zao za taifa kushiriki michuano mikubwa.

Kama anahitaji kushinda ‘Balon d’or’ mara nyingi zaidi ya Ronaldo au Messi ili aonyeshe thamani aliyo nayo basi ni wazi kuwa Bale hataweza kuonyesha thamani yake. Lakini kama kuipeleka Wales kwenye fainali za Uefa Euro kunatosha basi huenda Gareth Bale ameshaonyesha thamani yake.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ujerumani na hongo Kombe la Dunia

Tanzania Sports

Kuna wachezaji 176 kutoka England, kati ya wachezaji 528 wa EPL