in , ,

HILI LA PAMBA NA TIMU ZA MWANZA, WASUKUMA MNACHEZA NGOMA GANI?

George Masatu, Fumo Felcian, David Mwakalebela, Khalfan Ngassa,
Madata Lupigisa hawa ni baadhi ya wachezaji nyota ambao waliwahi
kutikisa nyasi za viwanja vya soka la Afrika wakiwa na Pamba ya Mwanza
“Tp Lindanda”.

Haikutosha kwao kuwa na wachezaji bora pekee, bali waliimarisha na
uongozi wa timu yao.

Uongozi wa Pamba ulikuwa ukiwazidi maarifa ya uendeshaji wa klabu
vilabu vyote ikiwemo Simba na Yanga.

Kuna mambo mengi ambayo viongozi wa Pamba waliyafanya ambayo viongozi
wa Simba na Yanga hawakuyafanya na hawajawahi kufanya mpaka leo.

Leo hii Simba ina mechi Songea Jumatano, inaondoka Dar jumapili kwa
basi, hiki hakikuwepo kwa upande wa Ndanda kipindi kile.

Ilikuwa ni jambo la kawaida timu kuondoka Mwanza saa saba mchana huku
wakiwa na mechi saa kumi jioni.

Hii yote ni kwa sababu uongozi wa Pamba uliingia mkataba maalumu na
mgodi wa Mwadui ,mkataba ambao ulikuwa unahusiana na kutumia ndege ya
wamiliki wa mgodi huo uliokuwa chini ya Fred Williamson.

Hiki kitu hakijawahi kufanywa na hakifanywi na viongozi wa vilabu
vyote vya hapa kwetu, ila Pamba walifanikiwa kukifanya kwenye miaka
ya 90 na wakati tuliopo ni mwaka 2017.

Miaka ya 90 ilikuwa ngumu kwa mchezaji wa Pamba kulia njaa, ila mwaka
2017 ni jambo la kawaida kulia njaa.

Unaikumbuka safari ya Pamba waliyoenda Tanga kuishusha Coastal Union
daraja?, Safari ile ilikuwa na huduma bora kwa wachezaji tofauti na
safari iliyofanywa na timu ya pamba wiki iliyopita kwenda kucheza na
Coastal Union kwenye ligi daraja la kwanza msimu huu.

Nyakati za safari hizi zinatofautiana kabisa kwenye kila kitu, safari
ya kwanza ilifanyika mwaka 1992 kwa kutumia ndege na timu kufikia
kwenye hotel kubwa huku wakipewa huduma bora ya malazi na chakula
bora.

Safari ya pili ilifanyika mwaka 2017 kwa kutumia basi na timu kufikia
kwenye gest house huku ikikosa chakula siku moja kabla ya mechi.

Ni jambo la kusikitisha sana, viongozi wa Pamba na vilabu vingine
vimekuwa vikikosa ubunifu wa kuendesha vilabu vyao na kutegemea mapato
ya mlangoni ambayo huwa siyo ya kiwango kikubwa.

Pamba ilifanikiwa kupata ndege ya kusafirishia wachezaji wake kipindi
kile ambacho hakukuwa na mashirika mengi ya ndege ukilinganisha na
kipindi hiki ambacho kuna mashirika mengi ya ndege, ambayo yapo
yanasubiri barua za viongozi wa vilabu wabunifu wafanye nao biashara
kwa pamoja.

Toto Afrika iko kwenye mazingira ya kushuka daraja, Pamba iko kwenye
hatihati ya kushuka daraja pia, Mbao nayo inajikongoja kubaki ligi
kuu. Na ukitizama kwa umakini matatizo yao ni ya aina moja.

Na kubwa kuliko yote ni njaa, inasikitisha sana timu kulia njaa
kipindi hiki ambacho wafanyabiashara wengi wamekosa Sehemu salama ya
kutangazia bidhaa zao.

Migogoro isiyokuwa na faida ndani ya vilabu imezidi kuua vilabu hivi
na kuwa na mwenendo mbaya kwenye ligi.

Utailamu kwa lipi MZFA kama ukishuka daraja kwa sababu ya migogoro
yenu ya kitoto, ukosefu wa ubunifu katika uendeshaji wa vilabu? Na
kutegemea mapato ya kwenye mechi ambazo mashabiki wanaoingia hawafiki
hata elfu moja?

Migogoro hii mnayoikuza ndani ya vilabu vyenu na nje ya vilabu vyenu
ndiyo inayowafanya mpaka mashabiki wapunguze hamasa ya kuja uwanjani.

Na kibaya zaidi mnawagawa mashabiki wa Ilemela na Nyamagana,
mkiwaambia watu wa Nyamagana hawatakiwi kuishangilia timu ya Ilemela
hata kama ikicheza na timu ya nje ya mkoa.

Uko wapi umoja na ushikamo wenu wasukuma wa Mwanza? Kwanini mnaizomea
Toto Afrika inapocheza na Ruvu Shooting? Furaha yenu ni kuziona timu
zenu zikishuka daraja baada ya hapo muanze kulia kuwa hamna timu
inayocheza ligi kuu?

Hapa ndipo mnaponichanganya wasukuma wa Mwanza na kushindwa kuelewa
kuwa mnacheza ngoma gani? Maana mlio wa ngoma unaopigwa ni mmoja
lakini aina ya uchezaji wa ngoma hiyo ni tofauti.

Hebu kuweni ni umoja wasukuma, shikamaneni kuzibakisha timu zenu
kwenye ligi kuu na ligi daraja la kwanza huku mkipigana Alliance
ipande daraja.

Viongozi kuweni wabunifu, kama miaka ya 90 viongozi wa Pamba
walifanikiwa kupata ndege ya kuwasafirisha inashindikana nini kipindi
hiki ambacho kuna mashirika mengi ya ndege ambayo yanahitaji
kujipambanua zaidi ili kuendana na ushindani wa kibiashara?

Martin Kiyumbi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILCHOKIONA KWENYE BAADHI ZA MECHI ZA EPL ‘WEEKEND’ HII

Tanzania Sports

Chelsea wabanwa, Leicester hoi