in , ,

HILI LA MAANDAMANO YA SIMBA WANAFANYA KWENYE TAA NYEKUNDU

Mpira kwetu umekuwa ukihusisha vitu vingi sana kwa siku za hivi
karibuni, Mpira umechukua nafasi ya sanaa, na matawi yote yaliyokuwa
yanapatikana kwenye sanaa siku hizi yanapatikana kwenye mpira.

Siyo jambo la kushangaza kila ukiamka utakutana na filamu ya maigizo
kwenye mpira tena ikifanywa na watu ambao nafsi zetu ziliwaamini kwa
kiasi kikubwa na kuwapa dhamana ya wao kutuongoza katika maendeleo ya
mpira wetu kwa kuwakabidhi funguo za maendeleo.

Imefikia hatua hata kama una msongo wa mawazo unapungunzwa na
vichekesho vilivyomo kwenye mpira wetu. Tumekuwa wajuzi wazuri sana
katika suala la ufinyanzi ndiyo maana tunachukua udongo na kufinyanga
mpira wetu na kuuweka katika taswira mbalimbali za vinyago ili tu
tunufaishe nafsi zetu kwa kuvitazamana vinyago vilivyotokana na udongo
wa mpira wetu.

Hakuna jema tunalolishona kwenye tambala letu bovu la mpira badala
yake tumeamua kuliweka tambala letu la soka kwenye gunia kisha
tukaamua kushona gunia na kulitumbukiza kwenye maji. Hatuna huruma
kabisa na tambala la soka letu tuliloliweka kwenye gunia ambalo
tumelitupa kwenye maji.

Kuna faida ya kutunza chochote kile ambacho tunacho hata kama ni
kichakafu kina thamani kubwa sana, sema siku zote huwa tunaangalia leo
zaidi kuliko kesho ndiyo maana ni ngumu kuona thamani ya kichakafu leo
hii na kusahau leo hii waweza kukitengeneza kichakafu ili kesho kiwe
na thamani kubwa zaidi.

Inahitaji busara ndogo sana kutofautisha kiganja na unyayo, ndiyo
maana mwenye hekima na busara huwezi muona akitumia unyayo kula
chakula na kiganja kutembelea ,lakini maswali mengi huja kichwani pale
unapomuona mtu akilazimisha matumizi ya unyayo wa mguu yahamie kwenye
kiganja cha mkono, na matumizi ya kiganja ya mkono kuhamia kwenye
unyayo wa mguu.

Hapo ndipo tafasri halisi ya mtu kutokujua anachokitafuta huja. Kuna
wakati nyama inaweza ni hitaji zuri na la starehe la mwanadamu lakini
tatizo huja njia ambazo mtu anaamua kutumia ili apate nyama .

Kuna busara kubwa ambayo inahitajika kutumika pale unapoamua kutafuta
njia sahihi ya kutafuta nyama kwa ajili ya kustarehesha nafsi yako.

Kuna vitu vingi sana unaweza ukavipoteza bila kujua kama ukiamua
kuchagua njia ambayo siyo sahihi. Kitu kinachomfanya mtu afanikiwe
kwenye kitu chochote ni pale anapoamua kuchagua njia sahihi ya
kupitia, usahihi huja na matokeo chanya na yenye manufaa makubwa
kwenye jamii yoyote ile.

Simba muda huu inapigana kwa nguvu zote ichukue ubingwa, nguvu zote
zimehamishiwa kwenye ubingwa kitu ambacho ni sahihi kabisa maana ni
muda mrefu timu haijashiriki kwenye michuano ya kimataifa na hii
inaonekana ni nafasi kubwa kwao kupigania tena wawe mabingwa ili
wapate nafasi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani.

Ni wakati muhimu na ugumu sana kwa Simba na timu yoyote ambayo
inahitaji ubingwa . Kuhitaji ubingwa kunahitajika vitu vingi sana
kwenye timu. Moja ya kitu muhimu ambacho kina umuhimu sana kwenye
hitaji la timu iliyo katika mbio za ubingwa ni utulivu.

Utulivu kwenye timu huja na mambo mengi sana na kikubwa ni mshikamano
wa pande tatu kwenye timu , yani mashabiki, viongozi na wachezaji
pamoja na benchi nzima la ufundi.

Mshikamano huzaa nguvu ya upiganaji kwa wachezaji na hamasa kubwa kwa
benchi la ufundi ili kwa kutuliza akili zao waweze kufanikiwa kubeba
ubingwa.

Ndicho kitu ambacho Simba walikihitaji kipindi hiki kuliko hata pointi
tatu wanazozidai kwa Kagera Sugar.

La point za Kagera Sugar hii vita sitaki kuitazamana hata kidogo ila
wenzangu watanisimulia matokeo yake ila hili la kuandamana limenishtua
sana.

Hili linaweza ƙlikaonekana kama jambo dogo kwa timu lakini lina
madhara hasi mengi sana. Kuna hatari kubwa kwa wachezaji wa timu ya
Simba kupoteza utulivu katika mechi hizi tatu walizobakiza kwenye
mikono yao ili waweze kuwa mabingwa.

Focus ya timu imeshaanza taratibu kupotea, na timu sasa hivi inapigana
zaidi nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja.

Vita ya nje ya uwanja ni ngumu kuleta ushindi wa ndani ya uwanja ,
kikubwa utakachokipata nje ya uwanja ni njia ya kukuelekeza kupata
matokeo hasi ndani ya uwanja kwa sababu wachezaji , mashabiki, na
viongozi watahamisha nguvu, akili zao zote nje ya uwanja kwa kiasi
kikubwa na kusahau kuwa matokeo hupatikana ndani ya uwanja.

Wakati huu haukuwa wakati wa kuwachanganya wachezaji na mambo ya nje
ya uwanja , haya maandamano yanaweza kuwatoa wachezaji mchezoni na
kujikuta wapo nje ya kugombea ubingwa. Mimi nahisi wazo la wao
kuandamana waliwaza kwenye mstari mwekundu wangesubiri taa ya kijani
iwaruhusu ndiyo waandamane kwa usalama wao.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE MECHI ZA UEFA

Tanzania Sports

SERENGETI BOYS INAZIDI KUTUPA SABABU YA KUICHANGIA