in , , ,

Hii ni BARCA ndani ya miaka 10 iliyopita

Wakati naangalia mechi ya juzi kati ya Manchester United na Barcelona kitu pekee ambacho kilikuwa kinakuja kwenye kichwa changu ni fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya kati ya Barcelona na Arsenal.

Fainali ya moto, fainali ambayo iliwakutanisha watu ambao walikuwa wa moto. Watu ambao walikuwa na wauaji kila upande.

Arsenal ilikuwa na majemedari haswaa!. Ndicho kipindi ambacho Arsenal ilikuwa na Thierry Henry. Nyota ambaye aliacha alama kwenye mioyo ya mashabiki wa Arsenal.

Ndiyo Arsenal ambayo ilikuwa na Robert Pires na ndiyo Arsenal ambayo ilikuwa ya mwisho mwisho kupata mafanikio makubwa barani Ulaya.

Tangu hapo hawakupata nafasi ya kufanya vizuri tena kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya kama ambavyo walifanya kipindi kile.

Inawezekana kabisa kadi nyekundu ya Jens Lehman iliwafanya watoke kwenye mchezo siku ile. Iliwezekana kabisa kadi ile ilipunguza nguvu ndani ya kikosi cha Arsenal.

Kwa sababu tu, ilimbidi Robert Pires atoke ili kipa mpya aingie kwa ajili ya kuziba pengo la Jens Lehman ambaye alikuwa ametolewa kwa kadi nyekundu.

Yani ndani ya dakika moja tu Arsenal ikawa imewakosa wachezaji wawili muhimu ndani ya kikosi chake. Robert Pires na Jens Lehman.

Hili lilikuwa pigo kubwa sana kwa Arsene Wenger na hii inaweza ikawa sababu moja wapo ya Arsenal ƙkupoteza ile mechi.

Lakini kuna sababu moja kubwa ambayo huwezi kuikwepa kabisa. Uimara wa kikosi cha Barcelona. Hapana shaka kwa kipindi hicho Barcelona ilikuwa imara sana.

Na hii ni moja ya sababu ambayo ilisababisha Barcelona washinde ile mechi. Hapa siongelei uwepo wa Ronaldinho ndani ya kikosi.

Ingawa huwezi kukwepa kabisa kuutambua uwezo binafsi wa Ronaldinho katika kuamua mechi ndani ya uwanja.

Lakini ninachojaribu kuongelea ni uwezo wa kitimu kiujumla wa Barcelona. Barcelona ilikuwa ni timu bora kiujumla kwa kipindi hicho.

Ndiyo maana nikasema fainali hii ilizikutanisha timu ambazo zilikuwa za moto kwa kipindi hicho (Arsenal na Barcelona)

Baada ya fainali hii timu zote mbili zilichagua njia mbili tofauti za kupita. Njia ambazo ziliwatofautisha sana kimafanikio.

Arsenal walichagua kurudi nyuma. Hawakutaka tena kabisa kutembea kwa kwenda mbele. Ila Barcelona walichagua kutembea kwa kwenda mbele.

Ndipo hapo walipomchukua Pep Guardiola kuwa kocha wao mkuu. Mabadiliko ambayo yalijenga jeshi ambalo lilikuwa na uwezo mkubwa wa kushinda kila vita.

Ndipo hapo tuliposhuhudia Barcelona ambayo ilikuwa imekamirika idara nyingi. Sehemu ya kiungo kulikuwepo na utatu mtakatifu.

Utatu uliokuwa umebeba majina ya Sergio, Iniesta na Xavi. Utatu ambao ulikuwa na uwezo wa kupiga pasi mpaka 300 kutoka miguuni mwao tu.

Utatu ambao ulikuwa unaitengeneza timu. Utatu ambao uliifanya Barcelona ionekane kama playstation.

Nani ambaye alikuwa anaichukia kuitazama Barcelona kipindi hicho? Barcelona ambayo kila muda ilikuwa inatamani kuwa na mpira mguuni.

Ilikuwa ngumu kushindana na Barcelona katika umiliki wa mpira, walihakikisha wanamiliki mpira huku wakiupaka rangi kuhakikisha unakupendezesha machoni mwako.

Barcelona hii haipo tena. Haina uwezo tena wa kuhakikisha inacheza mpira unaovutia kama kipindi cha nyuma. Barcelona ya sasa imekuwa tofauti sana.

Haivutii kutazamika kama kipindi cha nyuma. Barcelona ambayo kwa muda mrefu inamtegemea Lionel Messi , yeye ndiye kila kitu kwa sasa tofauti na kipindi cha nyuma.

Yeye akikosekana timu inayumba. Imeshindwa kujitoa kwenye kivuli cha kumtegemea Lionel Messi kwa sasa. Imeshindwa kurudi kwenye nyakati zake.

Nyakati ambazo kila timu ilikuwa inaogopa kukutana nayo. Kwa sasa ukimtoa Lionel Messi kwenye kikosi cha Barcelona, inaonekana timu ya kawaida. Barcelona inaonekana hatari kwa sababu tu ina lionel Messi kikosini.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Karibu kwenye ulimwengu wa KINDOKI

Tanzania Sports

Ligi ya Mabingwa Ulaya: