in

Fahamu mambo yanayomkabili Pochettino PSG

Mauricio Pochettino

Mwaka mpya umeanza na mambo mapya kwa mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu nchini Ufaransa, PSG. Baada ya kumfukuza kazi kocha Thomas Tuchel sasa wamemwajiri Mauricio Pochettino. Je ni mambo gani yanayomkabili kocha huyo kuelekea kipindi chake cha miezi 18 jijini Paris?

Katika makala haya nabainisha mambo kadhaa ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa kipindi ambacho atamudu kwenye ukocha klabuni hapo.

MIEZI 18 NA TAJI LA UEFA

Mauricio Pochettino ni kocha mkubwa lakini alikaa nje ya uwanja kwa miezi 13 bila kufanya kazi ya ukocha. Amefundisha kwa mafanikio katika klabu ya Tottenham Hotspurs ambayo alifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako aliambulia kichapo cha bao 1-0 kutoka Liverpool.

PSG wamempa kazi Pochettino kwa kipindi cha miezi 18, sawa na mwaka mmoja na miezi sita. Ni kipindi kifupi ambacho kocha huyo anatakiwa kuleta mabadiliko. Ni kama vile Pochettino amepewa kazi hiyo kwa majaribio. Ni kama vile anamshikia mtu hiyo nafasi.

Hata hivyo mwaka mpya ndiyo umeanza na PSG wanaingia katika utawala wa kocha mpya. Nimeona PSG na Pochettino wakizungumzia suala la mpango mpya wa mafanikio, nimejiuliza hii inayoitwa ‘project’ kwa miezi 18 itafanyikaje?

Ni wazi akimaliza msimu bila kombe kibarua chake kipo hatarini. Ni wazi akitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa atajiweka hatarini kutimuliwa. Miezi 18 ya majaribio kwa kocha mkubwa kama huyu hakika inachekesha. Ni kibarua kigumu kweli kweli ikizingatiwa sharti lililopo katika mkataba wake ni kutwaa taji la UEFA.

HAWANA KIONGOZI DIMBANI

Ukweli ni kwamba Kimpembe hawezi kuwa beki hodari bila kusimamiwa. Kazi ya kuwasimamia mabeki wengine haiwezi kufanywa na kila mmoja ,lakini Thiago Silva alijaliwa kipawa cha kuwaongoza PSG uwanjani.

Kwenye safu ya ulinzi unahitaji beki ambaye anawaongoza wenzake, mwenye nguvu na sauti klabuni. Real Madrid wanaye Sergio Ramos. Liverpool wanaye Virjil van Diyk. Barcelona wanaye Lionel Messi. Sasa ukitazama PSG tangu kuondoka Thiago Silva huoni kabisa mchezaji anayewaongoza.

Nahodha mpya Marquinhos hajaweza kuvaa viatu vya Thiago Silva na anaonekana hana sauti kwa wachezaji ndani na nje ya uwanja. Tangu kuondoka Thiago Silva kwenda Chelsea safu ya ulinzi imepwaya na kuruhusu mabao mengi.

Msimu uliopita iliruhusu mabao manne katika mechi za makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Licha ya kuwa na mastaa wengi PSG hawana kiongozi dimbani.

HAWANA MFUMANIA NYAVU ASILIA

Kylian Mbappe na Neymar
Kylian Mbappe na Neymar

Tatizo jingine la PSG ni kukosa namba 9 asilimia. Safu ya ushambuliaji inawategemea Neymar Junior na Kylian Mbappe lakini hawa sio washambuliaji kwa asili, wao ni mawinga au viungo washambuliaji na washambuliaji namba mbili(namba 10).

Mara nyingi nimeshangazwa na wale wanaoamini Kylian Mbappe anaweza kucheza namba 9, naona kama utani kazini. Mbappe ni mchezaji mzuri lakini hawezi kuwa namba 9 mzuri kumzidi Edinson Cavani au Kari Benzema wala  Javier Chicharito.

PSG wanahitaji kuwa na nambari 9 asilia ambaye atanufaika na kazi inayofanywa na wawili hao, Neymar na Mbappe. Thomas Tuchel amewahi kukiri kuwa kumruhusu Cvani aondoke lilikuwa kosa kwa klabu hiyo.

Cavani ndiye aliyepachika mabao mengi kwa timu hiyo, lakini kutosajili nambari 9 kwa kigezo cha kuwategemea Mbappe na Neymar ni mzaha ambao unafanywa na klabu yenyewe akiwemo mkurugenzi wa michezo Leonardo kabla ya kusingizia udhaifu wa makocha.

Cavani aliruhusiwa kujiunga Manchester United, huku PSG wakibadili usajili wa mkopo kuwa wa kudumu kwa Mauro Icardi. Hata hivyo Mauro Icardi amekuwa majeruhi wa muda mrefu hivyo kushindwa kutoa mchango kwa timu hiyo. Ni Icardi pekee ndiye nambari 9 asilia, lakini hayupo uwanjani.

KUKUBALIKA NA WACHEZAJI

Tanzania Sports
Thomas Tuchel, inasemekana hana ushawishi miongoni mwa wachezaji

Kocha yeyote ili afanikiwe ni lazima akubalike na wachezaji. Ushawishi, uwezo, sifa za ushindi akiwa kocha na mchezaji na ubora wake katika ufundi vinaweza kumpa mafanikio kocha yeyote. Zinedine Zidane alikuwa mchezaji mkubwa sana wa dunia. Katika ukocha alikubalika licha ya kutoka Castilla.

Ole Gunnar Solskjaer anakubalika na wachezaji kama ilivyo kwa Jurgen Klopp ni kocha mkubwa ambaye amafanya mambo makubwa Bundesliga akiwa Borussia Dortmund kwahiyo anapokuja kwenye timu yako ni mtu mkubwa kweli kweli.

Mourinho pia anaweza kuwa kocha anayekubalika kila timu lakini naye amewahi kukumbwa na migogoro na wachezaji. Kwa Mauricio Pochetttino ili afanikiwe PSG lazima wachezaji wamkubali. Kukubalika na wachezaji ni silaha ya kwanza ya kupata mafanikio kwani ndiyo wanawajibika kumfanyia kazi anayowatuma.

Thomas Tuchel licha ya kutimuliwa alikubalika na wachezaji. Ndiyo maana baada ya kufukzuwa wengi wao waliandika katika mitandao ya kijamii kueleza thamani ya kile alichokifanya klabuni hapo. Je Pochettino atakubalika PSG? Ni suala la kusubiri na kuona.

MIPANGO YA USAJILI JANUARI

Tanzania Sports
Lille’s Burak Yilmaz, Houssem Aouar wa Olympique Lyon pamoja na Kylian Mbappe

Pochettino amejiunga PSG katika kipindi ambacho dirisha dogo la usajili linaendelea. Kama nilivyoeleza hapo awali kuwa safu ya ushambuliaji ina kasoro kama ilivyo kwa safu ya ulinzi.

Bila shaka mwezi Januari huu utampa nafasi ya kuketi mezani na mkurugenzi wake Leoanrdo kuangalia namna ya kuimarisha kikosi chao.

Kocha wa zamani Thomas Tuchel aligombana na Leonardo kuhusu suala la kuimarisha kikosi chao lakini hapakuwa na usajili wa maana. Kama Pochettino anataka kufanikiwa Ligi ya Mabingwa ni lazima awe na wachezaji wenye viwango vya juu.

Safu ya kiungo inamtegemea Marco Verrati peke yake, lakini wanaomfuatia hawana viwango kama yeye. Hii ina maana PSG licha ya uwekezaji wao mkubwa bado hawana wachezaji wa viwango vya juu.

KUPUNGUZA MZIGO KWA NEYMAR

Tanzania Sports
Mbappe

PSG wamekuwa wakimtegemea Neymar Junior kuwaletea mafanikio. Lakini wamesahau katika klabu yao wanahitajika kuwa na wachezaji wenye ubora angalau nusu ya uwezo wa Neymar. Kinyume cha hilo hawatakuwa na mafanikio makubwa.

Ukiwaondoa Mbappe na Neymar utaona PSG inakuwa timu ya kawaida kabisa ambayo inapokutana na mpinzani imara huwa inababaika na kugeuzwa gunia la mazoezi.

Lazima Pochettino atazame namna bora ya kuwezesha timu kucheza pasipo kumtegemea Neymar. Lazima PSG wapungumzie mzigo kwa Neymar, lakini hilo litawezekana kama watasajili wachezaji wenye viwango vya juu kukaribia vha Mbrazil huyo.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
The FA

BREXIT: Soka na maisha mapya

La Liga

La Liga bila nyota wakubwa hali itakuwaje, serikali itakwepa lawama?