in

Eden Hazard amekumbwa na janga gani Real Madrid?

Eden Hazard

Kwenye mchezo wa soka hakuna mchezaji ambaye hana ndoto za kuchezea Real  Madrid. Inawezekana mchezaji asijiunge nayo ama akachezea timu fulani hadi  mwisho wa maisha yake, lakini linapofika suala la kusajiliwa na Real Madrid  wengi wao hujutia baada ya kustaafu.  

Tumeyaona hayo kwa Andre Pirlo aliyestaafia Juventus, Francesco Totti aliyestaafia AS Roma na wengine ambao hawakupata nafasi ya kuchezea miamba  hiyo ya Hispania.  

Eden Hazard ni nyota ambaye amebahatika kujiunga na timu ya ndoto yake.  Kuhama kutoka Lille ya Ufaransa kwenda Chelsea ya England ilikuwa hatua ya  kukua kisoka wakati ambao Real Madrid haikuonesha nia ya kumsajili. Lakini sasa  Hazard ni mchezaji wa Real Madrid akiwa amejiunga msimu uliopita.  

Msimu wake wa kwanza 2019/2020 amefanikiwa kutwaa taji la La Liga chini ya  kocha ambaye anamhusudu tangu akiwa mchezaji Zinedine Zidane. Real Madrid  walilipa dau la pauni milioni 143 ili kupata huduma ya Eden Hazard.  

Jambo kubwa zaidi linaloeleweka ni kwamba Real Madrid ilikuwa na matarajio  makubwa kutoka kwa nyota huyo wa zamani wa Chelsea, ambaye alipata fursa ya  kucheza chini ya kocha anayempenda zaidi.  

Hata hivyo Hazard hadi leo hajafanikiwa kuonesha kile kiwango kilichosababisha  pesa nyingi zitolewe katika usajili wake. Sasa ana miaka 29, amefunga mabao  matatu katika mechi 29.  

Tanzania Sports
Eden Hazard 

Kasi yake ya mchezo imekumbwa na majeraha ya mara kwa mara. Anaweza  kucheza mechi tatu mfululizo kisha zinazofuata akawa hospitalini kupatiwa  matibabu. Tatizo hili limekuwa kubwa sasa, Hazard haonekani kuwa na mchango  mkubwa kama ule wa Lucas Vazquez wala thamani yake aliyonunuliwa. 

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan, ilionekana kama  Hazard angeweza kuinuka zaidi na kucheza kwa kiwango cha juu. Alianza mchezo  taratibu na alionesha namna anavyoweza kutoa mchango.  

Kifundi na uzoefu Hazard ni mzuri kuliko Vinicius Junior,Rodrygo Goes,Martin  Odegaard, Lucas Vazquez, Mariano Diaz na hata Luka Jovic. Ufundi wake wa  kusoma mchezo, uwezo wa kutengeneza mabao, kuifungua safu ya ulinzi ya timu  pinzani pamoja na kucheza kitimu ni mambo yanayompa sifa Hazard.  

Timu inapokosa maarifa ya kuipasua safu ya ulinzi ya timu pinzani, mara nyingi  Hazard ndiye amekuwa akitumika kufanya kazi hiyo. Yeye hutengeneza mianya ya  kufunga na kuipa ushindi timu yake.  

Hizo ndizo sifa alizokuwa nazo Lille hata kumvutia Zidane ambaye kwa miaka  mingi alibainisha umuhimu wa kusajiliwa nyota huyo alipokuwa kinda. Hata hivyo  Hazard akasajiliwa na Chelsea na akaonesha ubora wake kwa kipindi kirefu.  

Uwezo alionao ndio chachu ya kusajiliwa Real Madrid. Na kwahiyo matarajio  yaliyokuwepo ilikuwa lazima yatokee. Madrid kama klabu ilitambua kuwa mauzo  ya jezi yangekuwa makubwa. Ilitambua mchango wake kiufundi utaongeza  maarifa ndani ya kikosi cha Real Madrid. Vilevile ungesaidia kunyambulisha  maagizo ya kiufundi ya kocha Zidane. 

Lakini Hazard ni nyota ambaye amekuwa akisua sua msimu wa pili sasa.  Alinunuliwa akiwa na miaka 28, mzoefu wa kutosha na ambaye amejijengea  heshima inayompa nafasi ya kutamba kikosi chochote. Lakini mambo yamekuwa  magumu kwake. Real Madrid haijapata mchango wake. Madrid wameishia  kumtibu majeraha mengi huku kukiwa na maswali juu ya mustakabali wake.  

Inatarajiwa Hazard awe mchezaji wa kutumainiwa kuliko chipukizi niliowataja  hapo juu. Inatarajiwa Hazard awe kiongozi wa pili baada ya Karim Benzema  katika safu ya ushambuliaji. Lakini kwa sasa inawategemea chipukizi ambao hawawezi kubeba mizigo mizito ya ushindi wa timu hiyo. 

Martin Odegaard anazidi kuimarika akiwa na miaka 21. Vinicius na Rodrgyo bado  ni vijana walio chini ya miaka 20 ambao wanategemewa kwa miaka mitano ijayo.  Marco Asensio bado hajarudi katika kiwango chake, lakini naye ni miongoni mwa  wachezaji waandamizi wanaohitajika kubeba majukumu ya timu. 

Pembeni ya Hazard jina linalokaribia ni Asensio na Lucas Vazquez. Ni Vazquez  pekee amekuwa akitumika nafasi tofauti na kutoa mchango mkubwa kuliko  wengine waliotajwa hapo juu. Nafasi ya winga ambayo Hazard hucheza akiumia  inabaki kwa chipukizi. Isco naye hajawa katika kiwango bora na ndio maana  amebaki kucheza benchi tu. 

Huyu Hazard wa sasa anayecheza mechi 29 na kupachika mabao matatu  anasikitisha mno. Haonekani kuwa timamu kimwili kwa sababu amekuwa akiumia  mara kwa mara.  

Je, inawezekana tatizo ni matibabu hafifu? Tatizo ni benchi la ufindi kwenye  kitengo cha viungo? Je, ni kitu gani kinachokumba nyota huyo ambaye alitarajiwa  kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia? 

Kwa hakika jambo hilo litakuwa linamuumiza kichwa Zidane kwa vile amekuwa  akiamini Hazard ni mmoja wa nyota waliotakiwa kutikisa dunia mapema na  alitakiwa kuchezea Real Madrid. Klabu imemsajili akiwa na miaka 28, huwezi  kusema ni umri mkubwa kusajili na kwamba labda amefika kilele cha mafanikio. 

Zidane mwenyewe alisajiliwa akiwa na miaka 29 akitokea Juventus Turin ya Italia,  lakini alifanya mambo makubwa klabu hapo.  

Tanzania Sports
Zinedine Zidane

Mashabiki wa Real Madrid hawaambiliki kuhusu Zidane. Hawajali kuwa  alisajiliwa akiwa na miaka 29 yaani kuelekea mwishoni mwa uwezo wake lakini  kazi aliyoifanya kwa kipindi chote alichocheza Real Madrid inamfanya awe na  heshima kubwa.  

Kwa wakati huu itakuwa ni kujidanganya Hazard kupewa heshima na mashabiki  wa Real Madrid huku wakitambua mchango wake mdogo. Vilevile ni vigumu  kutegemea kuwa labda ataweza kurejesha kiwango Real Madrid kama kile  alichokionesha akiwa Chelsea.  

Majeraha ya mara kwa mara yanarudisha nyuma uwezo wa mchezaji. Tumeona  mastaa kadhaa wakishindwa kuendelea na kandanda tangu walipopata majeraha.  Real Madrid ilishuhudia kiwango bora cha chipukizi wake Jesse Rodriguez lakini  tangu alipoumizwa mguu hakuwahi kurejesha kiwnago chake cha awali. 

Ni kama majeraha hayo yalizika kabisa uwezo wake. Jesse alijiunga na miamba ya  Ufaransa PSG, lakini hakufanya maajabu na mwisho wakamtoa kwa mkopo kabla  ya kumuuza kabisa.  

Hazard anafikirisha mno kila anapokuwa uwanjani. Uchezaji wake umepunguza  kasi yake ingawa muono na maarifa yake yanaonekana kwenda vizuri. Mchezo  pekee ambao ulivutia kumtazama Hazard akicheza ni dhidi ya Inter Milan nchini  Italia. Alijaribu kutuonesha juu ya kile akilichomfanya asajiliwe Real Madrid.  Lakini bila mafanikio hakufikia hata robo ya uwezo alioonesha Chelesa. Sijui ni  nini kilichotokea kwake.  

Muda utaongea.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Neymar

KOMBE LA DUNIA 2022

Hekaheka za EPL mwishoni mwa wiki

Taratibu shangwe zinarejea viwanjani