in

Biashara United imefuzu katikati ya giza nene

KLABU ya Biashara United ya mkoani Mara imefanikiwa kusonga mbele kupeperusha vema bendera ya nchi yetu katika mashindano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitupa nje FC Dikhil ya Djibout kwa jumla ya mabao 3-0. Katika mchezo wa kwanza Biashara United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini lakini mchezo marudiano imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la soka barani Afrika CAF mshindi wa mchezo huo ambaye ni Biashara United anakwenda kupambana na mshindi kati ya Hay Al Wadi ya Sudan na Ahli Tripoli ya Libya.

Hii ni mara ya kwanza Biashara United kushiriki mashindano ya Kimataifa. Pia ni msimu wa pili mfululizo Tanzania inatoa mwakilishi mpya kwenye mashindano ya kimataifa baada ya Namungo kushiriki hatua ya makundi kwenye mashindano ya Shirikisho CAF msimu uliopita.

Mchezo huo ukioneshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam umeibua matatizo lukuki yanayoikabili Biashara United. Kocha Patrick Odhiambo ana kazi kubwa ya kufanya kabla ya kukutana na wapinzani wa raundi nyinginre.

Haya ni mashindano ya kimataifa, lakini kwa namna Biashara United inavyocheza inasikitisha mno; kuanzia nafasi ya golikipa,safu ya ulinzi,viungo,mawinga na washambuliaji pamoja na timu nzima imejaa vipande vingi. Na ikiwa haitajirekebisha kabla ya kukutana na wapinzani wake tutegemee kichapo kikubwa zaidi.

SAFU YA ULINZI

Kuanzia kwa golikipa wa timu hiyo wanakabiliwa na matatizo ya kufanya uamuzi pamoja na kuziba mianya ya hatari kabla haijatokea. Namna wanavyoanzisha mpira,kutoa pasi na kufungua na kuomba kumeonesha ni timu dhaifu. Makosa ya walinzi ni kutoa pasi kwa wapinzani,golikipa anapiga pasi kuwapa wachezaji wa FC Dikhil na kuhatarisha lango lake, ni mambo yanayoshangaza. Hakuna umakini.

SAFU YA KIUNGO

Eneo la kiungo mkabaji limekuwa kiini cha matatizo ya safu ya ulinzi. Eneo hili limepwaya kwa kiasi kikubwa kwa sababu kiungo cha ulinzi anacheza mtu mmoja ambaye hana uwezo wa kuwalinda mabeki. FC Dikhil waliichachafya safu hii kiasi kwamba wangekuwa makini wangeibuka na ushindi au kupachika angalau mabao 3 hadi 4. Ni bahati tu imewaokoa Biashara United sio uwezo wa kimchezo.

Eneo pekee linaloonesha uhai katika safu ya kiungo ni wakati wa kupiga mashuti nje ya 18. Ramadhan Chombo alifunga mabao mawili kutoka nje ya 18, na kudhihirisha majukumu ya kiungo wa ushambuliaji yanavyopaswa kufanyika.

Katika mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kocha Patrick Odhiambo aliwafundisha zaidi kupiga mashuti kutokea eneo la 18.  Mbinu hii ikikutana na viungo wakali wa ukabaji haiwezi kuisaidia lolote Biashara United kwa sababu hakuna umakini wala mpango madhubuti wa kupokezana majukumu ya kutafuta mabao.

SAFU YA USHAMBULIAJI

Hili ni eneo ambalo halina madhara yoyote na mwalimu wa Biashara United anapaswa kukiri ni safu butu isiyo na maarifa,imekosa umakini na haina mpango maalumu wa kutafuta ushindi. Washambuliaji walicheza kama vile wanacheza chandimu kwenye mashindano ya Kimataifa. Hata ari ya kucheza kwa umahiri ili kutangaza vipaji vyao nje ya mipaka ya Tanzania hakukuwepo na dalili hizo. Huu ni udhaifu ambao unapaswa kufanyiwa kazi mapema kabla ya kukutana na timu zenye uwezo mkubwa kisoka.

HAICHEZI KITIMU

Nilikuwa nahesabu pasi zinazopigwa na Biashara United kuelekea lango la adui. Timu nzima ilikuwa na uwezo wa kupiga pasi mfululizo chini ya 11 kwa kipindi cha kwanza. Mara nyingi pasi hizo zilifika 7 hadi 9, na dakika 44 ya kipindi cha kwanza pekee ndipo walifikisha pasi 11.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili angalau walifikisha pasi 15 mfululizo, lakini kila mara hawakuwa na uwezo wa kucheza kitimu, kuonana,kushambulia pamoja,kujilinda na kutafuta mabao kimbinu.

Butu butua zilikuwa nyingi kuliko mkakati wa timu kusaka ushindi. Utulivu ulikuwa hafifu mno, jambo ambalo mwalimu Patrick Odhiambo anatakiwa kuwaambia wachezaji wake hatua ya kwanza ya kumshinda mpinzani ni kushambulia wakati wote ukiwa na mpira na usipokuwa na mpira.

Soka la kisasa linahitaji wachezaji kucheza kwa kimahesabu, mfano timu inapotafuta mpira maana yake inatakiwa kushambulia kuanzia eneo la 18 la adui. Lakini kwa Biashara United hata ile hali ya kutuliza mpira,kuwafanya wapinzani wahahe uwanjani hakuna kabisa. Kifupi ni wawakilishi wetu wabovu, ambao tunalazimika kuwaombea kwa Mungu wasonge mbele kwa kutegemea bahati.

NANI KIONGOZI?

Kikosi cha Biashara United kinakosa mchezaji anayetoa amri uwanjani. Mchezaji mwenye sauti ya kusikika na kuheshimiwa na wachezaji wengine. Yaani mchezaji wa kuelekeza na kuwaamsha nyota wake. Katika nafasi hiyo kwa mbali Ramadhani Chombo anaibuka lakini haonekani kusimama imara katika mabega ya kiongozi wa wachezaji uwnajani.

Kamera za Televisheni zilimuonesha akiwaelekeza wenzake mambo kadhaa lakini suala la utulivu kwa timu hiyo ni tatizo. Kiongozi mchezaji ndani ya uwanja anatakiwa kuwa na sauti inayosikika na kueleweka.

HAKUNA MPANGO MADHUBUTI

Mojawapo ya mambo yaliyoshangaza katika mchezo huo ni namna timu hiyo inavyocheza bila kuwa na mpango madhubuti. Kwa lugha ya kimombo husemwa ‘clear plan’ wakati ambao timu inapanga mashambulizi na kuwasambaratisha wapinzani au namna inavyocheza na kuwadhibiti wapinzani wake. Biashara United chini ya kocha Patrick Odhiambo haikuwa na mpango madhubuti wa mchezo ambao unatambulisha namna wanavyozimaliza timu pinzani.

PATRICK ODHIAMBO ANATOSHA?

Pamoja na heshima anayostahili kuwaongoza Biashara United hadi hatua hii ya pili. Lakini namna timu yake inavyochjeza,makosa yanayofanyika,kukosa mipango na mikakati ya kucheza kitimu ni jambo ambalo linazua maswali juu ya ubora wa mwalimu huyu.

Timu inacheza ikiwa vipande viwili; ile inayojilinda na inayojaribu kushambuliaji lakini haina mipango. Wakati wa kujilinda timu inayumba kuanzia katikati,pembeni na mabeki wa kati na haina mpango. Vilevile uwezo wa kukabia juu (kwenye 18) haupo katika timu hiyo. Uwezo wa kutuliza mpira chini haupo. Ni kama Biashara United inajiendea kwenye mashindano haya. Je kocha huyo ana ufundi wa kutosha kuituliza,kuichezesha kitimu na kuipa mpango na mkakati wa ushindi? Sidhani.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Zinedine Zidane

Sababu 5 tofauti ya Zidane na Ancelotti

SIMBA SPORTS CLUB

Viwanja 10 vibaya vya Ligi Kuu Tanzania