in , , , ,

Balozi Kallaghe apigania wanasoka wa Tanzania


*Aanzisha mikakati waingie Ligi za Uingereza

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe amekutana na wadau kadhaa wa michezo waishio nchini humu, kubadilishana mawazo nini kifanyike katika suala zima la kusaidia maendeleo ya michezo nyumbani.

Katika mazungumzo yake, Balozi Kallaghe alieleza kusikitishwa na kutokuwapo Watanzania wanaocheza kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) inayopendwa na kufuatiliwa zaidi kote duniani au kwingineko Ulaya.

“Nakerwa sana na kutokuwa na Watanzania katika EPL, na hata ligi za chini hapa Uingereza na Ulaya kwa ujumla. Na sio hilo tu, hata michezo mingine hatufanyi vizuri ukilinganisha na wenzetu. “Mnajua kuwa nakutana mara kwa mara na mabalozi wenzangu katika masuala ya kazi zetu, linapokuja suala la mafanikio kimichezo, sina cha kusimulia,” Balozi Kallaghe akawaambia wadau.

IMG_1795
Israel saria, Johnson, Musema

 

Mheshimiwa Balozi Kallaghe ambaye ni mdau mzuri wa michezo tangu zamani, anasema lazima hali hiyo ibadilike, akieleza kuwa siku hizi michezo ni biashara, hasa mpira wa miguu.
“Kwa nyie mliopo hapa Uingereza, mna jukumu kubwa la kuchukuwa yale mazuri yote yanayofanya EPL kuwa nzuri na kuyapeleka nyumbani Tanzania.

“Huwezi kusema hatuna vipaji nyumbani, tupo zaidi ya Watanzania milioni 40, lazima tuna vipaji vilivyojificha sehemu mbali mbali za nchi, nataka tupendekeze nini kifanyike ili katika mipango ya muda mrefu na kati, tuwe na wachezaji katika ngazi ya juu, hili linawezekana kabisa,” akasema Mheshimiwa Balozi Kallaghe.

Alisema kinachomuumiza zaidi ni kwamba Tanzania ina Rais mpenda michezo, Jakaya Kikwete ambaye amekuwa akitumia muda wake
mwingi katika masuala ya kuhakikisha nchi inafanya vizuri, lakini inaelekea hasaidiwi.

“Na sasa tujaribu kumsaidia kwa kutoa mapendekezo ya kuboresha michezo kwa mfumo tulio nao, angalau kwa mipango ya muda mfupi, badala ya kulaumu tu,” Balozi akatoa mwongozo kwa wadau.
Mmoja wa wadau walioshiriki mkutano huo ni Athumani China, mchezaji mstaafu wa Yanga na Simba na Taifa Stars.
China aliwagusa wengi, ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Balozi, pale alipotoa kwa maandishi, programu yake ya muda mrefu.

China aliandaa programu hiyo pamoja na wataalamu wa soka wa hapa Uingereza kwa msaada wa maofisa wa ubalozi wetu hapa.

Anasema kwamba aliufikisha mpango huo kwa Rais Kikwete, na baadaye kuangaliwa na aliyekuwa Waziri Wa Michezo wa wakati huo, Joel Bendera. Baada ya Bendera kupangiwa kazi nyingine, waziri aliyemrithi hapo wizarani ni Dk. Emmanuel Nchimbi na sasa yupo Dk. Fenella Mukangara.
Hatimaye, anasema China, ni kwamba mpango huo ulikufa rasmi. Ulikuwa mpango uliolenga kuwaleta vijana wetu hapa Uingereza kwa awamu wafundishwe.

“Ilikuwa tuwaweke katika mazingira ya kuwafundisha jinsi watu wa huku wanavyoishi na ustaarabu wao, kabla hawajaingia katika timu za huku kwa majaribio.

20130907-095818.jpg
Mutani Yangwe, Athumani China.

“Hata mimi mara ya kwanza nilipokuja kucheza hapa Uingereza nilishindwa kumudu, hali iliyosababisha nilipoenda nyumbani likizo nisirudi tena, najutia kupoteza ile nafasi, lakini halikuwa kosa langu, kwani sikuandaliwa vizuri,” anasema China ambaye bado yuko ‘fit’.

Anasema kwamba kuna mbinu wanazotumia kufundishia nk, ambapo lazima vijana wetu waelekezwe, kwani mambo yamebadilika sana.

Kadhalika, mifumo ya soka nayo imebadilika, kwani sasa soka si tu kumiliki mpira, bali mchezaji lazima ajue vitu vingi, ikiwa ni pamoja na sayansi ya mpira wa miguu, kauli iliyoungwa mkono na Mheshimiwa Balozi Kallaghe.

Mapema Mkurugenzi Wa TSC Academy ya Mwanza, Mutani Yangwe alielezea uzoefu wake katika kukuza vipaji katika academy yake.
Yangwe alielezea mafanikio na mipango yao ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na ushiriano alio nao na timu za QPR, na Arsenal za hapa Uingereza.

Mheshimiwa Balozi Kallaghe aliisifu TSC kuwa ni mfano wa kuigwa, na akataka mafanikio hayo yaigwe na taasisi nyingine nchini.

Alisema kufanya hivyo kutatoa ushindani utakaopelekea kuwa na vijana wengi wataokuwa na sifa za kuja kufanya majaribio huku na kwingineko nje ya Tanzania.

Naye Musema Amuri, mkazi wa hapa Uingereza ambaye asili yake ni Kigoma, aliweka wazi mipango yake ya kuanzisha vituo vya michezo katika Kanda ya Ziwa, kwa lengo la kuwaleta pamoja vijana, kupitia michezo. Alimkabidhi Mhe Balozi nakala ya mipango yake.

Mwingine aliyehudhuria ni Bwana John Osunsami, ambaye ni Mtaalamu wa Michezo kutoka kampuni ya New Vision Entertainment, inayowaangalia baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa kama Rio Ferdinand, John Terry, Antoine Ince na wengineo.

Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

Huyu alisema kwamba hajawahi kufikia Tanzania, ila anafahamu sifa za vivutio vilivyopo huko nyumbani.
“Kwa kutumia vivutio hivyo sambamba na michezo tungeweza kufanya vizuri sana, nashauri kuwekwa utaratibu mzuri, ili wataalamu kutoka kampuni yangu kwa kushirikiana na Athuman China waende Tanzania kipindi cha mashindano.

“Wakienda hawa wataagalia vipaji vya vijana wachache, kwa kuanza nao, kisha tutatengeneza utaratibu wa kuwaleta hapa, kwa msaada wa vilabu,” akasema.

Mheshimiwa Balozi Kallaghe alisema kwamba ana mialiko kutoka baadhi ya academy za hapa Uingereza, lakini kabla ya kwenda alitaka ajifunze kipi kifanyike isije ikawa kituko, kwani ubora wa vijana wadogo walioko kwenye academy za hapa ni mkubwa sana.

“Tulikwenda Sunderland na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, tulistaabishwa sana na uwezo mkubwa wa wale watoto, kuna wengine ni wadogo wa miaka 11 tu, lakini thamani yao inaelezwa kuwa ni pauni nusu milioni!” Balozi akawajuza wadau.

Jambo jingine alilosisitiza Balozi ni nidhamu kwa wachezaji, akisema hawawezi kupata mafanikio Kama hawana nidhamu.

“Na hapa nazungumzia nidhamu ya mchezo, umakini, saikolojia, na ujue kuwa mpira sasa ni kazi na ni biashara, ni vizuri ukazingatia yaliyo bora, Kama lishe nzuri na kuwa mfano kwa wengine. Huwezi kuja kucheza Ulaya kama huna nidhamu. Hutafanikiwa!” alisisitiza Mheshimiwa Balozi Kallaghe.

Alionesha wazi kukerwa na tabia za utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanamichezo na kuwataka waoneshe uwajibikaji kwa lolote lile wanalotakiwa kufanya, kwenye fani yao, na huku wakiwa na uchu wa mafanikio maishani.

Mheshimiwa Balozi aliwashukuru wate waliifika na kuahidi kuwaita tena, wakiwa wengi zaidi ili kupata mawazo zaidi na hatimaye kujaribu kufanya jambo litakalopelekea kuwa na angalau wachezaji wachache kwa ngazi yoyote ile ya soka hapa Uingereza.

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Spurs, Man U walimzuia Ozil kutua Arsenal

STARS YAMALIZA VIBAYA MECHI ZA KOMBE LA DUNIA