in , , ,

Arsenal ndio Manchester United mpya  

 
* Man U wamechacha kama Liverpool ya 1990

*Lukaku aliyeitwa garasa anathibitisha ubora

*Krismasi kuwa chungu kwa baadhi ya timu
 
Kwa miaka 20 iliyopita ilikuwa kawaida kuona timu zikipepesuka nyuma ya Manchester United, zikiachia mabao ya kipuuzi, zikishindwa kufunga mabao na kupoteza kabisa mwelekeo dakika tano za mwisho.

Zikiisikia Man United basi wachezaji wake walicheza kwa hofu iliyoonekana wazi nyusoni mwao kana kwamba ni timu isiyotakiwa kufungwa au kupitwa kwenye msimamo wa ligi.

Lakini sasa inaonekana kwamba uwapo wa Arsenal dimbani unawakata maini wapinzani wao ambao hupoteana na kwa Jumamosi hii, walipata ushindi wa nane wa msimu huu.

Ilionekana dhahiri kwamba licha ya uimara wa kiungo cha Arsenal na kujituma kitimu kwa ujumla, makosa mawili – moja kutoka kwa kipa wa Southampton, Arthur Boruc na jingine kwa beki Jose Fonte yaliwamaliza vijana hao waliotokea kuwa bora.

Kipa Boruc alifanya jambo la ajabu kujaribu kupitisha mpira karibu kabisa na mshambuliaji wa kati wa kimataifa, Olivier Giroud ambaye hakufanya ajizi, akampokonya na kutikisa kamba.
Bao jingine lilitokana na Fonte kutoa penati ambayo haikuwa lazima kwa kumvuta kwa nguvu jezi beki wa Arsenal, Per Metersacker aliyekuwa anataka kufunga.

Ni muongo mmoja sasa tangu Arsenal waoneshe timu ngumu isiyotikisika, ile iliyoitwa ‘Invincibles’ msimu wa 2003-04 ambapo hawakufungwa hata mechi moja.

Sasa yaelekea Arsene Wenger amegundua mbinu bora za kuipaisha timu yake na kuwatisha wapinzani katika karibu kila mechi, anaongoza ligi na pia anatamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa ni pamoja na kuwafunga kwao Borussia Dortmund.

Anaonesha kiwango cha Manchester United ya Alex Ferguson wakati huu ambapo Mskochi huyo amestaafu na kurithiwa na mwenzake, David Moyes.
 
 
MANCHESTER UNITED NI LIVERPOOL MPYA
 
Ni mapema mno kukata shauri na hata kulinganisha Wekundu wa Liverpool wa msimu wa 1990-91 na Mashetani Wekundu (Manchester United) wa 2013-14.

Kujiuzulu kwa kocha wa Liverpool, Kenny Dalglish msimu ule kulishuhudia klabu ikimpoteza kocha wao shujaa na kumaliza miongo miwili ya Liver kuitawala Ligi Kuu ya England.

Kujiuzulu kwa Ferguson kumeshuhudia klabu ikimpoteza shujaa na mkongwe na inaelekea kumaliza nguvu ya klabu hiyo kwa kama miongo miwili iliyopita.

Katika misimu miwili mizima baada ya kujiuzulu Dalglish, Liverpool walimaliza ligi wakiwa nafasi ya sita.

Siwatishi Manchester United, lakini kwa mwenendo wao msimu huu si ajabu Mei mwakani, ligi itakapomalizika, nao wakawa wameikalia nafasi ya sita ya msimamo wa ligi.

Kinachotia wasiwasi zaidi ni aina ya mechi zenyewe wanazopoteza au kwenda sare. Jumamosi iliyopita ilikuwa dhidi ya timu ndogo iliyopanda daraja msimu huu tu – Cardiff City.
Fergie hangekubali kabisa kupoteza mechi kama hii, angekuwa na uhakika na pointi zake tatu bila kujali walicheza vizuri au vibaya kiasi gani.

Jumapili Mashetani Wekundu walionekana wa kawaida sana, tena wakafanana kiuchezaji na timu hiyo ya Wales inayoongozwa na Kocha Malky Mackay.

Wamepoteza sifa muhimu walizokuwa nazo chini ya Fergie – kufunga mabao ya kusawazisha au ya ushindi katika dakika tano au hata sekunde za lala salama. Wao ndio waliachia ushindi ukawaponyoka dakika hizo!
 
 
VILLAS-BOAS ASHIKILIE PLANI ‘A’
 
Kwa zaidi ya nusu ya kwanza ya mechi kati ya Tottenham Hotspur dhidi ya Manchester City Jumapili hii, Spurs walifanya kazi kwa mazoea.

Walimudu kumiliki mpira kwa asilimia 60 dhidi ya 40 za City lakini wakashindwa kabisa kugeuza udhibiti huo kuwa mabao.

Kocha Andre Villas-Boas hakuamini macho yake kuona nyavu za vijana wake zikitikiswa mara sita bila majibu na sasa washabiki wa London Kaskazini wanataka hatua za haraka kurekebisha hali hiyo.

Mafuriko ya Etihad dhidi ya Spurs yalikuwa makubwa na kudhihirisha kwamba Villas-Boas angekuwa sawa akiendeleza uhafidhina wake.

Alijaribu kutupa karata tofauti Jumapili hii alipomchezesha Erik Lamela tangu mwanzo; akajaribu tena kamari ya kubadili mfumo baada ya nusu ya kwanza kwa kucheza 4-4-2 na hapo viungo wake waliusikia tu mpira.

Mbaya zaidi alimpa Emmanuel Adebayor dakika 45 nzima za kucheza wakati alionesha uhai katika sekunde 45 tu.

AVB alishauriwa kujaribu mpango tofauti na wa awali kwa vile washambuliaji wake wameshindwa kuwa tishio langoni mwa maadui na hata akipata ushindi unakuwa wa matuta, lakini sasa, bora arudie alikokuwa kwenye ‘plan A’.
 
LUKAKU ANAWEZA KUAMUA UBINGWA
 
Msimu uliotangulia watu walishangaa kuona Chelsea wakimpeleka Romelo Lukaku kwa mkopo West Bromwich Albion alikoibuka mfungaji bora.

West Brom waliomba wabaki naye msimu huu, wakakataliwa lakini Jose Mourinho akamtoa tena kwa mkopo kwa Everton, na sasa anaonesha kiwango kikubwa kuliko washambuliaji wa ‘The Only One’.

Lukaku alipoza nyoyo za wana Everton baada ya kuwasha moto, kufunga na hatimaye timu hiyo kwenda sare ya 3-3 dhidi ya Liverpool kwneye derby ya Merseyside.

Mbelgiji huyo anaonesha vitu adimu ambavyo alitakiwa aachwe Stamford Bridge avioneshe, maana bila yeye Everton wangezikwa mapema na Liverpool wenye mwendo wa kasi msimu huu.

Sasa anachofanya Lukaku ni kuchomoa pointi tatu au moja moja kutoka kwa wapinzani wa Chelsea katika kuwania taji.

Hata hivyo, kwa kuwa hatacheza dhidi ya Chelsea, basi Mourinho anafurahia tu, labda Everton wapande hadi nafasi ya kwanza na kuwashinda Chelsea.
 
MAN CITY WAFUNDISHE WACHEZAJI WAO , ULIMAJI BUSTANI
 
Ilikuwa kitu cha kusisimua na kusikitisha kwa wakati mmoja pale vijana wa Manuel Pellegrini wakiwaharibu Spurs kwa 6-0.

Furaha ilikuwa wazi kwa jinsi wachezaji walivyocheza pamoja kuwasababishia mateso wenzao kana kwamba alikuwapo uwanjani Lionel Messi kufunga mabao yale mazuri.

Lakini uchungu ulikuwa jinsi City wanavyocheza vyema wakiwa nyumbani lakini wanakuwa hovyo ugenini.

Ni sawa na kumuoa mwanamitindo mahiri unayempenda muda wote lakini anakataa kutoka nawe nyumbani kwenda kujirusha na marafiki badala yake anajificha kwenye makabati pindi marafiki zao wakifika.

Sasa City wafanyeje? Wakae na wachezaji wao kuanzia sasa na kuwaeleza kwamba kila dimba la soka kwenye ligi hii lina urefu wa yadi kama 115 na upana wa yadi 75 hivi.

Kwamba viwanja vyote vimetengenezwa kwa majani kama zilivyo bustani nzuri na kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya dimba la nyumbani na ugenini, kwa hiyo kwa nini wafunge mabao 26 nyumbani halafu wanakwenda kutandikwa na Sunderland au Cardiff? Woga na aibu ugenini vinatoka wapi?

 
KUTAKUWA NA KRISMASI FULHAM?
 
Kocha Martin Jol wa Fulham ana wakati mgumu kwa sababu Jumamosi hii wakicheza nyumbani kwao Craven Cottage, Fulham walipoteza mechi.

Mdachi Jol huwa haelekei kubabaika lakini huenda akawa kocha anayefuata kupoteza kibarua hasa kwa kuzingatia kwamba atakaokabiliana nao hivi karibuni ni AVB wa Spurs, Chris Hughton wa Norwich.

Ikiwa Fulham watashindwa kuwapiga West Ham Jumamosi ijayo basi ni wazi kwamba Jol atajielekeza kukabidhiwa fomu yake ya P45.
 
VITA YA KUSHUKA DARAJA IMEANZA SASA
 
Klabu zilizo kwenye nusu ya chini ya msimamo wa ligi zinacheza zikiwa na mawazo yasiyo sahihi kwamba ni timu mbili tu zitashushwa daraja.

Kwa kuwa Crystal Palace walishaonekana wadhaifu kupindukia kabla hata ya msimu kuanza, basi wamewabatiza kuwa watashuka wao.

Lakini wikiendi imewashuhudia wakiwafunga Hull 1-0 na si ajabu ukawa mwanzo wa mabadiliko na kushangaza kwa kuzipiga timu nyingine hata kubwa kama Sunderland walivyowapiga Man City.

Maana kocha mpya, Tony Pulis alikuwa amekaa na washabiki tu baada ya kuteuliwa na vijana wakatoka na ushindi, itakuwaje akikaa kwenye benchi?
Kwa hiyo vita ya kushuka daraja si ya timu tatu za mkiani, bali na nyingine za juu yao zinazosuasua, lakini pia tusisahau kwamba timu tisa za juu zinatenganishwa na pointi nane tu, vita hii ni kubwa kuliko inavyochukuliwa.
 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

  Arsenal wang’ang’ania usukani EPL

KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI