in , ,

ZIMBWE ANGUSHA USO KABLA HUJAENDA MVANGE

Inawezekana ndiye alikuwa mchezaji bora na muhimu katika kikosi cha
Simba msimu uliopita.

Aliifanya kazi yake bila kupumzika, kila mechi mguu wake ulikanyaga
kila nyasi ya viwanja vyote vilivyoruhusiwa kwa ajili ya ligi kuu
Tanzania bara.

Lakini kwa sasa muda umechukua nafasi ya kufanya mabadiliko muda ni
nafasi ya mabadiliko.

Na mabadiliko ndicho kitu ambacho maisha hutoa kwa mwanadamu, huwezi
kukwepa na kuzuia mabadiliko kama maisha yameamua kutoa nafasi kwa
muda, ingawa mara nyingi mabadiliko huja na ukinzani mkubwa

Kinachobaki ni wewe kuchagua kitu kimoja kuangalia muda au kuangalia
saa, kwenye muda kila sekunde kuna badiliko jipya hujitokeza wakati
mwingine huitaji kuangalia saa kujua muda umekuacha.

Nafasi uliyopo sasa ndiyo hutoa jibu sahihi kuwa muda umekuacha au
unaenda sambamba na muda.

Inawezekana msimu jana Mohammed Hussein “Zimbwe jr” alikuwa kwenye
nafasi kubwa ya mafanikio lakini changamoto zikaja na upepo wa
kumshusha chini ya mafanikio aliyoyafikia na kuwepo kwenye nafasi
ambayo anatakiwa kukumbushwa kuwa muda unanyata taratibu kuelekea
mbele yake ili umpe kisogo.

Inauma kuona kipaji cha Zimbwe kikiachwa na muda ndiyo maana kuna haja
ya kumkumbusha kuwa muda haumsubiri mtu.

Najua kwa sasa anachangamoto kubwa ya kurejea kwenye kiwango baada ya
kutoka kwenye majeruhi, lakini changamoto kubwa kwake ni kufanikiwa
kumweka benchi Asante Kwasi, mchezaji ambaye amekamilika zaidi kuliko
Zimbwe.

Asante Kwasi ambaye anaonekana amepata mambo baada ya kupata fimbo,
waweza ukadhani labda fimbo yake aliyoipata anaitumia kumwadhibu
Zimbwe kwa sababu ana vitu vingi ambavyo Zimbwe hana

Ushawahi kuwaangalia usoni Zimbwe na Kwasi wanapokuwa wanashambulia?
Kuna vitu viwili utaviona kwenye mwili wao, cha kwanza ni kasi kubwa
ya Zimbwe dhidi ya ƙkasi ya kawaida ya Kwasi. Cha pili ni utulivu
hafifu wa Zimbwe dhidi ya utulivu mkubwa wa Asante.

Pamoja na kwamba Zimbwe anaposhambulia huwa anashambulia kwa kasi
lakini hukosa utulivu kama wa Asante anapokuwa anashambulia.

Ndiyo maana maamuzi yao ya mwisho huwa yanatofautiana kwa kiasi
kikubwa, mfano msimu jana Zimbwe alifanikiwa kutoa pasi mbili za
magoli wakati kwa mechi ambazo amecheza Asante Kwasi akiwa na jezi ya
Simba ambazo hazifiki kumi ameshahusika kwenye magoli zaidi ya mawili.

Hii yote inaonesha nani hupania kufanya kitu kizuri na nani hudhamiria
kufanya kitu bora, na ndiyo maana Asante kwasi ana magoli 6 kwenye
ligi kuu mpaka sasa.

Ni mtulivu anapokuwa katika eneo la kumi na nane, haoni ugumu kujivua
sura yake na kujivika sura ya Okwi anapokuwa eneo hili, ni mara
chache sana kupata mchezaji ambaye ni beki mwenye uwezo wa kufunga
magoli na kutoa pasi za mwisho, hii kwenye mpira ni vitu muhimu vya
nyongeza ambavyo Zimbwe hana ingawa akiamua anaweza kuvipata.

Utulivu pekee ndicho kitu kinachokosekana kwenye macho na akili ya
Zimbwe, waweza kumuona anahusika kwenye kujenga mashambulizi ya timu
lakini linapokuja suala la yeye kutoa maamuzi ya kuzalisha goli
kukuangusha ni kitu cha kawaida.

Na ugumu wa kumbeba mbele ya Kwasi ndipo unapoanzia, nafsi yako lazima
uiruhusu kumwelewa Kwasi na kumpa nafasi zaidi ya Zimbwe kujifunza.

Yupo kwenye umri wa kujifunza kwa sasa, umri unaompa nafasi ya kusoma
mambo mengi ambayo atayatumia kwa baadaye.

Umri ambao haumruhusu yeye kususa kukaa benchi, umri ambao unamruhusu
yeye kupigana na kuumia kwanini anakaa benchi?

Umri unaompa nafasi kubwa ya yeye kujihoji maswali mengi ya kwanini?

Kwanini yeye siyo mtulivu anapotakiwa kufanya maamuzi ya mwisho kwenye
eneo la hatari la adui( final third)?

Kwanini Kwasi ni mzuri zaidi yake kipindi anapobaki na mshambuliaji wa
timu pinzani kumkaba ( one to one battle)?

Kwanini Kwasi huwa anaziba nafasi eneo la beki wa kati kushoto kwa
uharaka kipindi ambacho beki wa kati kushoto anapokuwa ameondoka
kwenda kutimiza jukumu jingine la ukabaji?

Maswali chanya yanatakiwa yatawale katika kichwa chake, akubali
kuipokea hali iliyopo kwa sasa na kutozipa nafasi fikra hasi zitawale
katika kichwa chake.

Asikubali kuendelea kusimama, kwani asimamaye haendi mbio, anatakiwa
kujua ashapitwa na Kwasi anatakiwa aende mbio na kutoka sehemu ambayo
yupo kwa sasa.

Siyo muda sahihi kwake yeye kuanza kulaumu kwanini Mungu aliumba Chui,
anachotakiwa kushukuru kuwa Chui hakuumbwa na mabawa kisha aanze
kutetea nafasi yake kwa sababu cha mchama huchachama, cha mgura
hugura.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

WILSHERE, KALAMU YENYE FURAHA NA MWANDISHI MWENYE MAUMIVU

Tanzania Sports

MAHADHI WAKUMBUKE MAZEMBE UJIFUNGE MASOMBO