USHINDI wa mabao 5-0 waliopata Yanga dhidi ya wana Lizombe, Majimaji kutoka Songea mkoani Ruvuma umeifanya klabu hiyo ya mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es salaam kuweka rekodi ya aina yake katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo ulichezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwapa raha washabiki na wapenzi wake ambao wanaamini kuwa watatwaa ubingwa mbele ya Azam, Simba, na Mtibwa ambazo zinachuana vikali kuwania taji hilo.

Yanga imekuwa gumzo kubwa miongoni mwa wapenzi wa soka kutrokana na kasi yake msimu huu ambayo imeweza kuweka rekodi za kutisha ambazo hazijawekwa na timu yoyote kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Timu hiyo imefikisha pointi 39 sawa na Azam FC, lakini kasi ya safu yake ya ushambuliaji katika kupachika mabao inaonekana kuzitisha timu mbalimbali zinazoshiriki ligi hiyo.

Safu hiyo inayoongozwa na washambuliaji Amis Tambwe(raia wa Burundi), Donald Ngoma (raia wa Zimbabwe), Simon Msuva, Malimi Busungu, Deus Kaseke na Paul Nonga imeweza kutupia nyavuni jumla ya mabao 36 na kuizidi Azam yenye mabao 30.

Idadi hiyo ya mabao ni rekodi mpya katika historia ya Ligi Kuu ya Bara kwa timu kuiweka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ambapo hakuna timu iliyoweza kufikisha mabao hayo katika nusu ya mzunguko wa ligi.

Yanga imeweka rekodi nyingine nyingi ikiwemo ya kuwa na mshambuliaji anayeongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi kwa mzunguko wa kwanza ambaye ni Amis Tambwe.

Nyota huyo kutoka Burundi alipachika mabao matatu Alhamisi iliyopita na kufikisha jumla ya mabao 13 katika mechi 15 alizocheza katika mzunguko wa kwanza, alipofunga mabao matatu ‘Hat Trick’ katika mechi dhidi ya Majimaji, Yanga iliposhinda 5-0.

Idadi hiyo haijawahi kufikishwa na mchezaji yeyote katika mzunguko wa kwanza na Mrundi huyo anaonekana kumkimbia Hamis Kiiza wa Simba mwenye mabao 10.

Hat Trick hiyo ni ya pili msimu huu na ya saba kwake tangu aanze kucheza soka Tanzania mwaka 2013 na kumfanya aweke rekodi ambayo huenda ikachukua muda mrefu kufikiwa.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga kwa ujumla ndiyo inayoongoza kwa kuwa na watu wanaotisha zaidi katika suala zima la kucheka na nyavu kwani ukijumlisha mabao ya Tambwe na Mzimbabwe Ngoma ambayo ni 22 unaweza kukaribia idadi ya mabao yote 23 waliyofunga mahasimu wao Simba katika idara zote.

Katika idara ya kiungo, Yanga pia imetisha kwani kiungo wake Thaban Kamusoko(raia wa Zimbabwe) ameweza kung’ara katika mzunguko huu wa kwanza akipachika mabao matano na kutoa pasi za 5 za mabao katika mechi 14 alizocheza.

Safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa imara kwa kuruhusu mabao machache mno. Mabeki wake Nadir Haroub, Kelvin Yondani , Vincent Bossou (raia wa Togo), Juma Abdul, Haji Mwinyi na Mbuyu Twitte wamekuwa katika kiwango cha juu kwa kudhibiti washambuliaji hatari.

Kipa wa Yanga Deogratius Munishi  amecheza dakika 630, katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Bara hajaruhusu nyavu za lango lake kutikiswa.

Wakati golikipa mwingine Ali Mustapha ‘Barthez’ kabla ya kuwekwa benchi mwishoni mwa mwaka jana alikuwa amefungwa mabao matano.

Kipindi cha miaka 10 iliyopita tangu mwaka 2006, Yanga inaongoza kwa kutwaa taji la ubingwa ikiwa imefanya hivyo mara sita ikifuatiwa na Simba iliyofanya hivyo mara tatu, huku Azam FC ikilitwaa kwa mara ya kwanza mara moja.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TUNAPOINGIA JUMA LA 24 LA LIGI YA ENGLAND ?

Tanzania Sports

Goran Kopunovic anukia Simba