in , , ,

YANGA YAWANYOOSHA APR JIJINI KIGALI

 

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamepata ushindi wa 2-1 dhidi ya APR ya Rwanda jioni hii ndani ya dimba la Amahoro jijini Kigali.

Ni Juma Abdul na Thabani Kamusoko waliofunga mabao ya Yanga huku lile la APR likitumbukizwa na Patrick Sibomana ndani ya dakika za mwishoni za mchezo.

Juma Abdul alikuwa wa kwanza kuwainua mashabiki wa Yanga kwa bao la kuongoza kupitia shuti kali kutoka kwenye mpira wa adhabu, shuti lililomuacha golikipa Kwizera Janvier akiruka bila mafanikio huku mpira ukitinga wavuni.

Dakika mbili baadaye Bernabe Mubumbyi akatishia kusawazisha bao baada ya kuunganisha kwa kichwa safi krosi ya Iranzi. Hata hivyo Ally Mustapha akadaka kichwa kile dhaifu bila bugudha.

Nahodha wa APR Iranzi Jean Claude naye akamjaribu Ally Mustapha kwa shuti kali lakini golikipa huyo nambari moja wa Yanga akaonesha tena umahiri wake kwa kuudaka mpira ule.

APR wakafanya shambulio lingine hatari sekunde chache kabla ya kipenga cha mapumziko kwa krosi kali Rusheshangoga iliyookolewa na Mwinyi Haji na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.

Yanga wakatoka kifua mbele kwenye kipindi cha kwanza wakiongoza kwa bao moja kwa sifuri.

Ndani ya dakika 10 za mwanzo za kipindi cha pili APR walijaribu kushambulia zaidi lakini Yanga walifanikiwa kuyazima mashambulizi hayo mapema.

Ndani ya dakika ya 55 shuti kali la Sibomana lililokuwa likielekea wavuni baada ya kumpita golikipa Ally Mustapha aliyekuwa amesogea mbele kidogo ya mstari wa goli likaokolewa vyema na kiungo Patro Ngonyani.

APR waliendeleza mashambulizi mfululizo wakijaribu kusawazisha bao lakini juhudi zao hazikuweza kuzaa matunda huku wakipoteza nafasi kadha ya wazi ikiwemo ya Bernabe ndani dakika ya 65.

Mshambuliaji huyo wa APR alipaisha mpira uliomjia miguuni ndani ya eneo la hatari baada ya kona iliyopigwa na Iranzi kuokolewa na Ally Mustapha.

Thabani Kamusoko akawapatia Yanga bao la pili mnamo dakika ya 74 akimalizia kazi nzuri ya Donald Ngoma. Golikipa Kwizera alijaribu kuokoa shuti lile dhaifu lakini bado mpira ukaingia taratibu ndani ya goli.

APR waliendeleza mashambulizi wakijaribu kusawazisha huku wakipata kona ya saba ya kipindi cha pili ndani ya dakika ya 81 lakini kona hiyo pia ikashindwa kuwapa matunda yoyote.

Dakika tisini za mchezo zilimalizika matokeo yakiwa bado 2-0 lakini APR wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Patrick Sibomana.

Mchezo wa marudiano utapigwa jijini Dar-es-salaam wiki ijayo ambapo mshindi wa jumla atakutana na mshindi baina ya Libolo ya Angola au Al-Ahly ya Misri.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ulivyo uwezekano wa Arsenal ama Man City kutwaa taji la EPL

Tanzania Sports

Chelsea nje Kombe la FA