in , ,

YANGA INAWAZA VIZURI , INATEKELEZA KAWAIDA

YANGA INAWAZA VIZURI , INATEKELEZA KAWAIDA

Tulizoea kupata vitu kutokana na hisani ya mtu ili macho yetu yaweze kushuhudia jua likizama na kukaribisha giza.

Maisha yetu yalikuwa yanamtegemea mtu kutuletea mwanga ili tupate nuru, kuna wakati magoti yetu yalichubuka sana wakati tunaomba msaada kwa hawa watu.

Hatukuona haya kutembeza bakuri la mchango ili tupate kuwalipa kina Obrey Chirwa, tuliona ni jambo la kawaida kwa sababu hata waliokuwa wanatupa pesa walituaminisha ni jambo la kawaida ndiyo maana kila tulipokuwa tunawaomba walikuwa wanatupa pesa bila kutuachia wazo la kutafuta pesa ili tujitegemee.

Wazo la kujitegemea halikuwepo kwenye vichwa vyetu, hakuna aliyefikiria kujitegemea, hatukutaka kabisa kupitia ugumu wa kujitegemea

Kila mtu alikuja kuiongoza timu akiwa na malengo ya muda mfupi, malengo ambayo hayakumpa uhuru wa kujenga misingi ya kujitegemea.

Misingi ya kujitegemea hutokana na utashi wa mtu hasa hasa anapokuwa na malengo ya muda mrefu.

Ukali wa jua hutofautiana sana, ukali wa jua la leo unaweza kukusahaulisha mipango yako ya jana ya kutonunua mwamvuli.

Kuna vitu lazima uvifanye kutokana na hali halisi au kutokana na nyakati ulizopo kwa kipindi hicho. Tupo katika nyakati ambazo timu zinatakiwa zijiendeshe kibiashara bila kutegemea kumpigia magoti mtu ili atoe pesa yake mfukoni bila biashara yoyote inayofanyika kati yenu.

Yanga waliliona hili, wakaamua kuja na mawazo mengi sana ambayo waliona ni mawazo ambayo yatawapa kipato mbadala.

Nilimsikia na kumwelewa vizuri sana katibu mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa alipokuwa anatoa mpango wa wanachama kuichangia timu elfu moja kila mmoja kwa njia ya mtandao.

Lilikuwa wazo bora sana ambalo wengi walilibeza, Dismas Ten alikuja na wazo la jarida la Yanga.

Wazo ambalo lilionesha Yanga inaelekea kwenye njia ya kujiendesha kisasa kulingana na mahitaji ya dunia ya sasa huku ikijiingizia kipato kikubwa.

Wiki kadhaa zilizopita walitangaza mambo mawili makubwa sana, jambo la kwanza lilikuwa kutambulisha huduma kwa wanachama kupata habari za klabu kwa njia ya simu kwa gharama ya shilingi mia.

Wazo lilikuwa zuri sana, kimahesabu lina manufaa makubwa sana kutokana na matokeo makubwa.

Yanga kwenye hili wazo wanauwezo wa kutengeneza kiasi kikubwa cha pesa kama kutakuwepo na msukumo mkubwa

Msukumo ambao ulihitajika pia hata kwenye matangazo ya Yanga kuhusu kipindi chao kipya kitakachokuwa kinaruka Azam TV.

Tangu watangaze kuna kipindi kinakuja, hakuna kitu kikubwa kinachofanyika ili kuwapa hamasa mashabiki wa Yanga kusubiri kwa hamu kipindi hiki.

Kila kitu kinachofanyika kwenye matangazo ya kipindi hiki kinafanyika katika hali ya ukawaida.

Ukipita katika ukurasa wao wa Instagram na kuona matangazo waliyoweka hayana ushawishi wa kumshawishi mtu asubiri kwa hamu ƙkipindi hiki.

Kuna wakati uwekezaji wa akili na muda kuliko uwekezaji wa pesa, kuna vitu havihitaji pesa nyingi ili kufanya kitu kikubwa.

Yanga walitakiwa kutafuta waandishi wa mswaada (script writers) ambao wangeandika muongozo wa tangazo litakavyokuwa kisha wawakabidhi waongozaji, washika camera na watu wengine watakaohusika kwenye tangazo hili.

Watu wa Graphics wangemalizia kupendezesha tangazo hili kwa kuweka vitu ambavyo vingevutia, tofauti na sasa tangazo linaonekana halina mpangilio mzuri wala hakuna kinachovutia au kutia hamu mtu asubiri kipindi cha Yanga TV kwa hamu kubwa.

Kuanzisha kitu haimanishi umemaliza kila kitu, unatakiwa ufanye msukumo mkubwa sana ili kufikisha sehemu ya juu kitu ambacho umekianzisha.

Katika dunia hii ya sasa unatakiwa ufanye kila kitu kibiashara ili umvutie mteja wako awe mteja bora wa bidhaa yako.

Bidhaa nyingi wanazoleta Yanga hazifiki mbali kwa sababu hakuna msukumo mkubwa wa kuzitangaza, wanaamini wanachama watanunua bila kuwakumbusha au kutafuta wateja wapya.

Hii dunia ya kibiashara unatakiwa ufikirie namna ya kutengeneza wateja ambao ni loyal

Utengeneze wateja wapya kila siku ili biashara yako ikue.

Yanga wamekuja na bidhaa nzuri sana, kuja na biashara nzuri sokoni haimanishi kuwa tayari umeifanya biashara hii kuwa kubwa na imara sokoni.

Kabla ya bidhaa haijaanza kuingia sokoni kuna mazingira ambayo yanatakiwa kutengenezwa ili kuonesha kuwa kuna bidhaa bora na ya kuvutia inakuja .

Unanivutiaje mteja mimi ili niwe loyal kwako au niisubiri kwa hamu bidhaa yako??

Rahisi! Matangazo yanayovutia ili yanivute ili nipate hamu ya kusubiri bidhaa yako.

Kuna wakati watu waliisubiri Seduce Me ya Alikiba kwa hamu siyo kwa sababu walimkumbuka sana, ila uwekezaji wake wa muda na akili kutuambia nawaletea bidhaa mpya.

Lile tangazo lililowekwa kwenye ukurasa wa Instagram likimuonesha Katibu mkuu akiwa onset kila kitu kimefanyika kawaida kuanzia camera, camera man, mtu wa sauti yote kwa yote script ya kawaida. Script ndicho kitu cha muhimu lakini hakikuwekewa mkazo wa kutosha.

Yanga wasitegemee tu kuwa kipindi chao kitaangaliwa tu kwa sababu ina mashabiki wengi, wanatakiwa wakifikirie kuendesha kila kitu kibiashara hata kama wanamtaji mkubwa wa wateja.

Hebu mfanye hata shabiki wa Simba atamani kipindi cha Yanga TV kianze. Wekeza muda wako unishawishi mimi shabiki wa Simba niweke tarehe ya kipindi cha Yanga TV kwenye kitabu changu cha kumbukumbu za kila siku.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

YANGA WAMETUPA TULICHOKUWA TUNAKITAKA

Tanzania Sports

AUBAMEYANG AMEANZA KUANDIKA REKODI: DALILI NJEMA KWA ARSENAL