in , ,

Yanga hawakusajili mbadala wa Makambo na Ajib

Ibrahim Ajibu Yanga

Hapa ndipo pakuanza kupata jibu la swali letu la kwanini Yanga mpaka sasa hivi inafanya vibaya kwenye ligi kuu Tanzania bara? Ligi ambayo miaka ya nyuma muda kama huu Yanga ilikuwa kwenye harakati za ubingwa.

Hiki kitu ni tofauti kabisa kwa mwaka huu, Yanga ishakata tamaa na ubingwa. Haipo tena kwenye mbio za ubingwa kiuhalisia ingawa kimahesabu Yanga ipo kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara.

Mashabiki wamechoka , mioyo yao imekata tamaa. Kocha Luc Eymael haoni kama Yanga haina nafasi tena ya kuchukua ligi kuu ya Tanzania bara, kwa kifupi Yanga wameshamaliza msimu kwa sasa. Lakini swali kubwa la kujiuliza tatizo liko wapi?

Yanga msimu uliopita chini ya mwalimu Mwinyi Zahera ilikuwa na wachezaji wawili muhimu na bora katika kikosi chao, wachezaji ambao kwa mabega yao waliibeba Yanga pamoja na kwamba hawakuwa vizuri kiuchumi.

Yanga ilikuwa na Ibrahim Ajib ambaye alikuwa na pasi za magoli zaidi ya 20 kwenye ligi kuu ya Tanzania bara ndiye mchezaji ambaye alitoa pasi nyingi za magoli kwenye ligi kuu ya Tanzania bara.

Pamoja na kwamba Ibrahim Ajib alikuwa anatoa pasi nyingi za magoli, pia Ibrahim Ajib alikuwa anatengeneza nafasi nyingi za magoli katika eneo la mwisho la Yanga.

Kwa sasa Yanga inaonekana haipigi pasi nyingi kwenye eneo la tatu ya mwisho ya uwanja (final third) kutokana na kukosekana na kiungo ambaye ni msambazaji mzuri wa mipira na ambaye pia ni mbunifu.

Ukiangalia viungo wa Yanga wa msimu huu hakuna kiungo ambaye ana pasi hata tano za mwisho za magoli kwenye ligi kuu Tanzania, hii inaonesha pengo kubwa lililoachwa na Ibrahim Ajib.

Viungo wa sasa wa Yanga hawasambazi mipira mingi mbele kama kipindi ambacho Ibrahim Ajib alipokuwepo . Asilimia kubwa Yanga inacheza katika eneo lake la uwanja.

Pia Ibrahim Ajib alikuwa siyo mtengenezaji pekee wa magoli, pia alikuwa mfungaji mzuri wa magoli. Msimu jana alikuwa na magoli zaidi ya Saba kwenye ligi kuu Tanzania bara.

Lakini kwa sasa hakuna kiungo wa Kati wa Yanga ambaye ana magoli zaidi ya matatu kwenye ligi kuu Tanzania bara. Kwa hiyo kuondoka kwa Ibrahim Ajib kumesababisha Yanga ikose magoli takribani 30.

Ukimzungumzia Ibrahim Ajib lazima umtaje Makambo , mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita. Mchezaji ambaye alikuwa na magoli zaidi ya 15. Lakini kwa sasa Yanga haina mshambuliaji maalumu kwenye kikosi chake.

Leo atapangwa Taariq Seif, Kesho Yikpe, kesho kutwa David Molinga au Ditram Nchimbi. Hakuna ambaye amesimama kama mshambuliaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha Yanga kutokana na viwango vyao kuwa vya kupanda na kushuka.

Mpaka sasa hivi mshambuliaji ambaye anaongoza kwa ufungaji bora kwenye safu ya ushambuliaji kwenye kikosi cha Yanga ni David Molinga mwenye magoli 7. Mtu ambaye pia anaonekana kutokuwa na nafasi katika kikosi cha Yanga.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mvutano Corona soka ya EPL

Tanzania Sports

BALAA LA VIRUSI VYA CORONA: